SERA YA ELIMU YATAJWA KUCHANGIA TATIZO LA UKOSEFU WA AJIRA KWA VIJANA


Balozi wa Uswisi nchini, Florence Tinguely Mattli akitoa neno la ufunguzi katika mdahalo huru kuhusu ajira kwa vijana.
                           Wachangia mada katika mdaharo huru kuhusu ajira kwa vijana
                                                       Baadhi ya washiriki waliohudhuria mdahalo huo

       Washiriki wa mdahalo wakiwa katika makundi kujadili mada zilizotolewa

Katika kuadhimisha miaka 50 ya mahusiano na ushirikiano baina ya Uswisi na Tanzania, ubalozi wa Uswisi nchini umefanya mdahalo wa wazi kuhusu ajira kwa vijana ulioshirikisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ili kubadilishana mawazo jinsi wao wanavyofanya ili kupambana na tatizo la ajira.

Mdahalo huo ambao ulifanyika katika hoteli ya Coral Beach, jijini Dar es Salaam ulijadili mambo mbalimbali ambayo yanasababisha kuwepo kwa ajira chache lakini pia uwezo wa vijana wa kuingia katika soko la ushindani la ajira.

Aidha mdahalo huo uliweza kujadili kuhusu changamoto iliyopo ya ajira kwa vijana na kuependekeza njia mbalimbali ambazo zinaweza kutumika ili kukabiliana na tatizo hilo ambalo linaonekana kukua kwa jinsi siku zinavyokwenda.

Wakizungumza na Mo Dewji Blog baada ya kumalizika kwa mdahalo huo wadau mbalimbali ambalo walihudhuria walisema kuwa tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana linaanzia katika aina ya sera ambazo serikali inazitumia katika sekta ya elimu kushindwa kufanya kazi katika soko la ajira la sasa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema kuwa ili serikali kupunguza tatizo la ajira kwa vijana inatakiwa kuhakikisha inaimarisha uchumi wa nchi lakini ambao unatoa nafasi za ajira zaidi.

Alisema mbali na kuimarisha uchumi pia inatakiwa kuwatengenezea wananchi wake mazingira mazuri ambayo yatawashawishi kujiajiri bila kutegemea ajira ya serikali au makampuni binafsi ambayo kwa sasa ndiyo yanaonekana kutoa nafasi nyingi za ajira.

“Vijana wengi kwa sasa wakimaliza vyuo wanajiajiri na hata kama wanauza barabarani korosho huko nako ni kujiajiri … serikali inatakiwa kuimarisha uchumi wa nchi na sio kukuza tu lakini ukue na utoe fursa za ajira kwa wazawa,” alisema Eyakuze.

Aidha aliwataka vijana kuacha tabia ya kutegemea ajira za serikali na sekta binafsi kwani ushindani katika soko la ajira ni mkubwa na kama wanakuwa hawajajiandaa kwa kiasi kinachohitajika sasa katika soko la ajira basi inaweza kuwa ngumu kwao kupata nafasi.

Nae Amabalis Batamula kutoka Femina alisema sera ambazo zinatumika nchini hazitekelezwi kama zinavyopangwa na serikali na pia hazina faida kwa soko la ajira la sasa kutokana na kubadilika kwa jinsi miaka inavyozidi kwenda.

Alisema ni jambo la ajabu baadhi ya sera za elimu ni kuendelea kutumika hadi sasa licha ya soko la ajira kubadilika na hivyo kuhitaji sera mpya ambazo zinakwenda na wakati lakini pia kuwashauri vijana wanaohitimu kuacha kuishi kwa mazoea na badala yake wawe wakijiajiri ili kuepuka tatizo la ukosefu wa ajira.

Katika taarifa ambayo imetolewa na Shirika la Kazi Duniani (ILO), inaonyesha kuwa zaidi ya vijana 800,000 humaliza chuo kila mwaka na wanaokadiriwa kupata ajira rasmi ni 40,000 pekee hivyo kuonyesha ni jinsi gani kuna upungufu mkubwa wa ajira nchini.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni