Katibu
Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Omar Chambo (wa kwanza kulia)
akiangalia moja ya mashine zinazotumika katika shughuli za uchimbaji
madini katika eneo la Mirelani mkoani Manyara wakati alipotembelea eneo
hilo mara baada ya kumaliza kikao kikao chake na Kamati za Ulinzi na
Usalama za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara ambazo zimeamua
kufanya kazi kwa pamoja ili kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite.
Katibu
Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Omar Chambo (wa pili kulia)
akitembelea baadhi ya vitalu vya uchimbaji madini ya Tanzanite katika
eneo la Mirelani mkoani Manyara mara baada ya kumaliza kikao kikao chake
na Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na
Manyara ambazo zimeamua kufanya kazi kwa pamoja ili kudhibiti utoroshaji
wa madini ya Tanzanite.Kulia kwake ni Afisa Madini Mkazi katika Ofisi
ya Madini Mirelani, Mhandisi Henry Mditi.
Makamishna
Wasaidizi wa Madini,Wizara ya Nishati na Madini, kutoka kulia ni Julius
Sarota (Wachimbaji Wadogo), Latifa Mtoro (Uthaminishaji madini), Salim
Salim (Uchumi na Biashara) pamoja na Mkurugenzi wa Sheria, Justus
Mulokozi (wa kwanza kushoto) wakiwa katika kikao kilichojumuisha Kamati
za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara (hawapo
pichani) ambazo zimeamua kufanya kazi kwa pamoja ili kudhibiti
utoroshaji wa madini ya Tanzanite nje ya nchi.
Mwenyekiti
wa Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na
Manyara na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makalla (aliyesimama)
akizungumza na wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya
Arusha, Kilimanjaro na Manyara (hawapo pichani) ambazo zimeamua kufanya
kazi kwa pamoja ili kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite nje ya
nchi. Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini,
Mhandisi Omar Chambo, wa kwanza kulia ni Katibu Tawala mkoa wa Manyara,
Eliakim Maswi na wa pili kutoka kulia ni Mkuu wa mkoa wa Arusha, Daud
Ntibenda.
Katibu
Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Omar Chambo (wa kwanza kulia)
akizungumza na baadhi ya wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama za
mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara ambazo zimeamua kufanya kazi kwa
pamoja ili kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite nje ya nchi.
Afisa
Madini Mkazi katika Ofisi ya Madini Mirelani, Mhandisi Henry Mditi
akitoa taarifa ya kazi zinazofanywa na Ofisi hiyo iliyopo katika wilaya
ya Simanjiro mkoani Manyara.Wanaosikiliza ni Katibu Mkuu Wizara ya
Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo (wa pili kushoto), Wa kwanza
kushoto ni Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje. Wengine
katika picha ni Kamishna Msaidizi wa Madini sehemu ya Uthaminishaji
Madini, Latifa Mtoro (wa kwanza kulia) na wa pili kulia ni Mkurugenzi wa
Taasisi ya Uunganishaji na Ushirikishi Wadau katika Tasnia ya Uziduaji
(EISF), Catherine Lyombe.
Na Teresia Mhagama na Asteria Muhozya
Katibu
Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo ameeleza kuwa
madini aina ya Tanzanite yaliyokamatwa yakitoroshwa nje ya nchi bila
kuwa na vibali tarehe 15 Desemba, 2015 kupitia uwanja wa ndege wa
Kilimanjaro (KIA) yamefikia thamani ya Dola za Marekani milioni
1,207,990.
Katibu
Mkuu alisema hayo jijini Arusha wakati wa kikao chake na Kamati za
Ulinzi na Usalama za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara ambazo
zimeamua kufanya kazi kwa pamoja ili kudhibiti utoroshaji wa madini ya
Tanzanite na kufuatilia kwa karibu shughuli za uchimbaji na biashara ya
madini hayo ili yanufaishe taifa.
Katibu
Mkuu alisema kuwa Tanzanite hiyo ghafi yenye uzito wa gramu 2,015.59
ilikuwa ikitoroshwa na raia wa India, Jain Anurag aliyekuwa akitaka
kuelekea mji wa Jaipur kwa kutumia shirika la ndege la Qatar.
“Nataka
niwaeleze watanzania wanaoshirikiana na raia wa kigeni kutorosha
Tanzanite kuwa wajiepushe na biashara hii haramu kwani hatua kali
zitaendelea kuchukuliwa dhidi yao na hatuna mzaha katika hili,” alisema
Mhandisi Chambo.
Alieleza
kuwa madini hayo yaliyokamatwa yameshataifishwa kama ambavyo sheria
na kanuni za madini zinavyoelekeza na kwamba zoezi hilo la ukamataji
watorosha madini hufanywa na Wizara ya Nishati na Madini kupitia Wakala
wake wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) kwa kushirikina na Taasisi nyingine
kama Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa
Taifa, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Idara ya Uhamiaji.
Aidha
alieleza kuwa serikali itafuta leseni za wafanyabiashara wa madini
watakaobainika kutorosha rasilimali hiyo nje ya nchi ikiwemo kuwakamata
wachimbaji na wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi stahiki kwa
serikali.
“Ili
kudhibiti utoroshaji madini unaofanywa na wafanyabiashara wenye leseni
na wasio na leseni, wazawa na wasio wazawa, tumeshajipanga kwa
kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa mitatu ya Manyara,
Kilimanjaro na Arusha ili kudhibiti hali hii na Tanzania ibaki kama
kinara katika uzalishaji na uuzaji wa madini haya na sio nchi nyingine,”
alisema Mhandisi Chambo.
Kuhusu
wachimbaji wadogo nchini, alisema kuwa serikali itaendelea kugawa
maeneo ya uchimbaji madini kwa wachimbaji hao ikiwa ni pamoja na utoaji
ruzuku, uagizaji wa zana kama baruti na utoaji wa mafunzo huku akitoa
angalizo kuwa wachimbaji hao wanapaswa kuwa waaminifu na kuhakikisha
kuwa wanalipa kodi stahiki serikalini badala ya kusubiri kuchukuliwa
hatua za kisheria.
Wakati
huohuo Mwenyekiti wa Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Arusha,
Kilimanjaro na Manyara na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makalla
ametoa masaa 24 kwa raia wa kigeni wote wanaojihusisha na biashara ya
madini ya Tanzanite na madini mengine kinyume cha sheria kuondoka nchini
mara moja na watakaokaidi agizo hilo watachukuliwa hatua kali za
kisheria.
Agizo
hilo alilitoa baada ya Kamati hiyo kubaini kwamba uwepo wa wageni
mbalimbali kutoka nje ya nchi hususani Kenya, Sri Lanka, Nepal na India
ambao hujihusisha na biashara ya Tanzanite bila kuwa na leseni
zinazowaruhusu kufanya hivyo na hatimaye hutorosha madini hayo kwenda
nje ya nchi.
“Madini
haya yanauzwa kama njugu hivyo tumeona kwamba sisi Kamati za Ulinzi na
Usalama za mikoa hii mitatu tukishirikiana kuimarisha ulinzi tutakomesha
suala hili, tunataka kuona watu watu wanaouza madini ni wale wenye
leseni tu, na wachimbaji na wafanyabiashara wahakikishe wanalipa kodi
stahiki kwani kuanzia tarehe Tano Januari operesheni ya kuwakamata
itaanza,” alisema Makalla.
Vilevile
alieleza kuwa wafanyakazi wa kigeni waliopo katika mgodi wa Tanzanite
One unaomilikuwa na kampuni ya Sky Associates kwa kushirikiana na
serikali ambao hawana vibali vya kufanya kazi na wale wenye vibali vya
kufanya kazi ambazo zingeweza kufanywa na watanzania waondoke mgodini
hapo.
“Mchango
wa madini katika Pato la Taifa bado hauridhishi na sisi tunafanya kila
jitihada ili Tanzanite hii ambayo inachimbwa Tanzania peke yake
ifaidishe nchi, kila mwananchi anao wajibu wa kuhakikisha hili
linafanikiwa, wadau wa madini wana wajibu wa kuhakikisha kwamba wanalipa
kodi stahiki na kutoa taarifa za hujuma zozote zinazofanyika ambazo
baadhi ya wazawa wanashirikiana na wageni kuiibia nchi rasilimali hii
muhimu,” alisema Makalla.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni