Kutokana
na kukua kwa huduma za kibenki kupitia simu za mkononi (mobile
banking), Watanzania wametakiwa kutumia nafasi hiyo vizuri ili iweze
kuwasaidia kukuza uchumi wao.
Akizungumza
na waandishi wa habari katika mkutano wa siku mbili unaozungumzia
maendeleo ya sekta za fedha kwa kutumia mifumo ya huduma za kibenki kwa
kutumia mitandao ya simu (Africa Digital Banking Summit), Naibu Waziri
wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji amesema ni muda muafaka kwa
Watanzania kutumia huduma hizo kwa ajili ya kujiongezea kipato.
Alisema
kupitia huduma hizo, Watanzania wanaweza kutuma nakupokea pesa kutoka
maeneo mbalimbali hata ambayo yapo mbali na matawi ya benki hivyo
wanaweza kufanya shughuli mbalimbali ikiwepo kufanya biashara kwa
kutumia huduma hizo.
“Serikali
imeunganisha nchi nzima na mkongo wa taifa na hii inawapa fursa
watanzania kutuma pesa sehemu yoyote hivyo niwasihi watanzania kutumia
kikamilifu nafasi hiyo ili kuboresha uchumi wao,” amesema Dkt. Kijaji.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji akitoa hotuba katika mkutano huo. (Picha zote na Rabi Hume, Modewjiblog)
Nae
Mkurugenzi Mkuu wa NMB nchini, Ineke Bussemaker amesema kuwepo kwa
huduma za kibenki kupitia mitandao ya simu kumewezesha wateja wao kupata
huduma kirahisi tofauti na miaka ya nyuma kabla ya kuanza kwa huduma ya
mobile banking.
Alisema
kupitia huduma hiyo kwa sasa wateja wao wanauwezo wa kutoa fedha,
kulipia huduma mbalimbali kama kodi, kununua umeme, tiketi za ndege na
hata kuangalia salio lililo katika akaunti zao za benki na
wanachokifanya kwa sasa ni kuangalia jinsi gani wanaboresha zaidi huduma
hizo kwa wateja hasa walio maeneo ya vijijini.
“Miaka
ya nyuma kama mteja yupo kijijini anatumia muda mwingi kwenda sehemu
iliyo na huduma ya benki lakini kwa sasa huduma za kibenki katika
mitandao ya simu imerahisisha hata wateja wetu walio vijijini kupata
huduma zetu kiurahisi,” amesema Bi. Bussemaker.
Nae
Meneja wa Mifumo wa Malipo wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Bernard Dadi
amesema huduma za kibenki kwa kutumia mitandao ya simu imekuwa ikizidi
kukua siku baada ya siku tangu ilipoanza nchini mwaka 2008 na mpaka sasa
kuna benki 30 ambazo zimejiunga katika mfumo huo ili kuwasogezea huduma
wateja wake.
Meneja Mifumo ya Malipo wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Bernard Dadi akitoa taarifa kuhusu matumizi ya mobile banking nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni