Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa,viongozi wa dini na kimila huku mamia ya wakazi wa Shinyanga wakijitokeza kwa wingi kumsikiliza mkuu huyo wa mkoa. Akiwahutubia wakazi wa Shinyanga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela ambaye anakuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga wa 19 tangu nchi ipate uhuru na mwanamke pekee kuongoza mkoa huo,amesema amekuja mkoani Shinyanga kwa ajili ya kumsaidia rais John Pombe Magufuli kuwaletea maendeleo wananchi kwa kutekeleza kauli mbiu ya Hapa Kazi tu.
Kilango amesema atahakikisha tatizo la uhaba wa madawati katika shule za mkoa wa Shinyanga linamalizika haraka iwezekanavyo huku akisisitiza nia yake ya kutaka mkoa kushika nafasi ya kwanza mfululizo katika matokeo ya mitihani mbalimbali kitaifa pamoja na kwamba tangu mwaka 2012 hadi 2015 mkoa umekuwa ukishika nafasi ya kwanza na ya pili katika matokeo ya kidato cha nne.
Mkuu huyo wa mkoa aliyepewa jina la Mbula amepongeza viongozi wa mkoa kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa mauaji ya vikongwe na albino na kuhamasisha jamii kuachana na mila na desturi zilizopitwa na wakati. Katika hatua nyingine Kilango ambaye amekuwa mbunge kwa kipindi cha miaka mitano amesema hatakuwa kiongozi wa kukaa ofisini na badala yake atakuwa kiongozi anayewatembelea wananchi ili kutatua matatizo yao.
"Nitatenga walau siku moja kila wiki kuwatembelea wananchi katika mitaa na vijiji...watendaji wa serikali walioko chini yangu,nataka kuanzia leo iwe mwisho kunyanyasa wananchi,naombeni msikilize kero zao badala ya kuwapa majibu ya ovyo ovyo",ameeleza Kilango.
"Zile shilingi milioni 50 alizoahidi mheshimiwa rais wakati wa kampeni za uchaguzi zitaletwa,naomba mzitumie vizuri,nataka mkoa huu uwe wa mfano kwa maendeleo,naombeni ushirikiano,naahidi kushirikiana kwa ukaribu pia na viongozi wa dini,hawa ni watu muhimu sana",ameongeza Kilango Pamoja na mambo mengine wazee wa kimila/machifu wa kabila la Kisukuma wamesimika mheshimiwa Kilango kuwa chifu wa kisukama na wamemkabidhi dhana mbalimbali za kimila mkuu huyo wa mkoa ili azitumie katika uongozi wake kuwaongoza wananchi wa Shinyanga ambao wengi wao ni wasukuma.
Viongozi hao wa kimila pia wamemtangaza mheshimiwa Anne Kilango Malecela kuwa "Kanumba" maana yake mtendaji na msimamizi mkuu kwa mkoa na kumpa jina la Kimila "Mbula" likiwa na maana ya mvua.
Mkuu huyo wa mkoa pia ameombewa dua na viongozi wa dini waliohudhuria mkutano huo ambao umefurahiwa na wakazi wengi wa mkoa wa Shinyanga waliodai kuwa haijawahi kutokea mkuu wa mkoa akajitambulisha kwa wananchi mara tu anapoteuliwa kushika nafasi hiyo.
"Mbula" ni jina kiongozi mkubwa wa kimila,Mbula alikuwa mganga wa 33 kati ya waganga 54 maarufu nchini Tanzania. Mwandishi mkuu wa Malunde1 blog,Kadama Malunde alikuwepo eneo la tukio ametuletea picha 22 angalia hapa chini
Mkuu mpya wa mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela "Mbula" akiwa ameshikilia mkuki wenye kengele ukiwa na ishara kwamba asikike kila anapopita
Mkuu mpya wa mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela "Mbula" akikalishwa kwenye kiti cha kimila na mke wa Chifu Charles Njange kutoka Kizumbi katika manispaa ya Shinyanga,Kiti hicho maana yake ni ishara ya busara na hekima
Mkuu mpya wa mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela akiwa ameshikilia dhana za kimila
Baadhi ya wenyeviti wa serikali za mitaa katika manispaa ya Shinyanga wakitafakari jambo baada ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela kuondoka uwanjani. Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni