Na Frank Geofray wa Jeshi la Polisi.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini
IGP Ernest Mangu amewataka Makamanda wa Polisi kote nchini kuendesha
oparesheni kali ya kuwachukulia hatua kali za kisheria waendesha
pikipiki maarufu kama bodaboda wasiotii sheria za usalama barabarani
ikiwemo kubeba abiria zaidi ya mmoja, kupita katika taa nyekundu pamoja
na kutovaa kofia ngumu.
IGP Mangu alitoa kauli hiyo
wakati akizungumza na Maafisa wakuu wa Polisi wakiwemo Makamanda wa
Polisi wa mikoa, vikosi na makao makuu katika kikao kazi kilichokuwa
kikifanyika jijini Dar es Salaam ambacho kilifunguliwa na Waziri wa
Mambo ya Ndani ya nchi.
Alisema waendesha bodaboda
wamekuwa wakikaidi kufuata sheria za usalama barabarani lakini sasa
mwisho wao umefika na kuwataka makamanda wa polisi wa mikoa kote nchini
kutekeleza maelekezo hayo ili kuleta nidhamu kwa bodaboda katika kufuata
sheria za usalama barabarani.
IGP Mangu alisema suala la
kufuata sheria za usalama barabarani kwa bodaboda halina mjadala na kila
kamanda ahakikishe kuwa wale wote wasiofuata sheria na kukaidi
wanakamatwa bila kuoneana muhali kwakuwa wamekuwa wakisababisha ajali
zinazoweza kuzuilika.
“ Pamoja na kuendelea kudhibiti
uhalifu wa aina zote, natoa maelekezo kwa kila mkoa kuhakikisha
unaendesha oparesheni kali dhidi ya bodaboda ili kupunguza ajali
zinazosababishwa na bodaboda ambao wengi wao hawataki kufuata sheria na
kanuni za usalama barabarani, tusiwaonee muhali maana maisha ya watu ni
muhimu sana na jambo la msingi ni kusimamia sheria tu” Alisema IGP
Mangu.
Awali akifungua kikao
kazi hicho Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mh. Charles Kitwanga
alilitaka Jeshi la Polisi kuendelea na mapambano yake dhidi ya uhalifu
na wahalifu ili usalama wa raia na mali zao uendelee kuimarika na
watanzania waendelee na shughuli zao za kujiletea maendeleo bila hofu ya
kutendewa uhalifu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni