Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango akitoa hotuba katika
mkutano wa uzinduzi wa kitabu cha Mwongozo wa Usimamizi na Utayarishaji
wa Miradi ya Uwekezaji katika sekta ya Umma kilichofanyika mjini Dodoma.
Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango akikata utepe kuashiria
uzinduzi wa kitabu cha Mwongozo wa Usimamizi na Utayarishaji wa Miradi
ya Uwekezaji katika sekta ya Umma, kushoto ni Katibu tawala wa mkoa wa
Dodoma bibi. Rehema Madenge na kulia ni bi Anna Kimwela kutoka Tume ya
Mipango.
Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango akionesha kitabu cha
Mwongozo wa Usimamizi na Utayarishaji wa Miradi ya Uwekezaji katika
sekta ya Umma (Public Investment Management Operational Manual), kulia
ni Kaimu katibu mtendaji wa Tume ya Mipango Bibi Florence Mwanri na
kushoto ni katibu tawala wa Mkoa wa Dodoma Bibi Rehema Madenge.
Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (wa tano kutoka kushoto kwa
waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa mkutano mara baada
ya uzinduzi wa kitabu cha Mwongozo wa Usimamizi na Utayarishaji wa
Miradi ya Uwekezaji katika sekta ya Umma.
Na Adili Mhina, Dodoma
Tume
ya mipango imezindua kitabu cha Mwongozo wa Usimamizi na Utayarishaji
wa Miradi ya Uwekezaji katika sekta ya Umma (Public Investment
Management Operational Manual) kwa lengo la kuimarisha utendaji,
uwajibikaji na kuleta ufanisi katika matumizi ya rasilimali za umma
zinazoelekezwa katika miradi ya maendeleo.
Akizindua mwongozo
huo katika mkutano uliofanyika mwishoni mwa juma mjini Dodoma na
kuhudhuriwa na wataalamu wa uchumi, sera na mipango kutoka wizara,
halmashauri na taasisi mbalimbali za serikali, Waziri wa fedha na
mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango alieleza kuwa shabaha ya mwongozo huo ni
kutoa maelekezo ya mchakato na hatua zinazohitajika kufuatwa katika
kutayarisha na kutekeleza miradi yote inayotumia fedha za umma au kwa
kushirikiana na sekta binafsi.
Waziri mpango aliwataka viongozi
wote wenye dhamana ya kusimamia miradi kusoma mwongozo huo na kuuelewa
ili kuepuka makosa yaliyokuwa yakijitokeza huko nyuma huku akisisitiza
kuwa serikali ya awamu ya tano haitamvumilia wala kumonea huruma
mtendaji yeyote atakayeshindwa kuwajibika ipasavyo.
“Kuanzia
sasa watu ambao wamepewa dhamana ya kusimamia miradi ya maendeleo,
miradi itakaposhindwa kuna mambo mawili tu yakufanya; ama waachie ngazi
mapema wao wenyewe au basi wasubiri tuwatumbue. Kwahiyo nawaombeni sana
hiki kitabu ambacho kimeandaliwa kuanzia leo kila mmoja akisome vizuri
ili kusiwe na miradi tena ambayo ni ya ovyo ovyo,” alisisitiza waziri
mpango.
Mwongozo huo unazielekeza Wizara, Idarana
Wakala wa Serikali,Sekretarieti za Mikoa na Serikali za Mitaa jinsi ya
kufanya uchambuzi unaozingatia vigezo vya kiuchumi na kifedha na
kufafanua mbinu, hatua, taratibu, na kuweka viwango vinavyohitajika
katika kuandaa na kuwekeza miradi.
Waziri Mpango alieleza kuwa
maelekezo ya mwongozo huo yanafafanua vigezo muhimu vya uchambuzi wa
kiuchumi na kifedha ili kufikia uamuzi wa miradi ipi ina manufaa na
inaweza kupata mikopo katika soko la mitaji la ndani au la kimataifa.
“Mwongozo
huu umeanisha vigezo kama mzunguko wa mradi (project cycle) ikiwa ni
pamoja na andiko la awali (concept note), mchanganuo wa faida na hasara
(cost-benefit analysis) vigezo vya kuchanganua mradi kama vile uwezo wa
uzalishaji (internal rate of return) na thamani halisi ya uwekezaji
(Net Present Value), na vinginevyo”Alieleza Dr. Mpango.
Kuzinduliwa
kwa mwongozo huo kunatoa tafsiri kuwa miradi yote itakayohitaji fedha
za Serikali katika Bajeti italazimu kufuata utaratibu uliobainishwa
katika kitabu hicho ili kuweza kuimarisha ufanisi na kupata thamani ya
fedha. Hivyo, Mwongozo ni chombo muhimu katika michakato mbalimbali ya
kupanga bajeti kama vile Mwongozo wa Mpango na Bajeti, Mpango wa
Maendeleo wa Taifa wa Mwaka Mmoja na kadhalika.
Kwa
upande wake Kaimu katibu mtendaji wa Tume ya Mipango Bibi Florence
Mwandri alieleza kuwa mwongozo huo unategemewa kuwa mwanzo wa kujenga
uwezo katika usimamizi wa uwekezaji wa umma na utakuwa ni msingi wa
kuwaimarisha maafisa wa serikali kinyenzo katika kuchambua, kuchagua,
kuwasilisha miradi ya uwekezaji kiuchumi na kifedha, pia kijamii kwa
kukidhi taratibu na sheria zinazoendesha uwekezaji katika sekta ya umma.
“Katika kufanikisha utekelezaji wa Mwongozo huu na kujenga
uwezo wa kutosha, Serikali imedhamiria kuweka utaratibu wa kutoa mafunzo
kwa walengwa wakuu katika ngazi za mafunzo ya muda mfupi, muda wa kati
na mrefu ili kuongeza utaalam na kuwekeza miradi michache kwa mwaka wa
bajeti lakini kwa ufanisi zaidi”, alisema bibi Mwanri.
Mwongozo
huo pia unatoa taratibu kwa miradi ambayo haitapata fedha kwa mwaka
husika itawekwa katika kanzi-data (Database) ambayo itaanzishwa chini ya
Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango kwa ajili ya kufikia malengo ya
utekelezaji wa usimamizi wa uwekezaji katika sekta ya umma.
Kukamilika
kwa kanzi-data kutasaidia wadau mbalimbali wanaohusika na maamuzi ya
uwekezaji katika sekta ya umma kuwa na uelewa mmoja kuhusu miradi yenye
kipaumbele. Kanzi-data itaonesha miradi gani ya umma, inategemewa
kutekelezwa, itaanza lini, na kumalizika lini na ina fedha kiasi gani.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni