Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MKUU
wa mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana ameipongeza timu ya Uchukuzi SC kwa
kuleta wachezaji wengi kwenye mashindano ya Mei Mosi yaliyoanza Aprili
18 mwaka huu kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma.
Mh. Rugimbana
katika hotuba ya ufunguzi wa mashindano hayo iliyosomwa jana na Afisa
Maendeleo Vijana wa ofisi ya mkuu wa mkoa, Tumsifu Mwasambale kwa niaba
yake, alisema kuwa amedokezwa na waandaaji kuwa Uchukuzi SC ndio timu
pekee iliyoweza kuleta wachezaji wengi, hivyo anawapongeza viongozi wao.
“Ninaipongeza Uchukuzi SC pamoja na kudokezwa pia nimeona kwa
macho yangu wakati wa maandamano ya timu zikiingia uwanjani kuwa
Uchukuzi SC ndio wenye wachezaji wengi zaidi, nawapongeza sana viongozi
wao, wanatambua umuhimu wa michezo mahala pa kazi,” alisema.
Kwa
mujibu wa Katibu Mkuu wa timu ya Uchukuzi SC, Alex Temba amesema timu
yake imekuja na wachezaji takribani 96 ambao watashiriki kwenye michezo
ya kuvuta kamba, netiboli, riadha, kuendesha baiskeli, soka, bao, karata
na darts.
Tayari timu hiyo inayoundwa na wachezaji kutoka
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Bandari (TPA), Anga (TCAA), Hali ya
Hewa (TMA) na Chuo cha Bandari (DMI), imeshinda kwenye mechi zake za
soka dhidi ya Ukaguzi magoli 3-1 na upande wa netiboli waliwafunga CDA
magoli 23-15.
Hatahivyo, Mh. Rugimbana aliwashutumu na kusema
sababu zilizotolewa na viongozi hao kuzuia timu zao kushiriki kwenye
mashindano ya mwaka huu kwa kisingizio cha Mh. Rais John Magufuli kuzuia
michezo hii, hazina mashiko na ni kisingizio kilichopaswa kukemewa
vikali.
Alisema hajawahi kumsikia Mh. Rais Magufuli akizuia
michezo ya Mei Mosi, na mingine yeyote bali walimsikia akitoa maelekezo
ya kuzuia sherehe za Uhuru na sasa Muungano, na kutoa maelekezo na
tayari yanmefatwa kwa ufanisi mkubwa na wahusika.
“Ni uoga
usiokuwa na mashiko, kwani hata ingekuwa Mh Rais kazuia michezo, hata
Mh. Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) asingekuwa na nguvy ya kukutana na
viongozi wa mashirikisho na vyama vya michezo Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam, takribani miezi mitatu iliyopita wakijadili uimarishaji wa
michezo, na walaumu sana viongozi waliowanyima haki wanamichezo
kushiriki kwenye michezo hii,” alisema Rugimbana.
Mashindano ya
mwaka huu yenye kauli mbiu ya hapa kazi tu isiwe kisingizio kwa waajiri
kuondoa michezo kazini, yamekuwa na idadi ndogo ya washiriki, ambapo
hadi jana ni timu 14 pekee ndizo zilizofika Dodoma.
Hatahivyo,
awali Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mei Mosi, Joyce Benjamin,
naye katika hotuba ya ufunguzi aliwalaumu viongozi kuzuia timu zao kwa
kumsingizia Mh. Rais kuwa amezuia michezo.
“Kumbukeni Mh. Rais
wetu ni mmoja wa wanamichezo na ndio maana hata wakati wa kampeni
tulimuona wote akipiga pushapu jukwaani, sasa iweje leo hii viongozi wa
sehemu za kazi waseme amekataza michezo, michezo huu ni mikubwa imepata
Baraka zote kutoka TUCTA (Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi) na Baraza
la Michezo la Taifa (BMT),” alisema Benjamin.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni