SERIKALI YAELEZA MPANGO WA KUJENGA MAABARA ZA MKEMIA MKUU KILA KANDA NCHINI

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu.Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu.   
                                                                        Na Modewjiblog team
Uongozi wa Rais Magufuli unaonekana kujikita zaidi katika kutatua matatizo yanayowakabili wananchi na kuhakikisha inaboresha huduma wanazopatiwa wananchi kwa kuwasogezea huduma hizo karibu zaidi.
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu ameeleza mpango wa serikali kujenga maabara za wakala wa mkemia mkuu wa serikali kwa kanda zote nchini.

Mhe. Mwalimu aliyasema hayo wakati wa makabidhiano ya gari la huduma za dharura (ambulance) la kituo cha kitaifa cha kuratibu matukio ya sumu zinazofanyika wakala wa maabara ya mkemia mkuu wa serikali na kueleza kuwa serikali inataka kufanya ujenzi huo ili kuwasogezea wanachi huduma kwa ukaribu zaidi.

“Serikali kupitia wizara yangu imekuwa ikifanya jitihada za kuboresha huduma za wakala kulingana na uwezo uliopo ili kuhakikisha kuwa wakala unaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi,

“Baadhi ya jitahada hizo ni pamoja na, kuanzisha maabara za kanda ili kusogeza huduma karibu na wananchi na kuendeleza ujenzi na ukarabati wa majengo ya wakala,” alisema Mhe. Mwalimu.

Aidha Mhe. Mwalimu alisema tayari wizara yake imeshapeleka muswada bungeni ili bunge litunge sheria ambayo itampa wakala uwezo wa moja kwa moja kisheria kufanya kazi na kutekeleza majukumu kwa uhakika na ufanisi.

Pia Waziri wa Afya amewataka wananchi na taasisi mbalimbali kuiamini maabara hiyo kwa kuitumia kufanya vipimo wanavyohitaji bila kuwa na mashaka.

Hata hivyo katika maadhimisho hayo, Mhe. Ummy Mwalimu alizindua cheti cha Ithibati (Accreditation ISO 1705:2005) ambacho kinaifanya maabara hiyo kutambulika kimataifa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni