MADINI YATANZANITE YALIYOKAMATWA YAPIGWA MNADA HADHARA

Na Mahmoud Ahmad,Arusha
Hatimaye serikali imeamua kuyapiga mnada madini ya vito aina ya
Tanzanite yaliyokamatwa yakisafirishwa nje ya nchi bila vibali ambapo
jumla ya kiasi cha sh,1.6 bilioni zimepatikana mara baada ya madini
hayo kupigwa mnada.

Akizungumza mara baada ya kufunga maonyesho ya tatu ya kimataifa ya
madini ya vito jijini hapa kamishna wa madini kanda ya kazkazini,Elias
Kayandabila alisema kwamba zoezi la mnada huo bado linaendelea na
wanatarajia kupata kiasi cha zaidi ya sh,2.5 bilioni.

Kayandabila,aliliambia gazeti hili ya kwamba lengo kuu la kuyapiga
mnada wa madini hayo hadharani ni kuweka uwazi kwenye mauzo ya madini
hayo nchini na kuwapa fursa wafanyabiashara wakubwa na wadogo
kushiriki biashara hiyo kwa uwazi.

Akizungumzia maonyesho ya tatu ya kimataifa ya madini ya vito
yaliyofungwa juzi kamishna huyo alisema kwamba kumekuwa na mafanikio
lukuki yaliyojitokeza ikiwa ni pamoja na kuwapa fursa wauzaji wadogo
wa kushiriki maonyesho hayo tofauti na miaka ya nyuma.

Alitaja mafanikio mengine yaliyojitokeza ni pamoja na wauzaji hao
kununua madini yanayochimbwa katika mgodi wa Tanzanite One tofauti na
miaka ya nyuma ambapo kampuni hiyo ilikuwa ikiyauza madini hayo kwa
wauzaji wakubwa pekee.

“Kitendo cha kuruhusu hawa wauzaji wadogo wa madini kushiriki
maonyesho haya ni cha kipekee huko nyuma hawakuwahi kupata nafasi hii
“alisema Kanyandambila

Hatahivyo,kamishna huyo alitoa wito kwa wizara ya nishati na madini
nchini kuhakikisha wanavutia nchi mbalimbali kuja kushiriki maonyesho
hayo ikiwa ni pamoja na kuziondolea mlolongo wa kodi na usajili kabla
ya kushiriki kwa lengo la kuongeza idadi ya washiriki mwakani.

Baadhi ya washiriki katika maonyesho hayo walisema kwamba maonyesho
hayo yamekuwa na mafanikio makubwa mwaka huu huku wakiiomba serikali
kuhakikisha inatoa ushirikiano wa dhati katika kuyapa nguvu mwakani.

Mkurugenzi wa kampuni ya madini ya vito ya Crown Lapidary,Rajan Verma
pamoja na mkurugenzi wa kampuni ya madini ya vito ya Tom Gems ,Thomas
Munisi walisema kwa nyakati tofauti kwamba maonyesho hayo yatakuwa na
mafanikio katika siku za usoni endapo yakipewa uzito mkubwa na idadi
ya wageni ikiongezeka.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni