WAZIRI MKUU MAJALIWA AMESEMA VIJIJI 42 RUANGWA KUPATIWA UMEME



WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa, Kassim Majaliwa amesema vijiji 42 vya wilaya ya Ruangwa vitaunganishiwa umeme katika Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) awamu ya tatu.

Amesema hadi sasa tayari vijiji 48 vya wilaya hiyo vimeunganishiwa umeme na kwamba lengo lake ni kuhakikisha vijiji vyote 90 vinapata huduma hiyo, hivyo amewaomba wananchi kuendelea kuwa na subira.

Waziri Mkuu, Majaliwa ameyasema hayo jana alipokuwa akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Michenga, Chinongwe, Makanjiro na Chinokole katika mikutano ya hadhara aliyoifanya wilayani Ruangwa.

“Niliwaahidi kuwatumikia, kuwahudumia na kuwasemea ndani na nje ya nchi, nawahakikishia kuwa sitowaangusha hivyo endeleeni kuwa na subira, nitafanya mambo mengi ya maendeleo kama isemavyo kauli mbiu yangu, Ruangwa kwa maendeleo inawezekana.” amesema.

Kwa upande wake Meneja wa TANESCO mkoa wa Lindi, Sotco Nombo amesema tarehe 15 mwezi huu wataanza kusambaza vifaa katika kijiji cha Chinongwe na kwamba hadi kufikia mwezi Mei mwaka huu umeme utakuwa umewaka katika kijiji hicho.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu, Majaliwa amewasisitiza wananchi kuanza kulima kwa wingi zao la muhogo kwa sababu kuna soko la uhahika la zao hilo baada ya kujitokeza kwa wafanyabiashara kutoka China na Marekani wanaotaka kununua zao mihogo nchini.

“Mnataka hela, mnataka hela? ila lazima mfanye kazi…mimi nimewatafutia hela nawaomba mlime mihogo kwa wingi maana kuna wafanyabiashara wanataka kununua mihogo, hela ndiyo hiyo ambayo ni soko la uhakika la mihogo. Nawasihi mchangamkie dili hili,” amesema.

Amesema wafanyabiashara hao wanataka kununua mihogo kutoka wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale kwa ajili ya kusaga unga na kutengeneza vyakula vingine vitokanavyo na zao hilo, hivyo amewaomba wananchi hao kuchangamkia fursa hiyo na kulima mashamba makubwa ya mihogo.
 

                                                                              Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni