Waziri
 Mkuu, Kassim Majliwa akisalimiana na wapigakura wke baada ya kuwasili 
kijijini kwake Nndagala wilayni Luangwa kwa mapumziko mafupi Desemba 20,
 2015. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*Asema wabadhirifu watang’olewa mara moja
*Asema wako wasomi wengi wanaotafuta ajira
WAZIRI
 MKUU Kassim Majaliwa amewaonya watendaji wa halmashauri nchini kwamba 
atakayebainika ametumia vibaya fedha za Serikali atang’olewa kazini kwa 
sababu Serikali ya Awamu ya Tano haina mchezo na mtu.
  Ametoa
 kauli hiyo leo mchana (Jumapili, Desemba 20, 2015)  wakati akizungumza 
na mamia ya wananchi waliofika kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara 
uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Ilulu uliopo Lindi mjini.
  “Natoa
 onyo kwa watendaji wote wa halmashauri. Fedha ya Serikali itakayotumwa 
kwenu halafu mtu aifanyie ubadhirifu,  ole wake. Yeyote atakayebainika 
kuzitumia kwa ubadhirifu fedha hizi tutamng’oa. Wako wasomi wengi huko 
nje tena wazuri tu, wanasubiri kupata ajira.”
  “Nataka
 watumishi wa umma watambue kwamba Serikali ya Awamu ya Tano 
inajielekeza kujali wananchi.  Wao wana dhamana ya kuwasilikiliza na 
kuwahudumia wananchi ili kuhakikisha wanatatua kero zinazowakabili, ” 
alisema huku akishangiliwa na wengine wakisema huyu sasa ni Sokoine wa 
pili. (Edward Moringe Sokoine alikuwa ni Waziri Mkuu katika Serikali ya 
Awamu ya Kwanza).
  Waziri
 Mkuu ambaye amewasili Lindi leo, aliwaeleza wakazi hao kwamba amekuja 
kuwashukuru wazee na wana Lindi kwa dua zao na kuwaahidi kwamba 
hatawaangusha Rais John Pombe Magufuli na Makamu wake Samia Suluhu 
Hassan kwa kumuamini na kumpa dhamana ya kuwatumikia Watanzania katika 
ngazi ya Uwaziri Mkuu.
  Waziri
 Mkuu pia alimpa kazi Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Jordan Rugimbana ya 
kuhakikisha anaufufua uwanja huo na kuurudisha kwenye enzi yake 
ulivyokuwa maarufu katika mikoa yote ya Kusini. “Uwanja huu lazima 
uboreshwe kwa sababu unanikumbusha mwaka 1984 wakati nachezea timu ya 
Amri Rangers.  Kulikuwa na ukoka wa nguvu hapa uwanjani. Kwa hiyo timu 
aliyoiunda Mkuu wa Mkoa itafanya kazi lakini pia iwajumuishe Meya na 
mbunge wa Lindi Mjini kwa sababu huu uwanja ni mali ya Halmashauri ya 
Lindi, ” alisema.
Akielezea
 kuhusu mipango ya Serikali kuendeleza sekta ya viwanda, Waziri Mkuu 
alisema hivi karibuni mkoa huo utapata wawekezaji kwenye sekta ya gesi 
baada ya kampuni ya BG kutoka Uingereza kupata umiliki wa eneo la 
Kikwetu ili wajenge mitambo ya kusafisha gesi.
Aliwataka
 wananchi wa mkoa huo wawekeze kwenye ujenzi wa hoteli na nyumba za 
kulala wageni ili ifikapo Agosti mwakani, watu wanaokuja kushiriki 
maonyesho ya NaneNane kitaifa mkoani humo wasipate taabu ya malazi kama 
ambavyo imekuwa ikitokea huko nyuma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni