Mkuu wa Operesheni wa Jeshi la Polisi Mkoani Arusha (ACP) Edward Balele akifungua kikao kati ya Jeshi hilo na Taasisi za ulinzi kujadili mustakabali wa usalama ndani ya mkoa huu. Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa Bwalo la Polisi Jijini hapa (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ulinzi ya KK kanda ya Kaskazini Claude Herssens akichangia mada katika kikao kilichoandaliwa na Jeshi la Polisi Mkoani hapa na kuziusisha taasisi mbalimbali za ulinzi (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Baadhi ya washiriki wa Taasisi za Ulinzi wakiwa wanasikiliza moja ya mada kwa umakini ili baadae waweze kutekeleza kwa vitendo. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Na Mahmoud Ahmad Arusha
Jeshi la Polisi mkoani hapa limeazimia kushirikiana na Makapuni binafsi ya Ulinzi na taasisi za Ulinzi kutoka UN-ICTR, UNMICT, kitengo cha Ulinzi cha B.O.T pamoja na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu katika kupeana baadhi ya taarifa za uhalifu na wahalifu mara kwa mara kwa njia mtandao wa kijamii wa “whatsApp”.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Operesheni wa Jeshi hilo mkoani
hapa (ACP) Edward Balele wakati akifungua kikao kilichofanyika katika Bwalo la
Polisi mjini hapa alipokuwa anazungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoani
hapa mwishoni mwa wiki kati ya Jeshi hilo na wawakilishi wa Makampuni 31 ya
Ulinzi, Benki Kuu Kanda ya Kaskazini, Mahakama ya Afrika ya Haki za Kibinadamu,UN-ICTR
na UNMICT.
Mkuu huyo wa Operesheni alisema kwamba imefika wakati sasa
kwa taasisi hizo kuzidi kuimarisha mahusiano kwa ukaribu huku njia za kisasa za
mawasiliano zikitumika katika kupeana taarifa za uhalifu na pia kubadililishana
uzoefu katika masuala ya ulinzi na usalama.
Alisema awali taarifa juu ya matukio mbalimbali sio kwamba
zilikuwa hazipatikani bali zilikuwa zinawafikia walengwa kwa mtindo wa ujumbe
mfupi yaani SMS lakini kwa kutumia mfumo wa kikundi cha “WhatsApp” ambacho
kitapewa jina maalum, taasisi hizo zitakuwa zinapata na kutoa taarifa kwa
pamoja na kila mhusika atakuwa anachangia mawazo yake huku wanachama wengine wa
kikundi hicho wakiwa wanaona ushauri wa kila mchangiaji.
Aidha mbali na uundaji wa kundi hilo litakalotumia mtandao
huo wa kijamii mbao umeshika kasi katika mawasiliano pia aliyaomba Makampuni
hayo kutoa ushirikiano zaidi hasa kwa kutoa rasilimali vifaa pamoja na askari
katika kuelekea mwisho wa mwaka kwa nia ya kufanya doria ya pamoja hivyo
kudhibiti vitendo vya uhalifu ndani ya Mkoa wa Arusha.
Kwa upande wake Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa
Arusha (SSP) Muliro Jumanne Muliro alisema kwamba Jeshi la Polisi na Makampuni
hayo kila chombo kikiwa kinawajibika ipasavyo katika nafasi yake mafanikio ya
kudhibiti vitendo vya uhalifu yatakuwa makubwa.
Alisema anathamini mchango mkubwa unaotolewa na Makapuni hayo
ya Ulinzi kwani matukio mengi ya uvunjaji wa Maghala ya viwanda, Ofisi
mbalimbali na Makampuni yamepungua ukilinganisha na miaka ya nyuma kabla
Makapuni hayo ya Ulinzi kukubaliwa kisheria.
Mkuu huyo wa Upelelezi alisema kwamba wakati wa uajiri wa
askari hao wanatakiwa waangalie mambo mablimbali ikiwemo akili ya kuweza kugundua
kitu kinachoashiria uhalifu, kuwa mwaminifu, kuwa mtulivu na kuwa mvumilivu na
kusema kwamba huwa anafadhaishwa sana pale anapopata shauri linalomhusisha
askari yoyote katika uhalifu hali ambayo inatia doa na aibu kwa taasisi zote za
Ulinzi.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha Mrakibu
Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SSP) Mary Lugola ambaye alizungumzia juu ya
huduma bora kwa Mteja ambapo aliwataka Wawakilishi wa Makampuni hayo
kuwaelekeza askari wao kuwa, wawe na lugha nzuri kwa wateja wao jambo ambalo
pengine litakuwa linazidi kuwavutia wengine na hatimaye kupata malindo mengi
ambayo yatawaongezea kipato, mbali na hilo pia aliwataka kutotumia nguvu kupita
kiasi katika ukamataji ili kupunguza madhara makubwa yanayoweza kutokea.
Kwa upande wake Mkuu
wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) Mkoa wa Arusha (SSP) Ramadhani Giro yeye
aliyataka makampuni hayo kufanya mazoezi ya mara kwa mara na alisema baadhi ya
Makampuni ya Ulinzi huwa yanapata
mafunzo mbalimbali kama vile matumizi sahihi ya silaha, ukakamavu na mbinu
mbalimbali za kuweza kubaini uhalifu na wahalifu toka kwa askari waliopo katika
kikosi hicho na kutoa wito kwa askari wa makapuni mengine kujitokeza ili waweze
kupata mafunzo hayo na kupunguza madhara yanayoweza kutokea huko mbeleni.
Wakichangia katika kikao hicho baadhi ya wawakilishi wa
Makampuni ya Ulinzi, Mwakilishi toka Kampuni ya KK Security ambaye pia ni
Meneja Mkuu wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini Bw. Claude Herssens alilisifu Jeshi
la Polisi mkoani hapa kwa kuitikia wito kwa haraka pindi wanapoomba msaada na
kuongeza kwamba mtandao huo utawasaidia sana na hivyo kuwafanya wajue tukio
ambalo wanatakiwa kwenda kutoa msaada nje ya mipaka yao ya kazi na tukio ambalo
litakuwa linawahusu Polisi pekee.
Naye Katibu wa Chama Cha waajiriwa wa Makampuni Binafsi Kanda
ya Kaskazini (TUPSE) Aisha Masoud alizidi kusisitiza kwamba bado baadhi ya
Kampuni hizo zinachangamoto hasa katika suala zima la mishahara ya wafanyakazi
wao japokuwa serikali toka mwaka 2013
mwezi Agosti ilishatangaza mishahara mipya lakini baadhi yao hawajatekeleza
hilo na kuwataka wafanye hivyo pamoja na kuwaingiza katika mifuko ya Jamii.
Mara kwa mara Jeshi la Polisi Mkoani hapa limekuwa likifanya
vikao na Makapuni ya Ulinzi lengo likiwa ni kukumbushana majukumu ya utendaji
wa kazi za kila siku hali ambayo inasababisha kuimarika kwa hali ya usalama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni