Na Pili Khatib na Zuhura Omar, MUM
Mkurugenzi
Mwendeshaji wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar ZSTC Mwanahija
Almas Ali amesema Maendeleo ya Sekta ya Zao la Karafuu inaendelea
kuimarika zaidi Zanzibar hasa baada ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo
ya Karafuu.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari Makao Makuu ya ZSTC Maisara Bi. Mwanahija
alisema Mfuko huo ulianzishwa kuongeza nguvu jitihada za Serikali za
kuimarisha zao hilo la uchumi wa Taifa.
Alisema
utafiti ulifanyika juu ya namna ya kufanya mageuzi yenye tija katika
Sekta ya Karafuu ndipo ikaoneka umuhimu wa kuanzisha Mfuko huo ambapo
muda mfupi baada ya kuanzishwa unaonekana kuleta faida katika
uimarishaji wa zao hilo.
“Madhumuni
ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu ni kuhakikisha Sekta ya
Karafuu inakua na kuimarika zaidi. Kuongeza idadi ya mikarafuu na
uzalishaji ambapo hivi sasa Wananchi wamehamasika zaidi katika upandaji
mikarafuu kwa wingi”.
Alifahamisha
Bi. Mwanahija. Alisema Mfuko huo ambao upo chini ya Mkurugenzi
Mwendeshaji wa Shirika la ZSTC umejipanga kufanya sensa ya mikarafuu
sambamba na kuwasajili Wakulima na Wafanyabiashara wa zao hilo ili
kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Aidha alifahamisha kuwa
kupitia Mfuko huo na kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Maliasili
kutafanyika tafiti kwenye kila eneo linayohusu zao la karafuu kwa lengo
la kugundua changamoto na kuzifanyia kazi.
Alisema Shirika la
ZSTC kwa kushirikiana na Wadau wengine inakamilisha mpango maalumu wa
kuziongezea hadhi na thamani karafuu za Zanzibar kupitia mradi wa
‘Branding’ ili kuongezeka kwa uzalishaji kwenda sambamba na kuongezeka
kwa tija kwa Wakulima na Taifa.
Alisema hivi sasa mpango huo upo
katika kutafuta vinasaba vinavyoonyesha ubora wa karafuu za Zanzibar
kupitia Mkemia Mkuu wa Serikali Zanzibar.
Alisema kupitia Mfuko
huo Shirika limeongeza jitihada za kutoa elimu kwa Wakulima juu ya
uchumaji na uanikaji unaotakiwa ili kulinda ubora wa zao hilo katika
soko la nje.
Alisema Mfuko huo umekuwa ni msaada mkubwa katika
uimarishaji wa zao la karafuu hasa kwa Wakulima ambapo unatoa fidia kwa
Wakulima wanaopata ajali wakati wa uchumaji kupitia Shirika la Bima
Zanzibar.
Alifahamisha kuwa Mfuko huo umelipa bima
ya milioni 60 kwa Shirika la Bima ili kuwafidia Wakulima 100 wanaokisiwa
kupata ajali katika zoezi la uchumaji wa karafuu mwaka 2015/2016 ambapo
hadi sasa tayari watu tisa wameripotiwa kupata ajali wote kutoka Pemba.
Alisema Wakulima wanaendelea kupata mikopo ya uchumaji kupitia
Mfuko huo na alifahamisha kuwa katika bajeti ya 2015/2016 Mfuko umepanga
kutumia milio 140 kwa ujenzi wa barabara ya Ng’omeni ikiwa ni msaada wa
kusadia miundombinu ya sehemu za uzalishaji wa karafuu.
Akizungumzia
makadirio ya mavuno ya karafuu ya mwaka 2015/2016 Mkurugenzi huyo
alisema Shirika limekadiria kununua tani 2800 mpaka 3200 katika mwaka
huo.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni