MWADUI v AZAM, COASTAL v YANGA NUSU FAINALI KOMBE LA SHIRIKISHO

Droo ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) imefanyika usiku huu moja kwa moja (live) kupitia kituo cha luninga cha AzamTwo, huku timu za Coastal Union na Mwadui FC zikipata nafasi ya kucheza nyumbani.

Katika droo hiyo iliyochezeshwa na mchezaji mstaafu wa timu ya timu ya taifa ya wanawake (Twiga Stars), Esther Chaburuma, imewashuhudia vigogo wa Ligi Kuu ya Vodacom, Azam FC na Young Africans wakipata nafasi ya kucheza michezo hiyo katika viwanja vya ugenini.

Mwadui FC watakua wenyeji wa Azam FC katika mchezo unaotarajiwa kucheza Aprili 24, 2016 mjini Shinyanga, huku wagosi wa Kaya Coastal Union wakicheza dhidi ya Young Africans katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga siku hiyo hiyo.

Washindi wa michezo hiyo ya Nusu Fainali, watakutana fainali ya kombe hilo itakayofanyika mwezi Mei, ambapo Bingwa wake ataiwakilisha Tanzania katika michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF CC).

Wakati huo huo wadhamini wa michuano hiyo Azamtv kupitia kituo chake cha michezo cha Azam Sports, leo wameweza kulionyesha hadharani kwa mara ya kwanza kombe la ubingwa kukikabidhi kwa Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni