DC SIMANJIRO AWAPA WIKI MOJA WAJUMBE WA SEREKALI YA KIJIJI KURUDI OFISINI LA SIVYO UTAFANYIKA UCHAGUZI MWINGINE WA VIONGOZI


Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Lucas Mweri akisoma mapendekezo mbalimbali kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika juzi (kushoto) ni Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Jackson Sipitieck.
Na Mahmoud Ahmad,Simanjiro

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara Mahmoud Kambona ametoa wiki moja kwa wajumbe 12 wa Serikali ya Kijiji cha Kambi ya Chokaa waliosusa kutumikia nafasi hiyo kurejea ofisini au uchaguzi mwingine ufanyike.

Inadaiwa kuwa wajumbe hao walisusa kufanya kazi wakipinga kuchaguliwa Mwenyekiti Mbuki Mollel badala ya Joshua Kuney, hivyo shughuli za utawala kwenye kijiji hicho zinashindwa kufanyika kutokana na kutokuwepo uongozi.

Kambona alitoa agizo hilo juzi mbele ya baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo kwani michango na huduma za kijamii hazifanyiki na kiongozi aliyepo ni mtendaji wa kijiji pekee tangu mwaka juzi uchaguzi ulipofanyika.

Alisema anawapa muda wa wiki moja viongozi hao warudi ofisini na endapo hawatakubaliana na hali hiyo uchaguzi ufanyike upya kujaza nafasi hizo il ishughuli za kiutawala wa kijiji hicho ziendelee kwa manufaa ya wananchi.

Kwa upande wake, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Lucas Mweri alibainisha vyanzo vya mapato vinavyotarajiwa kukusanywa na halmashauri ambavyo awali vilikuwa vinakusanywa na vijiji.

“Vyanzo vya ushuru wa mchanga, kuni kavu na samaki wakavu, ambavyo awali vilikuwa vinakusanywa na vijiji, hivi sasa vitakusanywa na halmashauri kisha itatoa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya vijiji husika,” alisema Mweri.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Jackson Sipitieck, alisema makusanyo na ushuru unapaswa kufanywa na halmashauri, kisha inarudisha kwa jamii kutokana na kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Huko vijijini ndipo kunaliwa fedha za ushuru na michango mbalimbali, hivyo halmashauri itakusanya na kurudisha kwa kujenga shule, barabara, zahanati na kuibua miradi mingine ya maendeleo kama inavyofanya,” alisema Sipitieck.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni