TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI NEC NA UNDP ZAFANYA MIKUTANO YA MAJADILIANO KUBORESHA UTOAJI ELIMU YA MPIGA KURA


KALIMANI
Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Bw. Ramadhan Kailima alipozindua kituo Cham mawasiliano ambapo Jumla ya Simu 1,381 zilipokelewa katika kituo cha Mawasiliano cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi – Nec Call Center, kilichoanzishwa mahususi kwa lengo la kuwasaidia wapiga kura pamoja na wadau mbalimbali wa uchaguzi ili kupata elimu ya mpiga kura.
……………………………………………………………………………………………………………..…..
Na Lydia Churi-NEC
Hivi karibuni, Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana na Mradi wa ukuzaji wa Demokrasia nchini (DEP) chini ya shirika la Maendeleo la Kimataifa (UNDP) iliandaa mikutano ya tathmini ya utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura  wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka jana ili kujadiliana juu ya kuboresha utoaji wa Elimu hiyo katika Chaguzi na kuboresha ushirikiano kati ya Tume na Wadau mbalimbali wa Uchaguzi.
Mikutano hiyo pia ililenga kuainisha maeneo ambayo wadau wanataka yafanyiwe marekebisho ili  kuboresha utendaji kazi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika kukuza Demokrasia nchini na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa Chaguzi.
Mikutano hiyo ilifanyika kwa Kanda kwa kuwashirikisha Mwenyekiti wa Tume na Makamishna, Mkurugenzi wa Uchaguzi Wakuu wa Idara pamoja na Maafisa Kutoka Tume ya Taifa ya uchaguzi na Mikoa iliyoalikwa kwenye Mkutano huo.
Mikutano hii ilifanyika kuanzia Februari 2 hadi 11, mwaka huu katika miji ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Lindi, Mtwara, Mbeya, Rukwa na Katavi. Miji mingine ni pamoja na Pwani, Dar es Salaam, Morogoro, Unguja, Pemba, Dodoma, Singida, Tabora, Kigoma, Kagera, Mwanza, Geita, Shinyanga, Mara, Simiyu,  Ruvuma, Njombe na Iringa.
Aidha, Mikutano hiyo ilishirikisha wadau mbalimbali wa Uchaguzi wakiwemo wawakilishi wa Asasi za Kiraia wa makundi mbalimbali ya jamii kama vile Wanawake, Vijana, Watu wenye Ulemavu, na Wazee. Wengine ni Waratibu wa Uchaguzi wa Mikoa (Regional Election Coordinators), Wasimamizi wa Uchaguzi wa Majimbo ambao pia ni Wakurugenzi wa halmashauri (Rertuning Officers), Maafisa Uchaguzi na Maafisa Habari kutoka kila Halmashauri ulipofanyika mkutano wa wadau.
Kwa mujibu wa Ibara ya 74(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kifungu cha 4C cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, imepewa jukumu la kutoa Elimu ya Mpiga Kura na kusimamia Asasi, Makundi au watu wanaotoa Elimu hiyo. 
Kwa kuzingatia umuhimu wa jukumu hilo, Tume ilishirikisha Asasi za Kiraia 447 katika kuhamasisha wananchi na kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kushiriki na kujitokeza kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na pia kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Asasi za Kiraia ni wadau wakubwa katika mchakato wa Uchaguzi kwa kuzingatia ukweli kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi peke yake haiwezi kuwafikia Watanzania wote kutokana na kutokuwa na rasilimali watu ya kutosha katika kuwafikishia Elimu ya Mpiga Kura pamoja na utaalamu mbalimbali wa utoaji wa Elimu hasa jinsi ya kuwafikia watu wenye mahitaji maalumu kama walemavu, wanawake, vijana pamoja na wale walioko pembezoni na maeneo yasiyofikika kwa urahisi kwa sababu mbalimbali zikiwemo za miundombinu

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni