UDHIBITI WA SILAHA ZA MAANGAMIZI UNAHITAJI UTASHI WA KISIASA-TANZANIA

Silaha  kama  hizi  ( Pichani) na nyinginezo nyingi  na ambazo mataifa mbalimbali  yanaendelea kujilimbikizia  si tu zinataharisha  uhai wa sayari dunia lakini pia uhai wa mwanadamu na viumbe hai.  Jumuiya  ya Kimataifa imekuwa ikikuna vichwa na kujiuliza  nini kitatokea  endapo silaha hizi ambazo zimeshindwa kudhibitiwa zitangukia mikononi mwa magaidi na makundi mengine ya kiharamia.  Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu upunguzaji na udhibiti wa silaha za nyukilia na za maangamizi imeanza mkutano wake wa wiki   mbili  hapa Umoja wa Mataifa.

Wakati Kamisheni  ya Umoja wa Mataifa kuhusu upokonyaji wa  silaha za maangamizi  zikiwamo za  nyukilia kushindwa kwa miaka  kumi na tano kuwasilisha taaria ya mapendekezo ya kina kuhusu utekelezaji wa jukumu hilo, Tanzania kwa upande wake imeungana na  mataifa mengine   katika kutoa wito wa  kuhakikisha kwamba silaha  za maagamizi haziangukii  mikononi mwa magaidi na makundi mengine hatari.

Jana Jumatatu, Kamisheni kuhusu ukoponyaji wa  silaha,   imeanza mkutano wake wa wiki mbili ambapo   washiriki wanajadiliana na  kubadilishana mawazo kuhusu dhima ya upokonyaji wa silaha za maangamizi na masuala mengine yahusianayo na silaha. Akichangia majadiliano  katika siku ya kwanza ya mkutano , Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, amesema, utashi wa kisiasa unahitajika  hasa kutoka kwa nchi ambazo  zinamiliki  silaha za  nyukilia  na  silaha ninyingine za maangamiii ili  kuifanya dunia   iendele kuwa mahali salama.

Akabainisha kwamba kutonyesha nia ya kweli ya kudhibiti malimbikizo ya silaha hizo na, kwa Kamisheni kutowasilisha mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa   ripoti yake  kwa kipindi cha miaka  kumi na tano sasa ni wazi kwamba  kunatoa mwanya  wa silaha hizo kuangukia mikononi mwa makundi ya kigaidi na mengineyo.

Ni katika kuliongopa hilo  Tanzania kupitia kwa mwakilishi wake, Balozi  Manongi imeeleza kwamba   hoja ya kwamba kwa nchi kumiliki silaha za maangamizi zikiwamo za nyukilia kunazifanya   nchi hizo kuwa na  nguvu  lakini pia kujenga mazingira ya  Amani kuwa haina tija  wala matinki yoyote.

“ Suala la upunguzaji  wa silaha za nyukilia  na  silaha nyingine za maangamizi ni  jambo linaloitia wasi wasi mkubwa nchi yangu, ni wazi kwamba hatari zitokanazo na nyukilia ziwe kwa  bahati mbaya,  za kimkakati au  kukosewa kwa mahesabu siyo tu kunaitishia dunia  lakini pia na wanadamu”. akasema Balozi

Na kuongeza kwamba “ Tanzania  inaendelea kuikata ile dhana kwamba kwa namna moja silaha ya nyukilia zinatoa dhamana ya uwepo wa  Amani. Kwa upande wetu hatujawahi kujihisi tukiwa na Amani kwa misingi ya  kwamba  silaha hizo amana zinamilikiwa na  rafiki  zetu au washirika  wao”.

Balozi Manongi ametahadharisha kuwa ,  katika  mazingira ya sasa ambapo  pamekuwapo na ongezeko  kubwa la  makundi yasiyo ya kiserikali yanayotaka kuzipindua serikali halali, hakuna uhakika kwamba makundi hayo  hayawezi kugeukia mbinu zozote zile ambazo zinaweza kuingia mikononi mwao.

Kuhusu  Kamisheni ya   Umoja wa Mataifa kutowasilisha  ripoti yoyote mbele ya  Baraza Kuu    kwa miaka  kumi na  tano,  Balozi Manongi asema. Kamisheni hiyo haiwezi kukwepa majukumu yake   na hasa kama inataka  kuendelea kujijenga uhalali.

“Baraza  Kuu la Umoja wa Mataifa,  limetoa wito wa kuitaka  Kamisheni ifanye tathmini  na kutoa  mapendekezo kuhusu matatizo mbalimbali katika eneo  hili la upokonyaji wa silaha, na  kutoa  maamuzi ya utekelezaji. Mapendekezo ya  Kamisheni kwa Baraza Uuu  yanatakiwa kutekelezwa na huu ni wajibu wa msingi wa Kamisheni”. akasisitiza Balozi Manongi.

Pamoja  na  mapungufu kwa upande wa Kamisheni,  Tanzania imesema bado na  Imani   na Kemisheni hiyo na inaitambua  kama chombo pekee  halali na  chenye maamuzi  katika Umoja wa Mataifa kuhusu  upunguzaji wa silaha za  maangamizi..

Awali akizungumza  mwanzoni mwa mkutano wa Kamisheni, Mwakilishi  Maalum  wa Masuala ya  upokonyaji wa silaha,  Bw. KIM  won-soo, pamoja na  mambo mengine alikiri kwamba   Kamisheni ilikuwa inaingia katika kipindi  kingine ambapo  kuna mgawanyiko  mkubwa  miongoni wa  jumuiya ya kimataifa kuhusu upokonyaji wa silaha za nyukilia na silaha nyingine za maangamizi.

Akasema kila mjumbe anafahamu kuhusu mgawanyiko huo. Ambao  umejidhihirisha wazi kuanzia mkutano wa majereo kuhusu Mkataba wa upunguzaji  na usambazaji wa silaha za nyukilia ( NPT) uliofanyika mwaka jana,  kushindwa kuanza kwa utekelezaji wa mkataba  unaozuia majaribio ya silaha za nyukilia, na kutokuwapo kwa mwendelezo wa majadiliano katika  mkutano kuhusu upunguzaji wa silaha.

 Hata hivyo na kama ilivyokuwa kwa wajumbe wengine, Bw. KIM  won –soo alionyesha matumaini yake kwa Kamisheni  ya Umoja wa Mataifa kuhusu  upunguzaji wa silaha za nyukilia  za  maangamizi  na kwamba wajumbe wake wakifanya kazi  kwa pamoja na  ushirikiano  na bila kutiliana mashaka hapata kuwa na sababu ya  kuwenda kutafuta njia mbadala nje ya Umoja wa Mataifa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni