Daktari Bingwa wa Masuala ya Usingizi na Wagonjwa
Mahututi Vence Sakwari akijadili jambo na mwenyeji wake katika Hospitali ya
Mkoa wa Kagera kabla ya kuanza kutoa huduma kwa wagonjwa wake.
|
Sehemu ya wagonjwa wakisubiri kuelezwa utaratibu
wa kuwaona madaktari bingwa waliofika hospitalini hapo.
|
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Michael Mhando
akikabidhi msaada uliotolewa na Mfuko kusaidia zoezi la huduma za Madaktari
Bingwa. Msaada huo ni pamoja na vifaa tiba, dawa na mashuka 300.
|
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Michael Mhando akimsalimia mmoja wa wagonjwa
ambaye tayari alikuwa kwa Daktari Bingwa wa njia za mkojo na vibofu.
|
Wananchi wakiwa na shauku ya kukutana na
madaktari bingwa
|
Wagonjwa wakiendelea kusubiri kutolewa kwa
utaratibu wa namna ya kuonana na madaktari bingwa ambao wameanza rasmi huduma
leo katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera.
|
Wagonjwa wakiwa kwenye foleni ya kuonana na
daktari
|
Wagonjwa wakiwa kwenye foleni ya kuonana na
madaktari kulingana na matatizo yao.
|
Daktari Bingwa wa Watoto Dr. Kabibi Byabato
akiwa na watoto tayari kwa kuwahudumia .
|
MFUKO wa
Taifa wa Bima ya Afya umesema hautawavumilia watumishi katika hospitali ya Mkoa
wa Kagera wanaojihusisha na vitendo vya kughushi nyaraka za kuchukulia dawa
katika maduka ya dawa na kuusababishia Mfuko kulipa fedha ambazo hazijatumika
kihalali.
Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Bw. Michael Mhando ameyasema hayo mjini hapa
wakati akizungumza na uongozi wa Hospitali ya Mkoa wa Kagera kabla ya uzinduzi
wa mpango wa Madaktari Bingwa ambao wamepelekwa na Mfuko huo kutoa huduma kwa
wanachama na wananchi kwa ujumla.
“Niseme tu
kwamba tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali zikiwemo za kuwaonya kwa barua na
wengine kuwafutia usajili na wengine kuwafikisha mahakamani watoa huduma ambao
wanajihusisha na vitendo vya udanganyifu lakini niseme kwamba kwa hospitali hii
natangaza rasmi kuwa kuanzia sasa naanza kuchukua hatua kali kwa watumishi
ambao watabainika kujihusisha na udanganyifu wowote,”,” alisema Bw. Mhando.
Alisema kuwa
Mfuko unalo jukumu la kulinda fedha za wanachama wake na kuhakikisha zinatumika
katika matumizi sahihi hivyo hauko tayari kuendelea kuvumilia watoa huduma
ambao sio waaminifu.
“Nawaomba
sana toeni huduma kwa wanachama wetu na sio kutumia vitambulisho vyao kughushi
nyaraka mbalimbali zikiwemo za kuchukulia dawa katika maduka ya dawa…sisi tuko
tayari kusaidia kituo chochote katika uboreshaji wa huduma zake ili wananchi
wanufaike kwa ujumla na sio kikundi cha watu wachache,” alisema Bw. Mhando.
Katika hatua
nyingine aliitaka Hospitali hiyo kuangalia namna ya uboreshaji wa huduma zake
hususan upatikanaji wa dawa ambao umeonekana kuwa tatizo kubwa linaloikosesha
mapato hospitali hiyo.
Alisema kuwa
mpaka sasa Hospitali ya Mkoa wa Kagera imekuwa ikipoteza mapato mengi kutokana
na ukosefu wa dawa na vipimo ambavyo ndivyo vinaingiza fedha nyingi katika
vituo vya kutolea huduma hali ambayo inakwamisha uboreshaji wa huduma.
“Mapato
mnayopata kwa kweli niseme kwamba hayalingani na ukubwa ama huduma mnazopaswa
kuzitoa nah ii inasababishwa na ukosefu wa dawa na huduma zingine hivyo
hakikisheni mnaboresha haya maeneo ….Mfuko uko tayari kushirikiana na nyie ili
kuifanya hospitali iwe na huduma nzuri kwa ajili ya Watanzania…mapato kidogo
yanawanyima fursa ya kunufaika na mikopo yetu hivyo naomba hili eneo mlifanyie
kazi kwa maslahi yetu sote,” alisema Bw. Mhando.
Kwa upande
wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera Dr. Thomas Rutachunzibwa aliunga mkono
kuchukuliwa kwa hatua zozote kwa wanaojihusisha na udanganyifu ili kuleta
nidhamu ya kazi katika maeneo yao.
Alitumia
fursa hiyo kuupongeza Mfuko kwa jitihada mbalimbali ambazo imekuwa ikifanya
katika kusogeza huduma kwa wateja ikiwemo ya kupeleka madaktari bingwa katika
hospitali hiyo.
“Kitendo cha
kutuletea wataalam hapa kwanza kitasaidia kuongeza mapato yetu lakini pia
utaalam utakaoachwa kwa watumishi wetu hapa utaendelea kutumika hivyo
tunawashukuru sana,” alisema.
Mwisho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni