Serikali yatoa wito wafanyabiashara wa Mauritius kuwekeza nchini.

Mkurugenzi wa Uhamasishaji Biashara na Masoko wa Wizara ya Viwanda na Biashara Odilo Majengo akipokea maelekezo ya bidhaa kutoka kwa mwakilishi wa kampuni ya SLK Gold Taste wakati wa Mkutano na Maonyesho ya kibiashara ya kimataifa ya Mauritius jana Jijini Dar es Salaam. Wengine ni Mkurugenzi wa huduma za kibiashara wa Tantrade, Fidelis Mugenyi (kushoto) na Balozi wa heshima wa Mauritius, Abbas Rizvi. 
 Mkurugenzi wa Uhamasishaji Biashara na Masoko wa Wizara ya Viwanda na Biashara Odilo Majengo akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa Mkutano na Maonyesho ya kibiashara ya kimataifa ya Mauritius jana Jijini Dar es Salaam. Wengine ni Balozi wa heshima wa Mauritius, Abbas Rizvi (kulia) na Meneja wa kampuni ya Enterprise Mauritius, Rajen Subbamah,
 Meneja wa kampuni ya Enterprise Mauritius, Rajen Subbamah akizungumza wakati wa mkutano na maonyesho hayo
 Mkurugenzi wa TICC, David Lutabana akiongea wakati wa shughuli hiyo
 Baadhi ya washiriki wakifuatilia mkutano huo.
Washiriki wa maonyesho wakitembelea baadhi ya wafanyabiashara


Serikali imeahidi kuendelea kuboresha mazingira rafiki kwa wawekezaji ili kuongeza miradi ya uwekezaji ili kufikia lengo na Dira ya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara Bw. Charles Mwijage wakati wa ufunguzi wa Mkutano na Maonyesho ya kibiashara ya kimataifa ya Mauritius yakilenga kujenga mahusiano na kutizama fursa za kibiashara baina ya mataifa haya mawili jana Jijini Dar es Salaam.

Alisema moja kati ya jitihada zinazofanywa na serikali ni pamoja na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano kufanya baadhi ya mambo ambapo sasa usajili wa kampuni unaweza kufanywa mtandaoni.

“Natoa wito kwa ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Mauritius kuwekeza nchini kutokana na uwepo wa rasilimali za kutosha, bandari pamoja na soko la uhakika kwani nchi yetu inapakana na nchi saba ambazo muwekezaji anaweza kuuza bidhaa huko kwa urahisi,” alisema Mh. Mwijage katika hotuba yake iliyosomwa naMkurugenzi wa Uhamasishaji Biashara na Masoko wa Wizara ya Viwanda na Biashara Odilo Majengo.
Maonyesho hayo yanaandaliwa na kampuni ya Talemwa Investment Consulting Company (TICC) pamoja na  Enterprise Mauritius kwa ushirikiano na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) na Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA).
Awali akiongea wakati wa mkutano huo, Mkurugenzi wa TICC, Bw. David Lutabana alisema maonyesho hayo ni fursa ya kipekee inayowakutanisha wafanyabiashara kutoka nchi hizi mbili ili kuweza kubadilishana uzoefu pamoja na kujadili fursa mbalimbali zilizopo katika nchi hizo.
Akizungumza wakati wa shughuli hiyo, Meneja wa kampuni ya Enterprise Mauritius, Rajen Subbamah, alisema sekta zinazoshiriki kutoka Mauritius ni pamoja na sekta ya ukandarasi, bidhaa za kilimo, kemikali, viwanda vya utengenezaji nguo na vidani, pamoja na sekta zingine.


“Nchi yetu ina uhaba mkubwa wa malighafi na kwa upande mwingine Tanzania imebarikiwa kwa kiasi kikubwa kuwa na rasilimali mbalimbali. Kupitia mkutano huu tunatizamia kujenga mahusiano na wafanyabiashara wa hapa Tanzania ili tuweze kufanya biashara zitakazonufaisha pande zote mbili,” alisema Bw. Subbamah.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni