Bwana Bony Lukas akieleza jinsi anavyofanya uraghbishi hasa katika kuwasaidia vijana kujua haki zao na kujitambua.
Na Fredy Njeje wa Blogs za Mikoa.
Ni
suala ambalo lipo wazi kuhusu tofauti za kimaisha baina ya wakazi wa
mijini na vijijini, ila changamoto nyingi zaidi zinaonekana kuwakabili
zaidi wale wanaoishi vijijini. Huko wananchi wanakosa huduma ambazo
kimsingi ni haki zao na hivyo kutokuwa na usawa baina yao na wale wa
mijini.
Picha
kubwa inayojionesha vijijini kwa upande wa wanawake ni hasi kwa kiasi
Fulani ukilinganisha na ile ya wanaume. Usawa wa kijinsia na kielimu
baina yao na wanaume ni mkubwa sana, kesi za unyanyasaji kwao ni nyingi
zaidi. Pamoja na jihudi nyingi za kuwawezesha wanawake bado hawajapata
nafasi ya kutoshwa kuweza kusikilizwa. Wanaume wameendelea kuwa watoa
maamuzi na wanufaikaji wa kimfumo.
Mmoja wa waraghbishi akiwa anaonesha ripoti ya wanafunzi watoro katika shule ya msingi ya Nyandekwa .
Takwimu
zinaonesha kuwa hata idadi ya ufauru kwa wasichana kwa Shule za msingi
imeongezeka ambapo mwaka 2013 wasichana waliofaulu ni 281,460 sawa na
asilimia 50.20 ya wanafunzi 560,706 wakati wavulana waliofaulu ni
279,246 sawa na asilimia 49.80. Kabla ya ya matokeo wasichana waliofanya
mtihani walikuwa 456,082 sawa na asilimia 52.68 na wavulana 409,745
sawa na asilimia 47.32. Mwaka 2014 jumla ya watahiniwa 808,085 wa shule
za msingi Tanzania wasajiliwa kufanya mtihani huo wakiwemo wasichana
429,624 sawa na asilimia 53.17 na wavulana 378,461 sawa na asilimia
46.83. Jumla ya watahiniwa 451,392 kati ya 792,118 walifanya mtihani,
wasichana waliofauru ni 226,483 ambao ni sawa na asilimia 53.59 na
wavulana 224,909 sawa na asilimia 46.41.
Mraghishi Mariam Stephano (katikati) akieleza jambo wakati wa kikao.
Katika
nchi yetu ya Tanzania kuna makabila zaidi ya 100 na kila moja likiwa na
mila na tamaduni zake. Ni vizuri ikaeleweka kwamba wazee wetu hawakuwa
wakichangamana kimakabila hivyo ni watu wachache walikuwa wanahama toka
sehemu moja kwenda nyingine. Aina hii ya maisha ilipelekea wengi wao
kuoana wa kabila moja, tofauti ikiwa ni vijiji ama kata, ila wengi
ilikuwa toka mkoa ama wilaya moja.
Tofauti
na sasa ambapo watu wanachanganyikana kutokana na shughuli za kiuchumi
na kijamii. Hali hii ya kuchanganyikana baina ya makabila ndani ya mkoa
ama wilaya ama kijiji kimoja imeleta tamaduni tofauti na zile ambazo
zilikuwa zimezoeleka kiuchumi na kijamii.
Pamoja
na mchanganyiko huo bado kumekuwa na changamoto nyingi sana
zinazowakabili wakazi wa vijijini. Bado wanaishi kwenye lindi la
umaskini na ukosefu mkubwa wa huduma za kijamii. Changamoto hizi
zinasababisha baadhi yao kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wanadai
na kusimamia haki za msingi za kijamii; hawa wanaitwa waraghbishi.
Waraghbishi
ni mtu mmoja mmoja ama kikundi cha watu ambao wamevutika kufanya
uraghbishi aidha kwa kufundishwa ama kwa kuona matokeo ya matendo
wanayofanywa na wanajamii wenzao. Hususani wale ambao wanachukua hatua
katika kustawisha au kulinda haki za binadamu na kuwakumbusha wenzao
majukumu yao kwa maslahi ya kijamii, kiuchumi ama kisiasa.
Matilda
Peter(wa pili kushoto) aliyeanza Uraghbishi 2015 akieleza namna
anavyofanya Uraghbishi kwa kuwapa elimu wasichana juu ya kujitambua, na
kuepuka mimba za utotoni
Moja
ya haki hizo ni zile za wanawake ambao kwa muda mrefu wameonekana kuwa
nyuma zaidi. Hali hii imewaondelea kujiamini na kujiona wao ni wa daraja
la pili na hivyo kutokuwa na sauti katika jamii zao.
Mmoja wa waraghbishi hao ni Bw. Bony Lukas toka kijiji cha
Nyandekwa wilayani Kahama katika mkoa wa Shinyanga. Mraghbishi huyu
ameweza kuelimisha watu wa kijiji chake.
Akielezea jinsi anavyoraghbisha vijana katika kijiji chao, Lukasi anasema:
“Vijana ndio wenye nguvu za kuweza kuleta maendeleo na ndio wenye
mchango mkubwa ndani ya jamii zetu. Kwa hiyo ni lazima wawe ni watu
wenye kujitambua katika nyanja zote. Ili waweze kupata nafasi mbalimbali
za kuweza kutoa mchango wa mawazo ili yaweze kufanyiwa kazi”
Hali inatokana na ukweli kwamba vijana wamekuwa nyuma kwa muda
mrefu bila. Uraghbishi kwao ni mrejesho wa nafasi finyu ambazo vijana wa
vijijini wamekuwa hawapewi nafasi ya kuweza kuchangia pindi wawapo
katika mikutano ya kimaendeleo ndani ya vijiji. Hii ilitoa nafasi ya
mraghbishi kupokea mawazo kutoka kwa vijana wa kike na wakiume kwani
vijiji vilivyo vingi hupuuza mchango wa mawazo ya mtoto wa kike na
kumuona hana thamani.
Kwa mantiki hiyo mraghbishi Lukasi aliweza kuwatia ujasiri kwa
kutoogopa kwani watakavyo kuwa na roho ya uoga ndio itakayo wafanya
wabaki nyuma kimaendeleo. Kuna msemo unasema “woga wako ndio umaskini
wako”. Hivyo alihakikisha anawawezesha vijana kujiamini na kushirikiana
vyema na uongozi wa kijiji.
Elimu ya jinsia pia ni tatizo katika vijiji vingi vya hapa
Tanzania ambapo mraghbishi Miriam Stephano yeye aliweza kutumia nafasi
hiyo kwa kuweza kuwaelimisha vijana kuhusu elimu ya jinsia. Akilielezea
hilo anasema:
“Hapa kijijini kuna vijana wa rika tofauti tofauti. Wapo wale
ambao ndio wanabalehe na wale waliovuka hiyo ngazi ya kubalehe.
Mabadiliko hayo ya kimaumbile hupelekea vijana wengi kuanza kuwa na
muelekeo usio sahihi. Sababu ikiwa ni mihemko inayo wakumba pindi wawapo
katika shughuli za kila siku hasa kwa wale wanao soma.”
Mraghbishi Bujika Adam Joseph kutoka kijiji cha Guduba akitoa
mchango wake wa namna alivyofanya uraghbishi kwa kuwahimiza vijana
kuhudhuria mikutano ya vijiji ili nao wapate kushiriki katika kutoa
mawazo na michango yao mbalimbali ya mawazo.
Vijana hawa katika kijiji hicho wanapata changamoto mbalimbali
zinazotokana na mabadiliko ya kimaumbile. Hili linapeklekea kupata mimba
za utotoni pamoja na maambukizi ya virusi vha Ukimwi. Hivyo kupitia
waraghbishi vijana hawa wamekuwa wakipewa elimu ili waweze kujikinga na
kujiepusha na hari zinakokuwa zikiendelea kuleta mabadiliko katika miili
yao.
Changamoto hii ndio iliyomplekea mraghbishi huyu mwanamke toka
kijiji cha Nyendekwa, wilayani Kahama Bi. Mariam Stephano kuraghbisha
kundi hili, kama anavyofafanua yeye mwenyewe:
“Nikiwa kama mwanakijiji mraghbishi huwa ninapita katika mashule
mbalimbali. Huko naomba ruhusa kwa mwalimu mkuu na kuweza kuzungumza na
wanafunzi wa kike jinsi gani wanaweza kushughulika na mabadiliko ya
miili yao. Nawaelekeza nini wafanye pindi wanapofikia umri wa kubalehe.
Hapo ntawafundisha usafi wa mwili na namna ya kukwepa vishawishi
vitakvyowapelekea aidha kupata maambukizi ya virusi vya Ukumwi ama mimba
za utotoni”
Elimu hii ya jinsia inawasaidia watoto katika kijiji cha
Nyandekwa, kwani wengi wao huanza kujitambua na kuwa na akili ya
kutafakari yale yaliyo mema na mabaya. Na pia inawasaidia hata upande wa
serikali katika dhana ya kupunguza maambukizi ya Ukimwi na magonjwa ya
zinaa.
Bi
Anna Zengu aliyepata uwenyekiti wa Kitongoji cha Busolwa kutokana na
Uraghbishi akielezea kwa kina jinsi alivyo wasaidia akina mama wenzake
kujitambua na kujua umuhimu wa kupiga kura na kuchagua viongozi bora
wanaofaa kuongoza Taifa.
Kwa upande wa mraghbishi Wilbert Michael kutoka kijiji cha Kakebe
wilayani Kahama yeye alifanya utafiti usio rasmi juu ya tabia za uongozi
wa kijiji chao. Hapo aliweza kugundua mambo kadhaa yaliyokuwa
yakifanywa na viongozi wa kijiji hicho pasipo kuwashirikisha na
wananchi. Na walifanya hivyo kwa maslahi binafsi.
Akielezea hali hiyo, Michael anasema:
“Kupitia uraghbishi nilionao niliweza kufuatilia mambo mbalimbali
katika ofisi ya kijiji pamoja na ile ya kata. Lengo ikiwa ni kubaini
tatizo lililokuwa linakabili kijiji. Kubwa likiwa ni viongozi kujali
maslahi binafsi, hapakuwa na uwazi kwenye mikataba ya kimaendeleo ya
kijiji,”
Swali la kujiuliza yeye mraghbishi alijuaje habari hizo, akijibu swali hilo ansema:
“Nililigundua kupitia mbao za matangazo ambapo walibandika tangazo
la kuingia kwa mkataba na watu wanao sambaza vyandarua vijijini na wao
kuchukua kama ni mradi wa kujipatia kipato. Kupitia mradi vijana
walitakiwa kugawa vyandarua hivyo, na hivyo ilikuwa ndio iwe ajira yao.”
Badala yake Mwenyekiti na Afisa Mtendaji wa kijiji wao wakawa
wanawachangisha vijana fedha kiasi cha shilingi elfu kumi (10,000) kwa
kila mmoja. Lengo lao likiwa ni kuwasajili kwa kuwa wasambazaji wa
vyandarua hivyo kinyume cha dhana nzima ya kuleta maendeleo kijini.
Na ndipo mraghbishi Michaeli alitumia uraghbishi wake kwa kuweza
kuwataarifu wananchi na ndipo wananchi walipoamua kumwajibisha
mwenyekiti huyo. Walichoamua ni kupeleka malalamiko katika ngazi
mbalimbali za kata na wilaya ili waweze kumvua madaraka yake na
kupendekeza jina la mweenyekiti mpya wanayemtaka na atakayeshirikiana na
wanakijiji.
Hii ni dhahiri kwamba bado wananchi wanaoishi vijijini wanahitaji
elimu ya kiraia itakayowawezesha kuwasilisha matatizo yao kwenye ngazi
husika. Ili nao waweze kuwasaidia wenzao wanapogundua yale yanayofanywa
na viongozi wao hayaendani na dhana ya ukweli na uwazi. Na piakuwa na
ujasiri wa kuweza kuongea sehemu mbalimbali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni