WAZIRI MBARAWA AIAGIZA HALMASHAURI YA BUSEGA KUTUMIA MFUMO WA KIETRONIKI KATIKA UKUSANYAJI WA MAPATO

HALAMASHAURI ya wilaya ya Busega mkoani Simiyu imeagizwa kuanza mara moja kutumia mfumo wa kietroniki kuanzia sasa kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato kwa ajili ya utoaji wa huduma safi kwa jamii.

Agizo hilo limetolewa jana na Waziri wa Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano nchini Mh.Makame Mbarawa wakati alipokuwa anakagua miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo.

Mbarawa alisema kuwa mfumo huo utawasaidia katika kurahisisha kazi mbalimbali na pia utaongeza mapato ya serikali na kupunguza wizi unaotokana na matumizi mabaya ya hundi ambao umekuwa ukiinyima serikali kipato cha kutosha.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa halmshauri hiyo Gaudencia Bamugileki amesema kuwa watahakikisha wanatekeleza agizo hilo la waziri ndani ya mwezi huu ili kuondoa changamoto zilizopo kwa wanajamii.

Alipongeza kuwa mfumo huo na kusema kuwa " ni mzuri sana katika ukusanyaji wa mapato na hata kutaifanya halmashauri yangu kupaa kimaendeleo kwani tutakusanya mapato mengi na hivyo kuweza kupiga hatua kubwa katika maendeleo na kufanya wilaya hiyo kuwa ni ya mfano wa kuigwa ndani ya nchi hii, alisema.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya hiyo Paul Mzindakaya amempongeza Waziri Mbarawa na kuweza kumhakikishia kuwa mashine hizo zitapatikana ndani ya mwezi huu na kuanza kazi kama kawaida ili ziweze kuiongezea kipato serikali yetu kwa ujumla.

Pia Mzindakaya aliongeza kuwa mashine hizo zikija inapaswa kutumika vizuri kwani watu wamekuwa na akili mbaya za kuchakachua mashine hizo, hivyo kwa wale watakao bainika kufanya hivyo wajiandae kuachishwa kazi .

Aidha mkuu huyo wa wilaya alimpongeza Waziri Mbarawa kwa jitihada zake katika shughuli za maendeleo na kumuomba asichoke kuwasaidia wanabusega katika maendeleo.
 

 
                                                                               Habari na Shushu Joel,Busega.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni