Ombi hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na Balozi wa Mataifa ya Umoja wa Falme za Kiarabu aliyepo Nchini Tanzania Bwana Abdullah Ibrahim Al – Suwaidi hapo Ofisi za SMZ Mtaa wa Magogoni Jijini Dar es salaam.
Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefikia hatua ya kuanzisha Kituo cha Kimataifa cha usajili wa Vyombo vya Baharini { Tanzania Zanzibar International Register Shipping } baada ya kuifutia Mikataba Kampuni ya Filtex iliyokuwa ikifanya kazi hiyo kama Wakala wa Zanzibar katika kazi hiyo.
Alisema Kampuni ya Filtex ilishindwa kutekeleza majukumu yake katika kiwango kinachokubalika Kimataita cha Usajili wa Vyombo vya Baharini na kufikia hatua za kusajili Meli zisizo na kiwango na kupelekea kuibebesha sifa mbaya Zanzibar katika sekta hiyo.
Balozi Seif alieleza kwamba lengo la kuanzishwa kwa Kituo hicho ni kuijengea uwezo zaidi Zanzibar katika kujitanua Kibiashara katika Nyanja za biashara ya Kimataifa.
Akizungumzia hali ya Kisiasa Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuhakikishia Balozi huyo wa Mataifa ya Falme za Kiarabu Bwana Abdullah Ibrahim kwamba Zanzibar bado ina Amani na utulivu hasa kipindi hichi inachoelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa marudio unaotarajiwa kufanyika mnamo Tarehe 20 Mwezi ujao.
Alisema Wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba hivi sasa wanaendelea na harakati zao za kimaisha bila ya bughdha licha ya kasumba zinazoendelea kusambazwa na baadhi ya vyombo vya Habari pamoja na Mitandao ya Kijamii inayoeneza na kutishia wageni kwamba Zanzibar hakuna tulivu katika kipindi hichi.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Sekta muhimu ya utalii imekuwa na inaendelea kutoa huduma kama kawaida ambapo watalii na wageni wanatumia fursa hiyo kupata mapumziko na burudani katika visiwa vya Viungo.
Naye Balozi wa Mataifa ya Umoja wa Falme za Kiarabu aliyepo Nchini Tanzania Bwana Abdullah Ibrahim Al – Suwaidi alimuhakikishia Balozi Seif kwamba Umoja wa Falme za Kiarabu utaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika jitihada zake za kuimarisha uchumi na Maendeleo ya Wananchi wake.
Balozi Abdullah Ibrahim alisema Umoja huo utakuwa tayari kuona mpango wa Zanzibar katika kuimarisha Kituo hicho unakamilika baada ya kumaliza taratibu zote za usajili ili kitoe huduma rasmi.
Alisema hivi sasa kitachosubiriwa na Uongozi wa Umoja huo ni Barua rasmi ya Maombi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar baada ya kukamilika kwa taratibu zinazosimamiwa na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Ushirikiano wa Kimataifa Tanzania.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana kwa mazungumzo na Ujumbe wa Wawekezaji wa Kampuni ya Kimataifa inayosafirisha Mafuta { Asean Petroleum Business } nyumbani kwake Mtaa wa Osterbay Bara bara ya Haile Selasie Jijini Dar es salaam.
Katika mazungumzo yao ujumbe huo ukiongozwa na Bwana Karim Jamal ulimueleza Balozi Seif azma ya Kampuni hiyo kutaka kuwekeza miradi yao ya kiuchumi Zanzibar kutokana na mazingira rafiki ya Kibiashara yanayovizunguuka Visiwa vya Unguja na Pemba.
Bwana Jamal alisema Kampuni yake yenye uzoefu wa kusambaza mafuta katika Mataifa mbali mbali Duniani imejipanga kuanzisha Kituo cha Kimataifa cha utoaji wa huduma za Mafuta kwa meli zinazofanya safari za kusafirisha mizigo na Abiria katika Bahari ya Hindi.
Alisema utafiti umeonyesha kwamba zaidi ya Meli 30,000 hufanya safari zake katika eneo la mwambao wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika ambazo wakati mwengine Meli hizo hukabiliwa na usumbufu wa kupata huduma hiyo muhimu.
“ Tumeamua kuiteua Zanzibar katika kutekeleza mradi huo ili ipate upendeleo wa kusimamia na kutoa huduma hizo kutokana na mazingira yake bora ya Kibiashara kwa miaka mingi ilizopita ”. Alisema Bwana Karim Jamal.
Kiongozi huyo wa Kampuni ya Asean Petroleum Business alifahamisha kwamba Uongozi wa Taasisi hiyo umependelea watendaji wake kufanya kazi Zanzibar ili kusaidia mapato ya Taifa zambamba na kuisaidia Serikali katika jitihada zake za kupunguza wimbi la ajira.
Alisema upendeleo huo umekuja zaidi baada ya kuzingatia kwamba Kizazi cha baadhi ya watendaji wa Taasisi hiyo asili na nasaba yao kimezaliwa katika Visiwa vya Zanzibar miaka mingi iliyopita.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuhakikishia Uongozi wa Kampuni hiyo ya usafirishaji wa mafuta baharini {Asean Petroleum Business} kwamba utapewa ushirikiano na Serikali kuu katika kuona lengo walilolikusudia kulitekeleza linafanikiwa vizuri.
Kampuni ya usafirishaji mafuta kwa njia ya Bahari { Asean Petroleum Business } tayari imekuwa ikitoa huduma za usambazaji wa Mafuta kwa Nchi mbali mbali za Mashariki ya Kati, India, Visiwa vya Mauritius pamoja na Dar es salaam Tanzania.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
25/2/2016.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni