Serikali imeridhishwa na maendeleo na kasi ya ujenzi wa
Mahakama ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa ya Masalia ya kesi za Mauaji
ya Kimbari ya Rwanda (Mechanism for International Criminal Tribunals
(MICT) katika eneo la Lakilaki jijini Arusha, uliozinduliwa rasmi Julai
mosi mwaka huu.
Akikagua ujenzi huo na
kupokea taarifa kutoka kwa wakandarasi na wasimamizi wa ujenzi wa
majengo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Kikanda na Kimataifa Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, amesisitiza kuwa
ujenzi huo uzingatie viwango vya kimataifa ili kuhakikisha usalama wa
nyaraka na ushahidi utakaohifadhiwa kwenye majengo hayo.
Alieleza kuwa
ahadi ya Serikali iko palepale kushirikiana na Umoja wa Mataifa na
kuhakikisha kuwa miundombinu muhimu kama vile barabara, umeme na maji
vinapatikana kwenye eneo hilo ambapo ujenzi unaendelea kwa kasi ya
kuridhisha.
“Nimefurahishwa na maendeleo ya ujenzi huu kwani
hii ilikua kazi yangu ya mwisho nilipokuwa mwakilishi wa kudumu wa
Tanzania kule Umoja wa Mataifa, kutetea mahakama hii ijengwe hapa
Arusha.
Akifafanua miundombinu
iliyowekwa na Serikali ya Mkoa wa Arusha, Katibu Tawala Msaidizi upande
wa miundombinu Nd. Hamdouny Mansour alisema kuwa kwa upande wa
upatikanaji wa maji, mkoa umefanikisha upatikanaji wa bomba maalum
linaloleta maji kwenye eneo la ujenzi mojakwamoja bila kuathiri
upatikanaji wa maji maeneo mengine pembezoni ili kutimiza azma hiyo ya
Serikali.
Ujenzi huo wa Mahakama
unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa unatarajiwa kuwa na majengo makuu
manne; jengo la mahakama, jengo la uhifadhi wa nyaraka, jengo la ulinzi
na jengo la ofisi za Umoja wa Mataifa. Msimamizi wa ujenzi wa Umoja wa
Mataifa alielezea teknolojia ya kisasa itakayotumika kujenga jengo la
kuhifanyia nyaraka haitahitaji kutumia viyoyozi ili kuhifadhi uhasilia
wa nyaraka.
Kwa upande wa wakandarasi
wanaojenga ambao ni kampuni kutoka India walielezea changamoto iliyopo
kwenye ujenzi huo ni kutekeleza mpango wa kupanda mti aina ya
mshita-acacia, utakaomaanisha haki ambayo kihistoria na jadi za kiafrika
ilipatikana kwa mazungumzo kwenye mabaraza ya kijiji. Mti huo wa mshita
au Tree of Justice utapandwa ndani katikati ya majengo hayo manne.
Serikali kupitia Hazina
ilinunua eneo hilo la Lakilaki lenye ekari 431 na kukabidhiwa Wizara ya
Mambo ya Nje ambapo limetengwa mahsusi kwa ajili ya ujenzi wa taasisi
mbalimbali za kimataifa. Taasisi nyingine zinazotarajiwa kujengwa kwenye
eneo hilo ni African Union Advisory Board on Corruption (AUABC),
African Institute of International Law (AIIL) na African Court on Human
and Peoples' Rights
(ACHPR).
Ujenzi wa majengo haya ya
awali kwenye eneo la Lakilaki unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili
mwakani. Ujenzi huo ulizinduliwa rasmi Julai mwaka huu wa 2015 na Rais
wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.MWISHO.
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali kwa Umma, Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni