MWANAHARAKATI KHADIJA LIGANGA ANUIA KUKUSANYA PEDI KWA AJILI YA MABINTI WANAOSOMA

Kutokana na Wasichana wengi walio Mashuleni kulazimika kukosa Masomo yao katika Kipindi cha hedhi, Mwanaharakati wa Kutetea haki za Wanawake na Wasichana nchini Khadija Liganga, amelazimika kuanzisha kampeni ya kukusanya pedi 3,000 ndani ya mwezi huu ili kuwasaidia wahitaji.

Akizungumza jana katika Kipindi cha Passion Break Fast kinachorushwa na Radio Passion Fm ya Jijini Mwanza, Liganga alibainisha kwamba ameamua kukusanya pedi hizo kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuziwasilisha katika Shule 10 za Msingi na Sekondari zilizo katika Mikoa ya Mwanza na Mara hii ikiwa ni maalumu kwa ajili ya wasichana wanafunzi ambao hawana uwezo wa kumudu kununua pedi hizo.

“Tarehe Moja mwezi wa Kwanza mwaka huu, wanawake tulikutana Jijini Mwanza chini ya mpango tuliouita Women Round Table kwa ajili ya kupanga mikakati mbalimbali ya kimaendeleo kwa mwaka huu 2016. 

Moja ya mikakati niliyoipanga ni pamoja kuanzisha mradi uitwao Binti Box ambao umelenga kusaidia uchangiaji na upatikanaji wa pedi kwa ajili ya wanafunzi wenye uhitaji mashuleni pamoja na kuwapa elimu ya namna ya kujiweka katika hali ya usafi wawapo katika kipindi cha hedhi”. Alisema Liganga na kuongeza kuwa mpango huo utakuwa endelevu.

Kumekuwepo na tatizo la wanafunzi wasichana katika maeneo mbalimbali nchini kukosa masomo yao katika kipindi cha hedhi huku baadhi yao wakilazimika kuacha shule kutokana na aibu wanayokumbana nayo wawapo shuleni hii ikiwa ni kutokana na kukosa elimu ya kutosha pindi waingiapo katika kipindi cha hedhi.

Unaweza kuungana na mwanaharaki huyo kwa kuchangia pedi ambapo anapatikana kwa nambari 0713 093 801 hiyo ikiwa ni kwa wale walio mbali na Jijini Mwanza ama waweza kutembelea ofisi za Dida Vitenge Wear zilizopo Nganza Sekondari barabara ya kwenda Chuo Kikuu cha SAUT jirani na ghorofa upande wa kushoto hapo.

                      Imeandaliwa na George Binagi-GB Pazzo wa Binagi Media Group

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni