Mke wa zamani wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, Rose Kamili jana aliibuka na
kumtuhumu mzazi mwenzake huyo kwamba anatumiwa kuvuruga upinzani katika
kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu.
Katika mkutano
wake na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamili alitamka
bila kuthibitisha moja moja kwamba mumewe huyo wa zamani anatumiwa na
baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku akihoji uadilifu
wake katika jamii.
Lakini jana alipotafutwa kwa njia ya simu
kujibu madai hayo ya chama chake kumtumia Dk. Slaa kuusambaratisha
upinzani, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema hana
taarifa na hivyo apewe muda kabla ya kutoa taarifa kamili.
“Sina
taarifa kama Rose Kamili kazungumza na vyombo vya habari leo. Ndiyo
kwanza nasikia kwako, naomba unipe muda niweze kusoma yote aliyoyaeleza
ndipo nikujibu,” alisema Nape.
Katika mkutano wake jijini Dar
es Salaam juzi, Slaa aliyekuwa kimya kwa siku kadhaa alitangaza
kuachana na shughuli za siasa kutokana na kile alichoeleza kuwa ni
kutoridhishwa na mwenendo wa chama chake, hasa katika mchakato wa uteuzi
wa mgombea urais uliompa nafasi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
kuwa mgombea wa Chama hicho.
Dk. Slaa alimuelezea Lowassa
kama mtu asiye na maadili wala sifa ya kuwa Rais wa Tanzania kwa sababu
anahusika katika tuhuma kadhaa za ufisadi ikiwemo ile kashfa ya zabuni
ya kuzalisha umeme wa dharura iliyohusisha kampuni ya Richmond LLC na
baadaye Dowans.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar
es Salaam jana, Kamili anayedai kuzaa watoto wawili na Dk. Slaa,
alisema anachofanya sasa kiongozi huyo wa zamani wa Chadema, ni
kukamilisha sehemu ya kazi aliyotumwa na baadhi ya makada wa chama
tawala kwa nia ya kuisaidia katika kampeni za uchaguzi mkuu kwani ni kwa
muda mrefu alikuwa akifuatwa na kuahidiwa ubunge na uwaziri pindi
akikubali kuachana na Chadema.
Hata hivyo, Kamili naye
hakuweza kufafanua kama naye kwa hatua yake hiyo ya kujitokeza hadharani
kumshambulia mumewe huyo wa zamani, naye alikuwa katumwa, au ulikuwa ni
utashi wake binafsi.
Aidha hakuweza kuweka bayana ni kwa
nini hakujitokeza siku zote kuhoji uadilifu wa mume wake huyo wa zamani
tangu alipojitokeza kugombea urais mwaka 2010 kupitia chama cha Chadema.
Alisema
baadhi ya vigogo wa CCM ndiyo waliokuwa wakiongoza mpango huo,
wakimuahidi Dk. Slaa vyeo hivyo huku yeye akiahidiwa kiasi kikubwa cha
fedha kama akikubali pia kuachana na Chadema.
Hata hivyo,
Kamili aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum kupitia Chadema katika Bunge
lililovunjwa Julai 9 mwaka huu, alisema kuwa yeye alikataa ‘ofa’ hiyo na
kubakia katika chama chake, lakini kwa anachokifanya Dk. Slaa sasa, ni
dhahiri kuwa mzazi mwenzake amekubali kutumika na hivyo hatashangaa
akimuona kwenye majukwaa ya kampeni za CCM ili kumchafua mgombea wa
Ukawa na kukinadi chama tawala katika kampeni zinazoendelea.
Lakini
katika mkutano wake na waandishi wa habari Dk. Slaa alitamka bayana
kwamba anaachana na siasa na hana mpango wa kurudi CCM. Kamili alidai
kwamba Dk. Slaa vilevile aliitwa na kigogo mmoja ndani ya Kanisa
Katoliki na kushawishiwa akubali mpango huo wa kujiweka pembeni Chadema
na kuitumikia CCM.
Alisema baada ya kumalizana na Dk. Slaa
ndipo wakamgeukia yeye na kumtaka ahamie kwao (CCM) ili washirikiane
katika kampeni za CCM.
“Mimi nimekataa... ila yeye amekubali
na wakati wowote anaweza kutekeleza kazi aliyoianza kwa kupanda
majukwaani kushiriki kampeni za CCM,” alisema.
Lowassa na ufisadi
Aidha
alihoji Dk. Slaa kumuita mgombea urais wa Chadema kuwa ni fisadi,
akimtaka ajihoji yeye mwenyewe kuhusu matendo anayoyafanya katika
familia, kabla ya kuwahubiria wengine kuhusu maadili na misingi bora.
Kamili
alisema kabla ya Dk. Slaa kuhoji mambo ya Lowassa ajihoji yeye mwenyewe
kuhusu sababu zilizomfanya aondoke Baraza la Maaskofu Katoliki (Tec)
akiwa kama Katibu mkuu na pia Kasisi wa kanisa hilo.
Aidha
alikanusha taarifa zilizotolewa na Dk. Slaa kwamba yeye (Slaa) na
familia yake wamekuwa wakila mihogo kama sehemu ya kutunza uaminifu
wake, na kusisitiza kwamba kuwa siyo za kweli.
Kwa nini kajitokeza
Kamili
alisema aliamua kujitokeza kuzungumza hadharani ni baada ya mzazi
mwenziwe huyo kugusia masuala ya familia wakati alishaitelekeza kwa muda
mrefu, pale alipoamua kuishi na mchumba wake mpya Josephine
Mushumbusi.
Kwa mujibu wa Kamili, mbali na mzazi mwenziwe
kuitelekeza familia yake, hakuwa, pia hajawahi kuwa na maisha magumu
kiasi cha kula mihogo kama alivyodai, na kuongeza kwamba labda kama
alikuwa anazungumzia watoto wake (Slaa) ambao amewatelekeza.
“Alisema
yeye na familia yake wamekuwa wakila mihogo…hata kama mihogo ni
chakula, watoto wangu hawajawahi kula mihogo hata kama aliwatelekeza
labda watoto wake anaoishi nao. Huo ni uongo, ni upotoshaji. Atoe
ufafanuzi kw Watanzania hao watoto anaowazungumzia ni watoto gani. Kama
wewe ni muongo, huwezi siasa.” Kamili alisema
Kuhusu ndoa
Kamili alisema katika mkutano wa juzi, Slaa hakueleza kwa usahihi juu
ya suala la ndoa kwa kudai kuwa serikali ya CCM ndiyo iliyoweka
pingamizi dhidi ya maamuzi ya kufunga ndoa na mchumba anayeishi naye,
Josephine Mushumbuzi.
Badala yake, Kamili alisema maneno hayo
si ya kweli kwani yeye (Kamili) ndiye aliyeweka pingamizi hilo kwavile
ndiye mke wa halali na kwamba, haiingii akilini kwa taasisi kama CCM
kuweka pingamizi la ndoa ya mtu.
Alisema maneno hayo ni ya
uongo kwani yeye ndiye aliyeweka pingamizi hilo kwa sababu ndiye
aliyefunga naye ndoa na kwamba ingewezekana kuwekwa pingamizi na CCM
iwapoa alifunga ndoa na chama hicho.
Alisema yeye na familia
yake ya watoto wawili, Emiliana na Linus Slaa, wamekuwa wakimfichia siri
nyingi lakini kwa taarifa hizo zimemfanya kuibuka huku akimtaka kuomba
msamaha kwa kuwasema viongozi wa dini kwamba walipokea rushwa ya
mamilioni kutoka kwa Lowassa.
Kugombea urais
Kamili
alipinga madai ya Dk. Slaa kwamba hakuwa tayari kugombea nafasi ya urais
kupitia Chadema, akisema ukweli wa suala hilo unadhihirishwa na ziara
yake (Slaa) ya Ujerumani alikojifunza namna ya kuvaa na kujieleza mbele
ya hadhara wakati wa kampeni za uchaguzi.
Aidha, Kamili
alihoji ujasiri wa Dk. Slaa kumuita mgombea urais wa Ukawa, Lowassa kuwa
ni fisadi anautoa wapi wakati yeye (Slaa) amejawa na matendo
yanayotilia shaka uadilifu wake, baadhi yakiwa ni kumuacha mke wa ndoa
(yeye Kamili) na kuishi na mwanamke mwingine.
Kadhalika,
alidai sababu mojawapo ya Slaa kuondoka katika nafasi ya Katibu Mkuu wa
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (Tec) ni kukosa uaminifu na hivyo,
kamwe hastahili kumnyooshea kidole Lowassa kwa tuhuma za kuzushiwa
kuhusu kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni