Watendaji
wakuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake wakimsikiliza Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipowasilisha bungeni Mapitio na Mwelekeo
wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za
Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka 2016/2017.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasilisha bungeni Mapitio na Mwelekeo wa
Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi
ya Waziri Mkuu kwa Mwaka 2016/2017.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Wenhye Ulemavu, Jenista Mhagama (kushoto) na Naibu wake, Dktt. Abdallah
Posi wakiteta bungeni mjini Dodoma Aprili 22, 2016.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya
Mifugo, Mwigulu Nchemba, Bungeni Mjini Dodoma Aprili 20, 2016.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Feza ambao
Aprili 22, 2016 walikwenda Bungeni mjini Dodoma kwa ziara ya mafunzo.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Afisa Habari wa Chuo Kikuu cha
Dar es salaam, Hamis Dambaya (katikati) na Mhadhiri Msaidizi wa Chuo
Kikuu cha Dar es salaam , Egbert Mkoko kwenye viwanja vya Bunge Mjini
Dodoma Aprili 22, 2016.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana
nchini kimepungua kwa asilimia 2.5 na kwamba Serikali itaendeleza juhudi
za kuvutia uwekezaji ili kupunguza zaidi kiwango hicho.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Aprili 22, 2016) wakati akiwasilisha
mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2016/2017 bungeni mjini Dodoma.
“Utafiti
wa hali ya ajira nchini wa mwaka 2014 umeonesha kuwa kiwango cha
ukosefu wa ajira kimepungua kutoka asilimia 11.7 mwaka 2006 hadi
asilimia 10.3 mwaka 2014. Aidha, ukosefu wa ajira kwa vijana umepungua
kutoka asilimia 14.2 mwaka 2006 hadi asilimia 11.7 mwaka 2014,”
amesema.
Waziri
Mkuu amesema moja ya changamoto zinazosababisha ukosefu wa ajira ni
vijana kutojengewa maarifa na ujuzi wa kuajiriwa na kuajirika. Hivyo, Serikali itaendelea kutekeleza Programu ya Miaka Mitano ya Kukuza Ujuzi Nchini (2015/2016 – 2019/2020).
“Programu
hiyo inalenga kuongeza idadi ya watu wenye kiwango cha juu cha ujuzi
kutoka asilimia tatu ya sasa hadi asilimia 12 inayotakiwa kuendesha
uchumi wa viwanda. Vilevile, kupunguza idadi ya watu wenye kiwango cha
ujuzi wa chini kutoka asilimia 75 ya sasa hadi asilimia 54,” amesema.
Amewaagiza
watendaji wakuu wa wizara, idara zinazojitegemea, wakala za serikali,
taasisi za umma, mikoa na mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha kuwa
ukuzaji wa ajira unakuwa ni agenda ya msingi ya kudumu katika
utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumzia kuhusu vitendo
vya ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu hususan watu wenye ualbino,
Waziri Mkuu amesema Serikali inafanya jitihada kubwa kukomesha vitendo
hivyo ikiwa ni pamoja na kuwakamata wote wanaojihusisha na vitendo hivyo
na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
“Ukatili
huo umesababisha watu wenye ualbino kupoteza maisha na wengine kupata
ulemavu wa kudumu. Hali hiyo haikubaliki na haivumiliki katika jamii ya
Watanzania. Napenda kusisitiza watu wenye ulemavu wana haki ya
kuthaminiwa utu wao na kulindwa dhidi ya ukatili na aina yoyote ya
ubaguzi,” amesema.
Waziri
Mkuu amesema katika mwaka ujao wa fedha, Serikali itaviboresha Vyuo vya
Ufundi na Marekebisho (Vocational and Rehabilitation Training
Centres) vya watu wenye ulemavu nchini ili kutoa ujuzi unaoendana na
mahitaji yao katika soko la ajira ikiwa ni pamoja na kuandaa walimu wa
elimu maalum na kutoa vifaa saidizi kwa walimu na wanafunzi wenye
ulemavu mashuleni.
Akitoa
maelezo kuhusu juhudi za Serikali kuwawezesha wananchi kiuchumi, Waziri
Mkuu amesema Serikali imesaidia uanzishwaji wa taasisi mwavuli ya
kusimamia VICOBA inayoitwa VICOBA FETA ambayo imeanza kuonyesha matunda
mazuri.
“Takwimu
zilizotolewa mwezi Februari 2016 na taasisi hiyo zinaonesha kuwa kuna
vikundi 100,000 vya VICOBA vyenye wanachama milioni 2.2 na mtaji wa
shilingi trilioni 1.2. Ni jambo la kujivunia kwamba asilimia 79 ya
wanachama wa VICOBA ni wanawake,” amesema.
Amezitaka
Halmashauri zote nchini ziweke orodha sahihi ya vyama vya ushirika wa
kuweka na kukopa vilivyosajiliwa kwa kila kijiji na kuchukua hatua za
kuwezesha uanzishaji na usajili wa SACCOs zinazokidhi vigezo kulingana
na shughuli za uzalishaji katika Halmashauri husika.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
IJUMAA, APRILI 22, 2016.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni