WAZIRI MKUU MH. MAJALIWA AMUAGIZA MKUU WA MKOA LINDI KUFUATILIA MRADI WA UMWAGILIAJI WA NARUNYU


WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi kufuatilia maendeleo ya mradi wa umwagiliaji wa Narunyu katika kata ya Kiwalala wilayani Lindi.

Hatua hiyo imekuja baada ya wananchi wa kata hiyo kusimamisha msafara wa Waziri Mkuu, Majaliwa katika eneo la Kiwalala jana na kumuomba awasaidie kuhusu hatma ya mradi wao wa umwagiliaji ambao walitakiwa wakabidhiwe tangu mwaka 2014.

Awali muwakilishi wa wananchi hao, Mohammed Bakar alisema kuwa mradi huo uliogarimu shilingi milioni 600 ulitakiwa uwe tayari umekabidhiwa kwa wananchi, lakini hadi sasa bado na hata banio halijakamilika, hivyo wanashindwa kuendelea na kilimo katika eneo hilo.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu mradi huu bado haujaanza ila tulishangaa wakati wa mbio za mwenge mwaka 2014 ilisomwa taarifa kwamba wakazi wa Kiwalala wananufaika na mradi wa kilimo cha umwagiliaji wa Narunyu jambo ambalo si kweli kwani mradi huu haujawahi kufanya kazi na hata banio hakuna,” amesema.

Waziri Mkuu, Majaliwa amesema malalamiko hayo ya wananchi wa Kiwalala lazima yafanyiwe kazi, hivyo amemuagiza mkuu wa mkoa wa Lindi, Zambi kuhakikisha anakwenda kwenye kata hiyo kulipatia ufumbuzi suala hilo.

“Kweli kuna miradi ambayo inaelekezwa na watu kwa viongozi kuwa imekamilika wakati bado, namuagiza mkuu wa mkoa kulifanyia kazi jambo hili,” amesema.

Pia amesisitiza kwamba serikali hii si ya kuleana, mtu atakayebainika kukwamisha miradi ya maendeleo watamalizana naye hapo hapo, hivyo aliwaomba wananchi kuwa na subira kwani taarifa yao imepokelewa na inafanyiwa kazi.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa huo, Zambi amesema tayari ameshapata taarifa za tatizo la mradi huo na kwamba atafanya ziara kwenye eneo hilo na mtu atakayebainika kutafuna fedha za mradi huo atamuwajibisha hapo hapo kwa sababu yeye hataki kutumbuliwa.
 

                                                                     Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni