Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe
(katikati) akiwa na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini,
wakisikiliza maelezo kutoka kwa Meneja wa Mgodi wa Tanzanite, Emmanuel Mbise
ulioko Kitalu B, Mirerani. Mgodi huo unamilikiwa na Mchimbaji Mdogo, Ester
Ndosi.
Kamishna Msaidizi wa
Madini, Kanda ya Kaskazini, Elias Kayandabila, akifafanua jambo kwa Wajumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, walipotembelea Mgodi wa madini
ya Tanzanite wa Franone uliopo Kitalu D, Mirerani. Wa kwanza Kulia ni Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, anayeshughulikia Madini, Profesa
James Mdoe.
Kaimu Kamishna wa
Madini, Mhandisi Ally Samaje (Kulia), akimwonyesha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara
ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe (Kushoto),
namna Kiberenge kinavyofanya kazi ya kushusha watu na vifaa chini ya ardhi
kunakochimbwa madini ya Tanzanite, wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Nishati na Madini katika Mgodi wa Tanzanite One uliopo Mirerani, hivi
karibuni.
Na Veronica
Simba - Mirerani
Kuwepo
kwa mitobozano ya mara kwa mara baina ya wachimbaji wadogo wenyewe kwa wenyewe
na kati ya Mgodi wa Tanzanite One na wachimbaji wadogo wa Tanzanite katika
vitalu B na D, kumeelezwa kuwa ni changamoto inayosababisha kukosekana kwa
usalama katika eneo la machimbo ya Tanzanite, Mirerani kutokana na kutumika kwa
silaha za moto na mabomu ya kutengenezwa kienyeji.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, Profesa
James Mdoe aliyasema hayo hivi karibuni mkoani Arusha, wakati wa ziara ya
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kukagua Migodi mbalimbali
inayochimba madini hayo eneo la Mirerani.
Akielezea
maana ya mitobozano, Profesa Mdoe alisema ni hali ya wachimbaji kuvuka mipaka
ya leseni zao na kuingia katika maeneo ya wachimbaji wengine wakiwa chini
ya ardhi.
Kutokana
na tatizo hilo, Profesa Mdoe alisema kuwa Serikali, kupitia Wizara ya
Nishati na Madini, hususan Ofisi ya Madini Mirerani, inaendelea na juhudi za
kuwaelimisha wachimbaji na wadau wote wa sekta ya madini katika kuhakikisha
wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria za nchi ikiwemo Sheria ya
Madini ya Mwaka 2010 na kanuni zake pamoja na Sheria ya Baruti ya mwaka 1963 na
kanuni zake za mwaka 1964.
Akifafanua
zaidi, Profesa Mdoe alisema kuwa, mbali na kuwataka wachimbaji kufuata sheria,
pia kumekuwepo na juhudi za kuwakutanisha wachimbaji wa Kitalu C na Vitalu B na
D ili kuweka namna ambavyo uchimbaji unaweza kufanyika kwa kuepuka
mitobozano.
Aidha,
alieleza kuwa Wizara ya Nishati na Madini imekuwa ikishirikiana na Kamati za
Ulinzi na Usalama za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara katika kudhibiti
utoroshaji wa Tanzanite.
Alisema,
wataalam wa Wizara kupitia Ofisi ya Madini Mirerani, Mamlaka ya Udhibiti wa
Madini Tanzania (TMAA ) na Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO),
wameongeza udhibiti wa Tanzanite kwenye maeneo ya uzalishaji chini mgodini.
"Kazi
hii inafanyika kwa kuhakikisha kuwa maafisa husika wanakuwepo wakati wa
uzalishaji ili kufahamu kiasi kinachozalishwa, " alisema Profesa Mdoe.
Vilevile,
alieleza hatua nyingine zinazochukuliwa na Serikali kutatua tatizo hilo kuwa ni
pamoja na kuandaa maonesho ya vito ya kimataifa ambayo hufanyika Arusha kila
mwaka ambapo wanunuzi wa kimataifa kutoka nchi mbalimbali hukutana moja kwa
moja na wauzaji wakubwa wa ndani hivyo kupunguza uwezekano wa wafanyabiashara
kuendelea kutorosha Tanzanite.
Alisema
kuwa, Serikali imeanzisha masoko ya ndani yatakayokuwa yanafanyika Mirerani
kila mwaka na ina mpango wa kuanza ujenzi wa soko kubwa Mirerani ili madini
yote yatakayozalishwa yaweze kuuzwa, kukatwa na kusanifiwa Mirerani.
Kwa
upande wao, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, waliitaka
Serikali pamoja na mambo mengine, kuhakikisha migogoro iliyopo katika machimbo
hayo ya Tanzanite Mirerani inatafutiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni