Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo
Vikuu Tanzania Prof Yunus Mgaya akizungumza na waandishi wa habari
(hawapo pichani) Kuhusu uamuzi wa Tume kufuta usajili wa vyuo vikuu
vishiriki vya Mtakatifu Joseph tawi la Songea. Picha na Raymond
Mushumbusi MAELEZO
……………………………………………………………………………………..
Na Nyakongo Manyama MAELEZO
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU)
imeamua kufuta kibali kilichoanzisha vyuo vikuu viwili vishiriki vya
Mtakatifu Joseph ambavyo ni Chuo Kikuu kishiriki cha Sayansi ya Kilimo
na Teknolojia (SJUCAST) na Chuo Kikuu kishiriki cha Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano (SJUIT) vilivyopo Songea.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika ofisi za Tume hiyo, Katibu Mtendaji wa Tume
ya Vyuo Vikuu Tanzania Prof Yunus Mgaya amesema kutokana na mapungufu
yaliyobainishwa na Tume ambayo ni matatizo ya ubora wa elimu na
ukiukwaji wa Sheria za uendeshaji wa Chuo Kikuu kama ulivyobainishwa na
Sheria ya Vyuo Vikuu hii imepelekea Tume kuchukua hatua ya kufuta
usajili wa vyuo hivyo.
“ kutokana na yaliyobainishwa
hapo awali tunapenda kutaarifu umma kwamba ,Tume imejiridhisha kuwa hivi
vyuo vikuu vishiriki viwili havitoi elimu ya Chuo kikuu ya viwango
stahiki na ukizingatia wanafunzi katika Vyuo hivi ndio waathirika
wakubwa wa matatizo yaliyopo”Alisema Prof Mgaya.
“Napenda kufafanua kwamba Vyuo
vikuu vishiriki tuliyovifutia usajili ni tawi la Songea na Vyuo vingine
vishiriki vya Mtakatifu Joseph vilivyopo Dar es Salaam na Arusha
vitaendelea kufanya kazi kama kawaida”Alisema Prof Mgaya.
Prof Yunus Mgaya amesema
wanafunzi wote wanaosoma katika vyuo vishiriki vilivyofutwa usajili
wanaarifiwa kuwa watahamishiwa kwenye vyuo vikuu vingine vinavyofundisha
programu za masomo zinazofanana na masomo wanayosoma hivi sasa chini ya
utaratibu uliopangwa.
Amevitaja vyuo ambavyo
watapelekwa wanafunzi walipo katika vyuo vishiriki vilivyofutwa usajili
kuwa ni Chuo Kikuu cha kilimo Sokoine (SUA), Chuo Kikuu cha Dodoma
(UDOM),Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge(MWECAU) na Chuo Kikuu cha
Kikatoliki cha Ruaha(RUCU).
Amesisitiza kuwa orodha ya
majina ya wanafunzi na vyuo watavyohamishiwa yatawekwa kwenye tovuti ya
Tume hivi karibuni na wale wote wanaonufaika na Mikopo toka Bodi ya
Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, mikopo yao itahamishiwa katika vyuo
watakavyokuwa wamehamishiwa.
Vyuo vikuu vyote chini
vinakumbushwa kufata Sheria na kuzingatia utoaji wa elimu inayokidhi
viwango vya ubora vinavyokubalika kitaifa na kimataifa, hivyo Tume
haitasita kuchukua hatua stahiki kwa chuo kikuu chochote
kitakachobainika kutoa elimu isiyokidhi viwango vya ubora kwa kisingizio
cha aina yoyote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni