Meneja wa Kituo cha kulelea watoto yatima cha Nuru Orphance Centre, Amanda Fihavango akiwa mbele ya vitu vilivyotolewa kama msaada na msamaria mwema kutoka nchini Marekani. |
Dynes Macha akiwa amemshika mtoto mchanga zaidi kati ya watoto wanaolelewa katika kituo cha Nuru |
Dynes Macha akiwakabidhi watoto msaada wa vitu mbali mbali kwa niaba ya rafiki yake anayeishi nchini Marekani Vida Katamba |
Watoto wa wanaolelewa katika kituo cha Nuru wakifurahia msaada wa vitu mbali mbali baada ya kukabidhiwa, wengine kwenye picha ya pamoja ni Joseph Mwaisango wa pili kulia. |
Watoto wakifurahia msaada |
Mmoja wa Walezi na wahudumu wa kituo cha Nuru akigawa juisi kwa Watoto |
Joseph Mwaisango ambaye ni mmiliki wa Blog ya Mbeya yetu akifurahia jambo na watoto wanaolelewa katika kituo cha Watoto Yatima cha Nuru. |
SERIKALI ya Awamu ya tano chini
ya Rais Dk. John Magufuli imeombwa kuviangalia kwa ukaribu vituo vya kulelea
watoto yatima kwa kuvipatia ruzuku ili viweze kujiendesha vyenyewe tofauti na
hivi sasa vinategemea misaada kutoka kwa wasamaria wema.
Rai hiyo ilitolewa na Meneja wa Kituo cha kulelea watoto yatima cha Nuru Orphans Centre,
Amanda Fihavango kilichopo Uyole jijini Mbeya alipokuwa akipokea msaada kutoka
kwa wasamalia wema ambao ni Watanzania wanaoishi nchini Marekani.
Meneja huyo alisema Kituo hicho
chenye watoto 26 kati yao wavulana 10 na
wasichana 16 wenye umri kuanzia wiki
moja hadi miaka 10 wanakabiliwa na ugumu wa uendeshaji wa shughuli za kila siku
ikiwa ni pamoja na vyakula pamoja na fedha za kuwalipa wahudumu wanaokaa na
watoto hao.
Alisema watoto waliopo kituoni
hapo mara nyingi hupelekwa baada ya kutelekezwa na mama zao mara baada ya
kujifungua hali inayopelekea kuwa waangalifu katika kuokoa maisha yao kwani
wengine hupokelewa wakiwa wamejeruhiwa kutokana na kutupwa.
Meneja huyo aliongeza kuwa
baadhi ya watoto hupelekwa na baba zao baada ya mama kufariki dunia akiwa
anajifungua hivyo humsaidia baba kulea ambapo huruhusiwa kumchukua baada ya
kukua na kufikisha miaka miwili.
Aidha alitoa wito kwa wazazi
hususani vijana kuacha tabia ya kuwapeleka watoto wachanga kwa bibi zao kwani
asilimia kubwa wanakosa malezi bora kutokana na walezi hao kuwa na hali mbaya
ya kiuchumi hivyo kushindwa kutoa huduma stahiki kwa motto mchanga na badala
yake wawe na utaratibu wa kuwapeleka kwenye vituo vinavyotambulika.
Alisema changamoto kubwa
inayokikabili kituo hicho mbali na ukosefu wa fedha ni uhaba wa viatu na mavazi
kwa watoto wakubwa kuanzia miaka mitano hadi kumi kutokana na gharama kubwa ya
nguo zao tofauti na watoto wachanga ambao hupatiwa misaada kiurahisi.
Alisema changamoto nyingine ni
ukosefu wa uzio kukizunguka kituo hicho kwani huhatarisha maisha ya watoto
ikiwa ni pamoja na kuibiwa vitu, kushindwa kuweka vifaa vya kuchezea na
kushindwa kuwadhibiti watoto wengine kutoroka kutokana na kuwa watundu kupita
kiasi.
Akizungumza baada ya kukabidhi
msaada huo kwa niaba ya Rafiki yake ambaye anaishi Marekani, Vida Katamba,
Dynes Macha alisema wametoa msaada huo kama ishara ya kusherekea sikukuu za
Krismas na Mwaka mpya pamoja na watoto yatima.
Macha alivitaja vitu
vilivyopelekwa kuwa ni pamoja na Unga wa ngano kilo 25, unga wa sembe kilo 25,
mafuta ya kupikia lita 10, sukari kilo 20,sabuni ya unga kilo 15,sabuni ya mche
boksi moja,mchele kilo 40,chumvi ndogo katoni moja,mafuta ya kupaka dazani moja
na nusu,sabuni za kuogea dazani 2, juisi dazani mbili na pipi kopo moja.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni