TIGO WAKABIDHI MADAWATI 400 KWA WILAYA YA MWANGA KATIKA SHULE NANE

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Meck Sadiki akikabidhi madawati 400 yenye thamani ya shilingi milioni 66 kwa mwenyekiti wa halmashauri ya Mwanga Theresia Msuya yaliotolewa na Kampuni ya Tigo, Kulia ni Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Kaskazini George Lugata.

Kampuni ya Tigo Tanzania imetoa msaada wa madawati 400 yenye thamani ya shilingi milioni 66 kwa shule nane za msingi katika manispaa ya Mwanga, mkoa wa Kilimanjaro, ikiwa ni mchango wa kampuni hiyo katika kuisaidia serikali kukabiliana na upungufu wa madawati katika shule za msingi nchini.

Akizungumza leo katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika shule ya msingi Reli Juu katika manispaa ya Mwanga, Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Kaskazini George Lugata amesema mchango huo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya kampuni hiyo ya kuunga mkono jitihada mbalimbali za kuleta maendeleo nchini.

“Mchango huu ni sehemu ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Tigo katika kusaidia utekelezaji wa miradi yenye tija kubwa kwa jamii. Tunaamini kwamba kupitia msaada huu, Tigo inatoa mchango wake katika kujenga viongozi wa baadayewa taifa hili na wanataluuma mbalimbali wakiwamo madaktari, wahandisi na wengineo, “amesema Lugata.

Lugata amesema mwaka jana Tigo ilikabidhi msaada kama huo wa madawati katika shule za msingi katika mikoa ya Shinyanga, Mbeya Iringa na Morogoro na kuongeza kwamba kampuni hiyo itaendelea kutoa madawati zaidi sehemu mbalimbali nchini siku za zijazo.

Makabidhiano yalihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro mheshimiwa Meck Sadiki ambaye alisema madawati hayo 400 yataboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto katika Mkoa wa Kilimanjaro na kutoa wito kwa wadau wengine kuunga mkono zoezi hilo.

“Tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa kampuni ya Tigo kwa kuwa mdau muhimu kwetu katika jitihada zinazoendelea za kujaribu kupunguza tatizo la ukosefu wa madawati ya kutosha katika shule za msingi za mkoa wetu wa Kilimanjaro. 
 
Ni dhahiri kwamba msaada huu wa madawati 400 yatawawezesha mamia ya wanafunzi wetu kupata sehemu za kukaa na hivyo kujipatia elimu zao katika mazingira bora zaidi,” alisema Sadiki

Madawati hayo yametolewa kwa shule za msingi nane kama ifuatavo, Mramba,Kawawa, Mwanga, Naweru,Kiboriloni, Lawate na Reli Juu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni