Baadhi
ya wenyeviti toka Halmashauri ya wilaya ya Kishapu wakimsikiliza
mkufunzi (hayupo pichani) wakati wa mafunzo ya uraghabishi
yaliyofanyika wilayani hapo
Na Krantz Mwantepele
“Unakuja
kwenye ofisi yangu na kutoa taarifa za ubadhirifu wa mtendaji wa
kijiji. Nakuuliza, je umechukua hatua zipi kama kiongozi wa kijiji kabla
kuja kwenye ofisi yangu? Unanijibu hapana, hii si sahihi,”
Hayo
ni maneno ya mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Hashim Mgandilwa, aliyoyatoa
wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya wenyeviti wa vijiji, watendaji wa kata
na vijiji kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Loliondo, mwezi
Agosti mwaka huu.
Alisema
hayo kwa lengo la kufafanua dhana ya uwajibikaji kwa viongozi kama njia
muhimu ya kutatua kero zinazowakabili wananchi wa maeneo ya vijijini
katika wilaya yake.
Ni dhahiri kwamba viongozi wa ngazi za vijiji na kata wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiutendaji katika maeneo husika.
Kuna
nafuu kwa watendaji wa kata na vijiji, ambao ni waajiriwa wa serikali
na hupewa kazi kutokana na miongozo, lakini siyo kwa wenyeviti wa
vijiji na madiwani, wakati mwingine hata wabunge.
Akielezea
changamoto hiyo wakati wa mafunzo ya wenyeviti wa vijiji kupitia mradi
wa Chukua Hatua yaliyofanyika Septemba mwaka huu na shirika mdau la
CABUIPA, mwenyekiti wa kijiji cha Nyakafulu kilichopo wilaya ya Mbogwe,
mkoani Geita, Salum Said amesema:
“Baada
ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa kijiji hiki, hakika sikufahamu vya
kutosha kuhusu majukumu yangu mapya kama kiongozi. Na hii ni changamoto
kubwa kwa wenyeviti wa vijiji karibu vyote vya wilaya yetu.”
Yeye ni mmoja kati ya wenyeviti 200 wanaopatiwa mafunzo katika mikoa ya Shinyanga, Geita na Simiyu.
Hii ni
kutokana na ukweli kwamba, katika awamu ya kwanza ya mradi wa Chukua
Hatua, nguvu kubwa iliwekwa katika kuwawezesha wananchi kuwachukulia
hatua watendaji na viongozi wabadhirifu wa mali za umma.
Wakati
wananchi wakiwezeshwa kuwasimamia viongozi wao, viongozi hawakuwa
wakiwezeshwa kutimiza majukumu yao kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi
wao. Hivyo, haja ya kutoa mafunzo kwa viongozi hao ili waweze kutimiza
majukumu yao kwa wananchi waliowachagua, ilikuwa lazima.
Akielezea
umuhimu wa kuwawezesha wenyeviti wa vijiji wakati wa uzinduzi wa
mafunzo ya wenyeviti na watendaji wa kata Julai 2015, mkurugenzi
mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, Jane
Mutagurwa alisema:
“Kwa
muda mrefu wenyeviti mmekuwa mkilalamika kusahaulika kwenye programu
zetu za mafunzo, fursa ndio hii imekuja. Tunafahamu kwamba wenyeviti
wetu mnakutana na changamoto nyingi za kiutendaji zinazotokana na
uwelewa mdogo katika majukumu yenu, hasa kwa wale wanaoingia madarakani
kwa mara ya kwanza. Hivyo mtumie mafunzo haya vizuri.”
Pamoja
na umuhimu wa mafunzo hayo kwa viongozi wa ngazi ya kijiji na kata,
bado imekuwa ni changamoto kubwa kwa serikali kuwawezesha wenyeviti
kujua majukumu yao. Na hii inatokana bajeti kuwa na vipaumbele vingine
ambavyo halmashauri huwa wamejiwekea katika kutimiza majukumu yao."
Kwa upande wa Ngorongoro, mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya hiyo mkoani Arusha anaeleza:
“Tangu
tulipofanya uchaguzi mwaka jana hatujawahi kutoa mafunzo kwa wenyeviti.
Kwa hiyo tunaunga mkono mafunzo haya yanayotolewa na PALISEP yatasaidia
sana kwenye kuwawezesha viongozi hawa na watendaji wetu,”
Kutokana
na hali hii, wenyeviti wamekuwa na changamoto za kuelewa mipaka ya
majukumu yao, hivyo muda mwingine hujikuta kwenye mzozo na watendaji wa
vijiji vyao. Mwenyekiti anawajibika kwa mwananchi aliyemchagua, wakati
mtendaji anawajibika kwa mkurugenzi aliyemwajiri.
Kutokana
na tofauti hizo, mafunzo ya sasa ya wenyeviti na watendaji yanaendeshwa
kwa pamoja kuwafanya waelewe mipaka yao ya kiutendaji, hivyo kuboresha
utendaji wao.
Afisa
Programu wa CABUIPA, Michael Ikila anafafanua: “Tunawafundisha vitu sita
muhimu; taratibu za uendeshaji serikali za mitaa, majukumu na haki za
wenyeviti wa vijiji, uwajibikaji na utawala bora, mamlaka za vijiji,
masuala ya fedha, ikiwamo uandaaji wa bajeti na mawasiliano mazuri
baina ya viongozi wa vijiji.”
Mada hizi ni kwa mujibu wa mwongozo wa wizara ya Tawala za Mikoa and Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Majukumu
mengine ya wenyeviti hawa ni pamoja na kuhamasisha shughuli za
maendeleo, utawala na kuhakikisha usalama wa watu katika maeneo yao kwa
kushirikiana na watendaji wa kata na vijiji.
Kwa
upande wa Wilaya ya Ngorongoro, hii ni mara ya kwanza kwa wenyeviti
kufundishwa majukumu yao. Mwanzoni mafunzo haya yaliwalenga madiwani
ambao kimsingi hawakuyapenda kwa sababu ya kutokuwapo kwa posho. Hivyo
mafunzo yao yakaamishiwa kwa wenyeviti wa vijiji ambao walipokea mwaliko
kwa furaha pasipo kudai posho.
“Mafunzo
haya yatatusaidia kuboresha mahusiano na utendaji wetu. Mara kadhaa
unakuta wenyeviti wanaingilia mipaka yetu ya kazi, hivyo kuathiri
uhamasishaji wa shughuli za maendeleo. Na hii hutokea pale mwenyekiti
mpya anapotaka kuwaonyesha wapigakura wake kwamba mwenzake aliyepita
hakufanya kazi,” anaelezea mmoja wa watendaji wa kijiji aliyehudhuria
mafunzo hayo.
Pamoja
na changamoto hizo, bado washiriki ambao ni wenyeviti, watendaji wa
kata na vijiji wamekiri kwamba mafunzo hayo yatakuwa chachu ya kumaliza
tofauti zinazojitokeza baina yao.
Lakini
si hivyo tu, viongozi wa wilaya wameonyesha kuunga mkono mafunzo hayo
kwa kuwa yanasaidia kuhamasisha wananchi kutimiza majukumu yao.
Lakini
pia viongozi hao walionyesha umuhimu wa kufikia wajumbe wengi zaidi ya
halmashauri za serikali ya kijiji. Kwa mfano, wakati akizungumza na
wakufunzi kwenye ofisi yake, mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya
Kishapu, alisema:
Halmashauri
ya Wilaya ya Kishapu ina jumla ya vijiji 117 vyenye wajumbe 2,925. Kwa
mantiki hiyo, mafunzo haya yanayoendeshwa kupitia mradi wa Chukua Hatua
yamefikia asilimia 4 tu ya wajumbe wanaounda uongozi wa serikali za
vijiji, hivyo wengi bado wanahitaji mafunzo. Katika mazingira hayo,
mkurugenzi alitoa ombi maalumu la kusaidiwa kuwawezesha wakufunzi 25 wa
wilaya watakaotoa mafunzo kwa wajumbe wa halmashauri za vijiji hivyo.
Gharama za wakufunzi hawa kuwafikia wajumbe wengine zitakuwa ni za
serikali.
Na huu
ni ushirikiano unaotakiwa baina ya sekta ya umma na binafsi kwa kuwa ni
jukumu letu sote kwa mustakabali wa maendeleo yetu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni