GAVANA AZINDUA MWONGOZO WA KWANZA WA KITAIFA WA ELIMU NA ULINZI KWA MTUMIAJI WA HUDUMA ZA FEDHA” (N-FEF).

Meza kuu ikifuatilia kwa makini yanayojiri katika kikao cha uzinduzi wa Mwongozo wa kwanza wa kitaifa wa elimu na ulinzi kwa mtumiaji wa huduma za fedha” (N-FEF).
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania akieleza jambo wakati wa uzinduzi Mwongozo wa kwanza wa kitaifa wa elimu na ulinzi kwa mtumiaji wa huduma za fedha” (N-FEF).
Bi. Susan Rutledge, Mtafiti na Mshauri wa masuala ya fedha, akieleza umuhimu wa elimu ya masuala ya fedha kuelekezwa kwa wananchi.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa kushirikiana na Mfuko wa Kuendeleza Huduma za Kifedha Tanzania (FSDT), imezindua Mwongozo wa taifa wenye lengo la kuongeza uelewa kuhusu elimu ya mambo ya fedha kwa wananchi.
 

Uelimishwaji wa wananchi kuhusu mambo ya fedha utatekelezwa kupitia “Mwongozo wa kwanza wa kitaifa wa elimu na ulinzi kwa mtumiaji wa huduma za fedha” (N-FEF). 

Gavana Prof. Beno Ndulu ameuzindua rasmi mwongozo huu ambao utajikita katika kutatua changamoto zilizobainishwa katika utafiti uliopima uelewa wa mambo ya fedha kwa watu wazima nchini Tanzania. Utafiti huu unaitwa “Uwezo wa Kifedha Tanzania” wa mwaka 2014. 

Utafiti huo umebainisha kuwa watanzania wengi hawana elimu na ujuzi mahususi wa masuala ya mambo ya fedha kwa ujumla, hivyo kuwanyima fursa ya kutumia huduma za kifedha kwa faida yao. 

Katika utafiti huo imeonyeshwa kuwa upatikanaji wa huduma za fedha umekuwa na changamoto katika maeneo mengi huku zile zitolewazo kwa njia ya mitandao bado hazikidhi matarajio ingawa zinawafikia wateja wengi kwa sasa. 

Sambamba na hilo kumekuwa na uhaba wa nyenzo na miundombinu ya kuhifadhi na kufikisha taarifa za fedha kwa watumiaji wa huduma hizo kwa kuzingatia namna sahihi ya kutoa taarifa, kuwaelimisha na kuwalinda.
 

Kutokana na utafiti wa “Uwezo wa Kifedha Tanzania” wa mwaka 2014 wananchi kutoka makundi mbalimbali katika jamii hawana ujuzi wa hesabu za kawaida ambao ndiyo msingi mkuu katika nadharia ya masuala yahusuyo mambo ya fedha. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni