MASHINE ZA MRI, CT-SCAN HAZITAKWAMA TENA

muh1 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Donan Mmbando (wa pili kutoka kushoto) akikata utepe kuashiria kufungualiwa kwa duka la dawa leo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambalo linalomilikiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD). Kutoka kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa MNH, Profesa Lawrence Mseru. Picha zote kwa hisani ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
muh2 
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Donan Mmbando akipewa taarifa ya utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli kuhusu kufungua duka la dawa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam.
muh3 muh4
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Donan Mmbando akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua duka la dawa linalomilikiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD). Duka hilo limefunguliwa leo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
muh5
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Lawrence Mseru akizungumza na waandishi wa habari baada ya uzinduzi wa duka la dawa la MSD.
muh6
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Donan Mmbando (wa pili kulia), Mkurugenzi Mkuu wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Laurean Rugambwa (kulia) na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Mseru (wa tatu kutoka kulia) wakiwa katika picha ya pamoja leo katika hospitali hiyo baada ya kufunguliwa kwa duka la dawa la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) leo jijini Dar es Salaam.

Serikali imewahakikishia Watanzania kwamba mashine ya Magnetic Resonance Imaging (MRI) pamoja na Computerized Tomography Scan (CT-SCAN) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) hazitakwama kufanya kazi kwa kuwa imeweka utaratibu mzuri wa kuzitengeneza.
 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Donan Mmbando amesema serikali imezungumza na Philips na wamekubaliana kwamba mashine hizo hazitakwama na endapo litatokea tatizo la kiufundi watashughulikia mara moja.
 

“Mwaka ujao ni mwaka wa bajeti serikali itatenga fedha kwa ajili ya kutengeneza mashine za CT-SCAN na MRI, lakini mtambue kwamba si tu mashine hizo zinapaswa kutengenezwa bali na mashine nyingine.”amesema Dk Mmbando.
 

Pia, Dk Mmbando amefungua duka la dawa la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ndani ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kueleza kwamba kufunguliwa kwa duka hilo kutasaidia wananchi kupata huduma haraka na kununua dawa kwa gharama nafuu na huduma hiyo itatolewa kwa saa 24.
 

Akifafanua kuhusu mashine za MRI na CT-Scan, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Profesa Lawrence Mseru amesema Novemba 25, 2015 alifika fundi kutoka Afrika Kusini ambaye pia ni fundi wa MRI na kuitengeneza na kuanza kufanya kazi tangu Novemba 26 mpaka Disemba 2, mwaka huu. Wagonjwa 152 wamepimwa na kwamba wengi wagonjwa wa dharura.
 

Amesema hivi sasa mafundi wanafunga mashine ya Digital X-Ray iliyotolewa na serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambapo usimikaji unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa juma hili.
Akielezea utekelezaji wa agizo la wagonjwa wanaolala chini kupatiwa vitanda, Profesa Mseru amesema ili kuondoa wagonjwa wote waliolala chini, serikali kupitia MSD ilileta vitanda 300 pamoja na magodoro yake, vitanda hivyo vyote vilipelekwa kwenye Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) na tayari MOI imeanza kuhamisha wagonjwa waliokuwa wamelala chini kutoka wodi za MNH walizokuwa wanazitumia, mpaka sasa wagonjwa 120 wamehamishwa.
Novemba 9, mwaka huu Rais John Magufuli alifanya ziara MNH na kutoa maagizo kwamba ndani ya wiki mbili mashine ya MRI na CT-SCAN ambazo zilikuwa zimeharibika ziwe zinafanya kazi, wagonjwa waliolala chini wawe wamepata vitanda na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ifungue duka la dawa ndani ya hospitali ili kuondoa ukosekanaji wa dawa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni