Mdau Krantz
Mwantepele akizungumza na Raia waamilifu kutoka kijiji cha Kilago
wilayani Kahama ambapo nilipata nafasi ya kujua mambo mbalimbali ikwemo
mchango wa uraghabishi katika kijiji hicho katika sekta ya elimu
Na Krantz Mwantepele , Kahama
Utoro
ni tabia ya kuondoka au kutokufika mahali mara kwa mara bila ya kutoa
taarifa. Tabia hii ipo kwenye maeneo ya makazini pamoja na shuleni.
Katika baadhi ya kata za wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.
Tabia
hii imekuwa kero kwa wanajamii wa kata za Nyandekwa na Kilago kwa kuwa
inawarudisha nyuma kimaendeleo. Wakiwa kama sehemu ya wananchi wa kata
hizo, waraghbishi wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha watoto watoro
wanahudhuria shuleni.
Ikiwa
kama sehemu ya uraghbishi, kutambua changamoto zinazokabili jamii
wanayoishi, waraghbishi walitambua kwamba hili ni tatizo na hivyo kuamua
kulishughulikia.
“Nikiwa
njiani kuelekea kwenye shughuli zangu, nikakuta watoto wamejibanza
kwenye kichaka, na wengine walikuwa wakicheza mpira. Nikataka kujua
kulikoni mbona hawapo shuleni, wakati ni muda wa masomo?”
Hili
ni swali ambalo raia mwamilifu na mraghbishi Paul Izengo toka katika
kijiji cha Nyandekwa kilichopo wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga,
alitaka kulipatia majibu yake. Udadisi huu ndio uliopelekea kwa yeye
kuwasogelea watoto ambao kimsingi walitakiwa kuwa shuleni mda huo na
kutaka kujua kulikoni.
Raia
Waamilifu, Mathew Charles (kushoto) wa kijiji cha Kilago na Alphonce
Peter toka kijiji cha Ufala wilayani Kahama wakifurahia jambo walipkuwa
wakijadili tatizo la utoro mashuleni
Na
jibu lilikuwa ni moja tu kwamba wametoroka shule na kwanini watoroke.
Paul hakuishia tu kujiuliza maswali, alikwenda hatua moja mbele kwa
kuwafuata watoto wale na kuwauliza,
“Nyinyi mnafanya nini hapa? Wakati huu ni muda wa kuwa darasani. Haya shuleni haraka, niliwakaripia, hao wakakimbia.”
Kukimbia
wakati umeulizwa ni dalili ya kuogopa kutokana na kosa unalojua
umefanya. Watoto wale walijua kwamba wamekosa, na kosa lilikuwa ni utoro
shuleni. Hili si tatizo tu la kijiji cha Nyandekwa, hata Kilago pia
ambapo baadhi ya wazazi wanatajwa kuwa chanzo cha tatizo hilo la utoro.
Akiwa kama raia mwamilifu na mraghbishi toka katika kijiji cha Kilago, wilayani Kahama Mathew Charles anasema:
“Wazazi
ndio sababu ya utoro huu mashuleni, wanawapa watoto wao kazi muda ambao
ni wa kwenda shule. HIvyo unapomwambia ukweli anachukia anaona kama
vile unamwingilia maisha yake,”
Tabia
hiyo ya baadhi wa wazazi kuunga mkono utoro wa watoto wao kwa visingizio
vya kutaka kuwa huru na maisha, haviwatakatishi tamaa waraghbishi hao.
Kwani hili ni jukumu lao katika kuhakikisha watoto wanapata haki zao.
Katika
kusadia watoto hao wanarudi shuleni, waraghbishi kupitia mtandao wao wa
wilaya ya Kahama, wamekuwa wakitoa elimu na kuwakishirikisha baadhi ya
wazazi wa watoto hao kutambua umuhimu wa elimu na inapobidi kukamata
watoto watoro na kuwapelekashule.
Na
baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwafuata na kuomba ushauri wanapoona mtoto
ameanza kuwa na tabia ya utoro. Na mara nyingi wamekuwa wakiwashauri
wazazi hawa kushirikiana na walimu ili kuweza kufuatilia maendeleo ya
watoto wao. Akifafanua hilo Michael Mathew anasema:
“Kwa
mfano katika kipindi cha mwezi wa 10 wazazi wawili wamekuja kuniomba
niongee na watoto wao umuhimu wa kwenda shule. Na nafarijika kuona
harakati zangu za uraghbishi zinatambuliwa kwenye kijiji change.
Tukiacha
hili za wazazi kutowapeleka watoto wao shule kwa sababu mbalimbali,
ambapo serikali imekuwa ikiwachulia hatua kali za kisheria wazazi hao,
watoto wenyewe nao ni chanzo cha kingine cha utoro mashuleni. Wengine
wanaaga wamekwenda shule lakini ukweli ni kwamba hawafiki shule na
badala yake wanajificha wanapokujua hadi muda wa kurudi unapofika nao
hurejea majumbani kana kwamba wanatoka shule.
Hivyo
ni wajibu wa raia mwamilifu na aliye mraghbishi anapaswa kuhakikisha
watoto wanapata haki yao hii ya msingi ya elimu. Na hivyo ikibidi hata
kutumia nguvu, kama anavyosimulia Mathew Charles:
“Muda
mwingine nawabeba kwa nguvu watoto hadi shuleni na kuwakabidhi kwa
mwalimu. Nimeshafanya hivyo kwa watoto watano sasa. Tunajua kwamba
wasiposoma sasa watakuwa mizigo kwenye jamii. Kuna siku watatukumbuka
kwamba tulikuwa tunawasaidia,”
Ni dhahiri kwamba tatizo hili ni kubwa na si jukumu la walimu peke yao?
Krantz
Mwantepele akiwa katika picha ya pamoja na waragahbishi na raia
waamilifu wa kijiji cha Kilago wilayani Kahama siku za hivi karibuni
Kila
mwananchi pale alipo ana jukumu la kuhahakisha huduma bora za jamii
zinapatikana kwa mustakabali wa maendeleo yao. Katika kufanikisha hili
raia waamirifu ama waraghbishi toka katika vijiji vya kata ya Nyandekwa
na Kilago wameonesha njia katika kuhakikisha wanafunzi watoro
wanahudhuria shuleni.
Waraghbishi na Raia Waamilifu toka katika kijiji cha Nyandekwa wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mkutano wao hapo kijijini
Akielezea
jinsi alivyoamua kushughulikia tatizo hilo kijijini pao, Paul ambaye
pia ni kiongozi wa waraghbishi wapya kutoka kijiji cha Nyandekwa
anasema:
“Nililazimika
kumpigia simu mwalimu mkuu na kuomba kuonana naye kwa lengo la
kujadiliana naye kuhusu hili tatizo. Na pale ndipo nilipoweza kuelewa
ukubwa wa tatizo la utoro. Hivyo nikakubaliana na mwalimu kuwa
tutasaidiana katika kuhakikisha kwamba watoto watoro wanahudhuria
shuleni.”
Kwa
mujibu wa orodha aliyokabidhiwa mraghbishi Paul Izengo na mwalimu mkuu
wa shule ya msingi Nyandekwa, kuna wanafunzi 21 ambao wameripotiwa utoro
kati ya 449 wa shule hiyo.
Kitendo
hiki cha mraghbishi kuamua pasipo kulazimishwa na mtu kufuatilia suala
la utoro wa wanafunzi katika shule yao ya msingi pale kijijini, ndicho
ambacho raia mwamilifu anatakiwa kukifanya.
Raia
mwamilifu ni yule ambaye anachukua hatua kwa kushirikiana na wanajamii
wengine wa maeneo yake. Huyu ni yule anayetambua majukumu na haki zake
kwa mujibu wa ibara ya 12 hadi 24 ya Katiba ya Muungano wa Tanzania.
Huyu ni raia anayependa kuona mabadiliko chanya kwenye jamii yake. Huyu
ni yule anayetenda pasipo kulazimishwa, bali kwa utashi na uelewa wake
kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.
Katika
kuhakikisha anaelewa vizuri chanzo cha tatizo hilo, ilimlazimu Paul
kwenda kumtembelea mzazi ambaye mtoto wake yumo kwenye orodha wa watoro.
Na huko alitaka kujua, nini hasa kinachosababisha tatizo hilo.
“Nilikwenda
kwa mama mzazi wa mmoja wa wale watoto walioripotiwa kuwa watoro. Lengo
langu nilitaka kujua nini hasa tatizo mpaka mtoto haendi shuleni. Ndipo
nilipogundua kuna changamoto kubwa zaidi. Inahitajika elimu ya ziada
kutolewa,”
Mama
mzazi huyo, alimweleza mraghbishi huyo kwamba michango kwa ajili ya
kulipia mitihani ya watoto wake waliopo darasa la 4 na la 6 ni
changamoto kubwa inayomkabili. Kushindwa huko kuwalipia watoto wake
gharama hizo kumepelekea kwa watoto hao kurudihswa nyumbani.
Sababu
nyingine anayoitaja mama huyo ni upungufu wa chakula hasa watoto
wanapokwenda asubuhi na kurudi shule mchana. Hali hii inasababisha
watoto wasiende shule na kujikita katika shughuli za kuzalisha kwa ajili
ya familia.
Pamoja
na changamoto hizo, bado raia huyu mwamilifu alimshauri mama huyo
kwenda kuonana na mwalimu mkuu ili aangalie ni kwa jinsi gani anaweza
kusaidiwa ili watoto wake wahudhurie shuleni.
Ushauri
huu unatokana na ukweli kwamba mwalimu mkuu wa shule hiyo Ramadhani
Masatu naye pia ni raia mwamilifu kwa nafasi yake. Uwamilifu huo
unaelezewa na mraghbishi Elizabeth Ngayalina, toka kijiji cha Nyandekwa:
“Mwalimu
mkuu ni muelewa na ndio maana amekubali kushirikiana nasi. Ametupatia
kwanza idadi ya wanafunzi ambao ni watoro kwa kuwa anajua ni jukumu letu
sote si la kwake na walimu wenzake”.
Nikiwa
katika picha ya pamoja na Waraghbishi na Raia Waamilifu toka katika
kijiji cha Nyandekwa wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mkutano wao
hapo kijijini
Kwa
hakika raia hawa waamilifu toka katika vijiji vya Nyandekwa na Kilago
wanahitaji kuungwa mkono na wadau wote wa maendeleo. Elimu ni haki ya
msingi ya kila mtoto na ndio maana sera ya serikali ni kutoa bure elimu
ya msingi na ile ya sekondari. Njia pekee ya kumkomboa mtoto ni kumpatia
elimu ambayo ndio dira ya maendeleo ya kila nchi, kuwa na wasomi wengi
kadri iwezekanavyo.
CHANZO; MWANAHARAKATI MZALENDO
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni