Na Anna Nkinda – Maelezo, aliyekuwa Tarime
WAKAZI
wa wilaya ya Tarime wametakiwa kuachana na vitendo vya unyanyasaji wa
kijinsia hasa mila za ukeketaji na ndoa za utotoni kwa watoto wa kike.
Mwito
huo umetolewa hivi karibuni na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati
akizindua uboreshaji wa Hospitali ya wilaya ya Tarime iliyopo mkoani
Mara.
Mama
Kikwete alisema ukeketaji unaleta matatizo makubwa ikiwa ni pamoja na
kupata matatizo wakati wa kujifungua, mtoto wa kike kupata maumivu
makali wakati wa ukeketaji na pia kitendo hicho husababisha kutoka damu
nyingi na matokeo yake ni kifo.
“Wazazi
na walezi acheni mila hizi ambazo hazina faida kwa wakati huu na ni
ukiukwaji wa haki za binadamu bali wasomesheni watoto wenu wa kike ili
waweze kuwa walezi bora wa familia zao na jamii kwa ujumla”,
alisisitiza.
Aliendelea
kusema kuwa katika jamii baadhi ya wanawake wanadhalilishwa,
kunyanyasika kijinsia na kupata mateso ya aina mbalimbali kama vile
kupigwa, kunyimwa haki ya kumiliki mali na kutokuwa na maamuzi ya
matumizi ya mali ya familia hata kama wao ndiyo wazalishaji.
Alisema,
“Tabia hizi hazikubaliki kabisa katika Dunia ya leo.Mwanamke anayo haki
ya kumiliki mali kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu pia anayo haki ya
kufanya maamuzi ya pamoja kwa kile alichozalisha kwani mwanamke ni
binadamu na siyo chombo cha kuzalisha mali. Binadamu wote ni sawa”.
Kwa
upande wa watumishi wa kada ya afya aliwahimiza kufanya kazi kwa bidii
na weledi kwa kuzingatia kwamba miundombinu ya Hospitali hiyo
imeboreshwa lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora
za afya hususani akina mama , watoto na wazee.
Mama
Kikwete aliwaomba viongozi, kina baba na wadau
mbalimbali waliohudhuria uzinduzi huo kushirikiana kwa pamoja ili
kupunguza na hatimaye kuokoa kabisa vifo vya akina mama wajawazito na
watoto katika wilaya hiyo pia wahakikishe kina mama na watoto wanapata
huduma bora za afya.
“Akina
mama wajawazito wahudhurie kliniki muda wote wa ujauzio pia hakikisheni
wanajifungulia katika vituo vya afya na hospitali. Wapelekeni watoto
kliniki hadi watakapotimiza umri wa miaka mitano ili wapate kinga
wanazostahili”, aliwasihi.
Kwa
upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Tarime Dkt. Calvin
Mwasha alisema wazo la uboreshaji wa Hospitali hiyo liliasisiwa na Mkuu
wa wilaya hiyo Glorius Luoga alipofanya ziara Hospitalini hapo mwanzoni
mwa mwaka huu na kubaini kuna matatizo ya uchakavu mkubwa wa majengo.
Uchakavu
wa miundombinu ya maji safi na taka, ubovu wa mfumo wa umeme, uchakavu
wa vitanda na matandiko,uchakavu na uhaba wa vifaa tiba na vitendea
kazi, uhaba wa madawa, ukosefu wa jengo la utawala na upungufu wa
watumishi mbalimbali.
“Wadau
mbalimbali wa ndani na nje ya wilaya ya Tarime wakiwemo wafanyabiashara
wakubwa na wakati, wachimbaji madini wakubwa (ACACIA North Mara Gold
Mine) na wadogo, Taasisi za Umma na binafsi, watumishi wa Umma na
wananchi walifanikiwa kuchanga shilingi milioni 345, mashuka 80 na
vitanda tisa”, alisema Dkt. Mwasha.
Aliyataja
maboresho yaliyofanyika kuwa ni majengo ya wagonjwa wa nje, akina mama
na watoto, maabara, upasuaji ambapo mwanzo kulikuwa na chumba kimoja
cha upasuaji baada ya maboresho kuna vyumba vinne na jengo la upimaji
virusi kwa hiari (VCT).
Wodi
za wazazi, magonjwa ya akina mama na upasuaji, akina baba, TB wanaume
na wanawake, majengo ya jiko ambalo kwa sasa litatumika kama jengo la
kuhudumia wateja wa mifuko ya bima ya afya (CHF na NHIF) na jengo la
ufuaji.Ujenzi ambao bado kuanza ni Jengo la utawala na sehemu ya
kupumzikia wagonjwa.
Dkt.
Mwasha alisema kuna vifaa tiba mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya
shilingi milioni 263 ambavyo vimeagizwa kutoka China kupitia kwa
mwenyekiti wa maboresho Peter Zacharia. Kutokana na mahusiano yake
mazuri na wafanyabiashara wa huko vifaa hivyo ambavyo bado havijalipiwa
vimeshafika wilayani Tarime.
Baadhi
ya vifaa hivyo ni mashine ya standard stabilizer moja, oxygen
concentrator moja, vitanda 130, baiskeli za kubebea wagonjwa 20, mashine
ya kupimia full blood picture moja, BP Machine Digital 50 na nguo za
kuvaa wagonjwa.
Hospitali ya wilaya ya Tarime ilijengwa mwaka 1956 tangu kipindi hicho inahudumia wananchi wa wilaya hiyo, Serengeti na Rorwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni