Na Mwandishi wetu
MAHAKAMA ya Mwanzo Mbagala, Dar es Salaam
imesema haiwezi kumuamuru Mmiliki wa nne za Shule za Sekondari, St
Mathew na St Marks ,Thadei Mtembei kutoa talaka kwa Magreth Mwangu
kutokana na ndoa yao kuwa batili.
Akisoma hukumu hiyo leo, Hakimu Rajab
Tamambele alisema ndoa aliyofunga Mwangu pamoja na Mtembei ambayo ni ya
kimila ni batili kwa kuwa mdai hakutoa cheti cha ndoa hiyo ilipofungwa.
Alisema kwa misingi hiyo, mahakama
haiwezi kumuamuru Mtembei kutoa talaka kwani aliwasilisha cheti cha ndoa
ya mke mmoja aliyoifunga mwaka 1985.
pia alisema mahakama hiyo haiwezi kugawa
mali kama ambavyo mdai ameiomba mahakama, ambapo amesisitiza kuwa
mgawanyo wa mali unatokana na ndoa halali ambayo baba na mama wanaishi
pamoja.
‘’Mashahidi wote wameeleza kuwa Mtembei
na Mwangu walikuwa wanakutana hoteli ya Sleep Inn. Kwa hivyo mahakama
inaona kuwa uhusiano kati ya mdai na mdaiwa ulikuwa wa kimapenzi pekee
au hawara na kwa lugha ya kistaarabu tunaita mzazi mwenzie,’’ aliongeza
Tamambele.
Alifafanua kuwa kulipa mahari ambapo
mdai aliieleza mahakama kuwa alitolewa ng’ombe watano, sio njia ya
kufunga ndoa bali ni kuelekea kufunga ndoa.
Aliendelea kusema kuwa kitendo cha baba
kupewa mahari akiwa peke yake bila ya kuwa na mzee wa kabila hilo
kuthibitisha, sio sahihi katika sheria za ndoa.
Akisoma hukumu hiyo kwa saa moja, Hakimu
Tamambele alisema kuwa watoto watatu kati ya Mtembei na Mwangu ni batili
kwani wamezaliwa nje ya ndoa, hivyo mahakama haiwezi kuamuru watoto hao
kupatiwa matunzo.
‘’Mdaiwa anatakiwa kushukuru kitendo cha
mdai kujenga nyumba tatu kwa ajili ya watoto kwani wengine hawawezi
kufanya kitu kama hicho. Kila mzazi anatakiwa kuwatunza watoto hao, ’’
alisema.
Akizungumzia kuwakilishwa kwa mdaiwa,
alisema kwa mujibu wa sheria ya kama mdaiwa ni mgonjwa anaweza
akawakilishwa ambapo mtoto wake, Peter ndiye alichukua nafasi ya
kumuwakilisha baba yake.
Aidha, alisema haki ya kukata rufaa kwa mdai iko wazi na kwamba inatakiwa kukatwa kwa siku 45.
Katika kesi hiyo ambayo ilifunguliwa Juni
5, mwaka huu, Mwangu aliiomba mahakama kumuamuru mdaiwa kutoa talaka,
matunzo ya watoto na ya machumo ya pamoja yenye thamani ya Sh milioni
800.
Alisema kesi hiyo ilikuwa na jumla ya mashahidi nane ambapo watano kutoka upande wa mdai na watatu upande wa mdaiwa.
Alisema mdai alifungua kesi kupitia ofisi
ya Ustawi wa jamii na ilipoanza kusikilizwa mdai alisema walianza
mahusiano mwaka 1995 ambapo walizaa watoto watatu na walijenga shule
nne, nyumba pamoja na hoteli tatu za Dar es Salaam na Bukoba.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni