Serikali
 imewataka wawekezaji wa ndani na nje kutumia fursa zilizopo Tanzania 
hasa katika eneo la kuongeza thamani ya malighafi mbalimbali.
Wito
 huo umetolewa na Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
 Dkt. Adelhelm Meru alipokuwa akiongea na maafisa kutoka kampuni ya 
nchini Ufaransa ya Endel Engie mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Maafisa
 wa kampuni hiyo walikuwa nchini na kufanya mazungumzo na viongozi 
mbalimbali waandamizi wa serikali kueleza nia yao ya kuwekeza Tanzania 
na kujua fursa zilizopo nchini.
Endel moja ya makampuni ya Engie Group yenye mapato yanayofikia Euro milioni 700 kwa mwaka na waajiriwa 6,000 nchini Ufaransa.
Baadhi
 ya shughuli za kampuni hiyo ni katika maeneo ya sayansi za anga, 
viwanda vya vyakula, reli, gesi, ujenzi wa meli, nishati ya nyuklia na 
viwanda vya chuma miongoni mwa vingine.
Kwa bara la Afrika, kampuni hiyo inafanya kazi katika nchi za Afrika ya Kusini, Angola na Congo DRC.
Akizungumza
 na waandishi wa habari baada ya mkutano huo, Dkt. Meru alisema eneo la 
kuongeza thamani bado halijafanyiwa kazi na lina fursa kubwa kwa watu 
wanaotaka kuwekeza katika viwanda vya aina hiyo.
“Kama serikali tunaweka mazingira mazuri ya kuhakikisha kuwa watu wanawekeza kwa faida ya pande zote mbili,” alisema.
Aliwaambia
 maafisa wa kampuni hiyo kuwa utulivu wa kisiasa na amani iliyopo 
Tanzania vinaifanya kuwa eneo bora la kuwekeza katika ukanda huu wa 
Afrika.
Kampuni hiyo iko katika mchakato wa kutafuta fursa na vivutio vya kuwekeza katika nchi za Tanzania, Kenya na Msumbiji.
Aliyataja
 maeneo mengine yenye fursa za kuwekeza kama madini, Kilimo, utafutaji 
wa gesi na mafuta na uzalishaji nishati miongoni mwa nyingine.
Makamu
 wa Rais, Maendeleo ya Kimataifa, Endel Engie, Bw. Olivier Rousseau 
alisema wamevutiwa na hali ya amani, utulivu na raslimali katika eneo 
hili la Afrika na hasa Tanzania.
“Tuko katika ziara ya kujifunza,” alisema.
Kwa
 mujibu wa afisa huyo, mwezi wa Kumi mwaka huu, wawakilishi wa kampuni 
hiyo, watarudi Tanzania na mapendekezo rasmi ya maeneo watakayokuwa 
wanataka kuwekeza hapa nchini.
Mbunge
 mstaafu wa jimbo la Mbinga Magharibi ambaye aliambatana na wawekezaji 
hao, Bw. Gaudence Kayombo alisema huu ni wakati wa kuitikia kwa vitendo 
azma ya serikali ya kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda.
Alisema uwekezaji katika maeneo hayo utasaidia kuleta teknolojia, mitaji na uzoefu Tanzania.
Serikali
 imedhamiria kuwa ifikapo mwaka 2020, asilimia 40 ya ajira zote  na 
asilimia 15 ya pato la Taifa vitokane na sekta ya viwanda.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni