MKOA WA ARUSHA WANNE KWA KUFAULISHA KITAIFA

Image result for ufaulu kidato cha nneNa Mahmoud Ahmad Arusha.
JUMLA ya wanafunzi,27005   ambao wamehitimu elimu ya msingi mwaka 2015  mkoani  Arusha wamechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2016
Akitangaza  matokeo hayo, Kaimu katibu tawala mkoa wa Arusha,Hamdouny Mansour, amesema jumla ya wanafunzi 33898 walifanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi ambapo wavulana walikuwa ni 15868 na wasichana 18,030 .
Amekiambia kikao hicho kuwa waliofaulu walipata  alama kati ya 100 hadi 250 ambapo wavulana ni 12563 na wasichana ni 14 442 na ufaulu huo ni sawa na asilimia 79.67 ukilinganisha na mwaka 2014 ambapo kiwango cha ufaulu ilikuwa ni asilimia 67.69.
 
Alisema kuwa matokeo ya mwaka huu  yalikuwa  na lengo la ufaulu wa asilimia 80 ambapo ni malengo ya kitaifa chini ya mpango wa matokeo makubwa sasa BRN,katika sekta ya elimu nchini.
 
Alisema kimkoa ufaulu umeongezeka kwa asilimia 12 na nafasi ya mkoa kitaifa mkoa wa Arusha umekuwa wa Nne ,ambapo kwa halmashauri jiji la Arusha ndilo limeongoza ambayo imefaulisha kwa asilimia 92.7 ikifuatiwa na halmashauri ya Arusha DC,ambayo imefaulisha kwa asilimia 90.
 
Mounsour, alisema halmashauri ya Ngorongoro imekuwa ni ya tatu kwa kufaulisha asilimia 73.45, ikifuatiwa na halmashauri ya wilaya ya Monduli ambayo imefaulisha kwa  asilimia 70.6 Halmashauri ya Longido imefaulisha kwa asilimia 68.7 halmashauri ya Meru, imefaulisha kwa asilimia 67.5 na Karatu imeshika mkia kwa kufaulisha kwa asilimia 65.
 
Akazitaka halmashauri zote saba za mkoa huo kuhakikisha kila mwanafunzi aliyechaguliwa kujiunga na sekondari  anaripoti kwenye shule aliyopangiwa kwa wakati .
 
Watendaji wa kata na maafisa tarafa wahakikishe wanawatambua wanafunzi waliofaulu katika maeneo yao na kwenda shule walizopangiwa na wasiporipoti hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wazazi ambao hawatawapeleka watoto wao shuleni.
 
Katibu tawala huyo, ameziagiza halmashauri za jiji la Arusha, kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa vinavyoendelea kujengwa kabla ya mwezi Marchi mwakani kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza.
 
Aidha halmashauri ambazo ufaulu wake ni wa kiwango cha chini ziweke mkakati  namna ya kuinua kiwango cha elimu na ufaulu ambapo lengo la ufaulu kwa mwakani ni asimilia 85.
 
Pia ametumia fursa hiyo kuzipongeza kamati za mitihani  kutokana na kutokuwepo udanganyifu kabla na wakati wa kufanyika kwa mtihani na kuzishauri ziendelee kuwa makini wakati wa kuchagua walimu makini wanaosimamia mitihani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni