WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amepiga marufuku chakula cha msaada kutumiwa
kutengeneza pombe za kienyeji na kwamba atakayekamatwa atachukuliwa
hatua za kinidhamu.
Ametoa
kauli hiyo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya
hadhara iliyofanyika leo (Jumatatu, Desemba 21, 2015) kwenye vijiji vya
Nangurugai, Machang’anja na Narungombe katika kata za Mbwemkuru na
Narungombe wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Waziri Mkuu alikuwa
akijibu hoja za diwani wa Narungombe, Bw. Rashid Nakumbya aliyetoa ombi
la kuongezewa chakula cha msaada kwa sababu wana hali mbaya. Alisema
msimu uliopita haukuwa mzuri kiuzalishaji kutokana na hali mbaya ya
hewa. Pia aliomba wasaidiwe kuboreshewa huduma za maji safi na salama.
“Natambua kuwa kuna tani 2,000 za chakula zimeletwa katika mkoa wetu
lakini hizo hazitoshi kwa sababu mahitaji yetu ni zaidi ya tani 5,000.
Chakula hiki hakitoshi kwa sasa lakini kitasaidia kupunguza makali ya
njaa,” aliwaeleza wakazi hao.
“Tumepiga marufuku kutumia
chakula cha msaada kupikia pombe. Mwananchi atakayekutwa akitumia
chakula hicho, atachukuliwa hatua za kinidhamu,” alisisitiza.
Alitumia fursa hiyo kuwahakikishia kauli ya Rais Dk. John Pombe Magufuli
kwamba hakuna mwananchi atakayekufa kwa njaa. “Mheshimiwa Rais ameahidi
kuwa hakuna Mtanzania atakayekufa kwa njaa. Tuna mahindi ya kutosha
kwenye maghala ya Songea, Dodoma na Makambako lakini changamoto ni namna
ya kuyasafirisha kutoka huko hadi kuyafikisha huku. Tunaendelea pia
kupeleka misaada kwenye mikoa mingine,” alisema Waziri Mkuu.
Akijibu hoja nyingine zilizotolewa, Waziri Mkuu ambaye pia ni mbunge wa
jimbo hilo alisema anatambua changamoto walizonazo za ukosefu wa maji
safi, ubovu wa barabara, zahanati na nyumba za waganga na kwamba ameanza
kuzishughulikia.
“Hivi sasa nimeanza kushughulikia suala la
uwekaji wa nishati ya umeme wa jua kwenye shule za msingi na zahanati.
Mtaalam ameshafika hapa wilayani kwetu na ameanza hiyo kazi, na hivi
karibuni mtamuona akifika maeneo ya huku,” alisema.
Kuhusu
maji safi na salama, Waziri Mkuu aliwaeleza wakazi hao kwamba tatizo la
maji analijua na kwamba changamoto kubwa waliyonayo ni upatikanaji wa
chanzo cha maji baridi kwani kiasi kikubwa eneo hilo lina vyanzo vya
maji yenye chumvi. “Wataalamu wanakuja kutafuta chanzo cha maji baridi
kwa sababu asilimia kubwa ya eneo hili maji yake yana chumvi,” alisema.
Aliwataka wakazi hao waendelee kuwaombea yeye pamoja na Rais Magufuli
na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan ili waweze kutimiza malengo
waliyoahidi kwa Watanzania wakati wa kampeni.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni