PROF. MBARAWA ATOA MWEZI MMOJA KWA MAKANDARASI.

 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akifafanua jambo kuhusu ukusanyaji madeni ambayo Wakala wa Majengo nchini (TBA) inadai wapangaji wake. 
 Muonekano wa barabara ya Sakina-Tengeru Km 14.1 inayojengwa kwa njia nne kwa kiwango cha lami ili kupunguza msongamano wa magari kuingia na kutoka katikati ya jiji la Arusha. 
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akijadiliana jambo na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Fadhili Nkurlu jijini Arusha.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (kulia) akikagua ripoti ya biashara inayofanywa na Kampuni ya Simu nchini (TTCL), jijini Arusha. Wa tatu kulia ni Meneja Kanda ya Kaskazini TTCL Bw. Peter Lusama. 
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (katikati) akiimba wimbo wa mshikamano daima na wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS kabla ya kufungua rasmi mkutano wa sita wa Baraza hilo. Kulia ni Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Patrick Mfugale na kushoto ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Fadhili Nkurlu. 
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akisisitiza kufanya kazi kwa malengo yanayopimika katika kikao chake na wafanyakazi wa taasisi zilizo chini ya wizara yake, jijini Arusha. 

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa mkandarasi M/S Hanil Jiangsu J/V anayejenga barabara ya Sakina-Tengeru Km 14.1 na barabara ya mchepuo wa kusini Arusha bypass Km 42.4 jijini Arusha.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. 


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ametoa mwezi mmoja kwa makandarasi wote nchini kuhakikisha wanasaini mikataba ya ajira na wafanyakazi katika miradi ya ujenzi wa barabara inayoendelea nchini kote.
Akizungumza jijini Arusha mara baada ya kufanya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Sakina-Tengeru yenye urefu wa Km 14.1 na barabara ya mchepuo ya kusini (Arusha bypass) yenye urefu wa Km 42.4, Prof. Mbarawa amesema mkandarasi atakayeshindwa kutoa mikataba kwa mujibu wa sheria za Tanzania, atanyang’anywa kazi ya ujenzi kwa kuvunja sheria.
“Barabara zinajengwa kwa kodi za wananchi hivyo wajenzi wa barabara nao ni lazima wafuate sheria za nchi ili kuhakikisha Serikali inapata kodi stahili na wafanyakazi wazawa nao wanapata haki stahili kwa mujibu wa ajira zao", amesema Waziri Prof. Mbarawa. 
Amezitaka taasisi za TRA, NSSF na nyingine zinazosimamia ajira za wafanyakazi kufuatilia miradi ya ujenzi ili kuona fursa za mapato ambazo serikali inaweza kupata na kusajili wafanyakazi katika hifadhi ya mifuko ya jamii.
Waziri Prof. Mbarawa amewataka mameneja wa tanroads na maafisa kazi kukagua mikataba ya ajira za ujenzi katika maeneo yao ili kuona haki inatendeka kwa makandarasi na kwa wafanyakazi ili ujenzi wa barabara ukamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amefungua mkutano wa Sita wa Baraza la Wafanyakazi la Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) na kuwataka kuweka mikakati itakayowezesha kulinda hifadhi ya barabara, kudhibiti magari yanayozidisha uzito na kusimamia kasi katika miradi ya ujenzi wa barabara.
“Mmekua mkifanya kazi nzuri, endeleeni kufanya kazi kwa uadilifu, uwazi, weledi na kujiwekea malengo ya kujipima mwaka hadi mwaka ili muendelee kuwa tassisi ambayo watu watakuja kujifunza kwenu”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Patrick Mfugale amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa TANROADS imejipanga kuhakikisha miradi ipatayo 90 ya ujenzi wa barabara inayoendelea nchini kote inakamilika katika ubora unaotakiwa na unao uwiana na thamani ya fedha.
Aidha, Waziri Prof. Mbarawa amemuagiza Meneja wa Wakala wa Majengo nchini (TBA), mkoa wa Arusha, Bw. Victor Baltazar kukusanya madeni yote kwa haraka ili kukamilisha miradi ya ujenzi wa nyumba za wafanyakazi na za biashara inayosimamiwa na Wakala huo mjini Arusha kukamilika kwa wakati.
Prof. Mbarawa ambaye yuko katika ziara ya mikoa ya kanda ya kaskazini amezitaka taasisi zilizo chini wa wizara hiyo kuhakikisha zinafanya kazi kibiashara ili kuboresha mapato ya Serikali na hivyo kuiwezesha Serikali kutoa huduma bora kwa wananchi.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni