MCHUNGAJI Christopher Mtikila ni Mwenyekiti wa chama cha Democratic Party (DP) ambacho kina usajili wa kudumu hapa nchini.
Mtikila alizaliwa mwaka 1950 mkoani Iringa, kusini mwa nchi yetu.
(Kwa
bahati mbaya, hadi nachapisha uchambuzi huu sikupata taarifa za elimu
yake) kwani hakuwa mwepesi kutoa ushirikiano mwezi mmoja uliopita
alisafiri kwenda nje ya nchi na kurejea wakati nikiwa katika hatua za
mwisho za uhariri.
Pamoja
na shughuli za siasa, Mchungaji Mtikila ni mwanzilishi na mkuu wa
kanisa la Kipentekoste la Full Salvation Church. Lakini pia kwa muda
mkubwa wa maisha yake amekuwa anajihusisha sana na harakati za haki za
binadamu kwa kupitia kitengo cha haki za binadamu cha kanisa hilo
kiitwacho “Liberty Desk”.
Kanisa lake ni moja ya makanisa machache sana hapa Tanzania yenye vitengo vya namna hiyo.
Umaarufu
wa Mtikila ulikua sana mwanzono mwa miaka ya 1990 kutokana na uwezo
wake mkubwa wa kuongea, upinzani wake dhidi ya muundo wa muungano kati
ya Tanganyika na Zanzibar, madai yake kuhusu kile anachokiita “uhujumu
wa uchumi unaofanywa na wahindi” (ambao anawaita Magabacholi), na kesi
mbalimbali za kikatiba alizokuwa akifungua katika mahakama za
Tanzania,ni kati ya mambo machache yaliyofanya asikike kila kona ya
nchi.
Kwa
muda mrefu chama chake cha DP hakikuweza kupata usajili wa kudumu
kutokana na kukataa kwake kuitambua Zanzibar, alikuwa akisisitiza kuwa
chama chake ni cha Tanganyika na sio Tanzania.
Hata
hivyo Mtikila ilimpasa abadili msimamo wake katika miaka ya hivi
karibuni kwa kukubali kutafuta wanachama toka Zanzibar (kama sheria ya
uchaguzi inavyotaka) na hivyo chama chake kilipata usajili wa kudumu.
Mtikila
alifungwa kwa mwaka mmoja mwaka 1999 baada ya kupatikana na hatia ya
kutoa maneno ya kashfa dhidi ya aliyekuwa katibu mkuu wa CCM, marehemu
Horace Kolimba.
Mwaka
2004 pia alihukumiwa kifungo kilichosimamishwa cha miezi sita kwa kutoa
maneno ya kashfa dhidi ya mkuu wa polisi wa wilaya ya Ilala. Kwa ujumla
maisha yake yamekuwa ni ya harakati muda wote, akipambana awezavyo,
akisimama kidete inavyowekana na akijikuta matatani kila uchwao. Mchungaji Mtikila amemuoa Bi. Georgia na wana watoto.
MBIO ZA UBUNGE
Mwaka
1997, Mbunge wa jimbo la Ludewa kwa tiketi ya CCM, Horace Kolimba
aliitwa na Kamati Kuu ya chama chake mjini Dodoma kwenda kujibu mashtaka
ya ndani ya chama juu ya kauli ambazo alikuwa akizitoa kwamba “CCM
imepoteza mwelekeo”, baadhi ya viongozi wa chama chake walimchukulia
kama msaliti na wengine wakimuona kama mtu aliyethubutu kusema ukweli
bila kumuhofia Nyerere.
Hata hivyo Kolimba alifariki hukohuko Dodoma katika siku ambazo alikuwa akihojiwa. Tume
ya Taifa ya Uchaguzi ilipotangaza kukuwepo kwa uchaguzi mdogo, ndipo
Mchungaji Christopher Mtikila, alikihama chama chake cha DP akajiunga
CHADEMA na kuomba ridhaa ya kugombea jimbo la Ludewa, Chadema ikampa
ruhusa hiyo.
Mtikila ni mzaliwa wa Ludewa na alifanya hivyo kwa sababu chama chake cha DP kilikuwa kimenyimwa usajili.
Uchaguzi
wa Marudio ulifanyika tarehe 25 Mei 1997 na kumpa ushindi mgombea wa
CCM Prof. Chrispin Haule Che Mponda. Prof Mponda alipata kura 20,111
dhidi ya kura 8,386 za Mchungaji Christopher Mtikila wa CHADEMA. Mgombea
wa NCCR ambayo haikuwa imejijenga vilivyo Ludewa, Barnabas Kidulile,
alipata kura 1,271.
Hata
hivyo, baada ya kushindwa uchaguzi huo, Mchungaji Mtikila alisikika
akihitilafiana na CHADEMA hadharani huku akiipa shutuma nzito nzito,
akafukuzwa kwenye chama hicho na ndipo akaendelea kuwekeza nguvu kwenye
mipango ya kukamilisha usajili wa chama chake.
MBIO ZA URAIS
Mtikila
alianza rasmi harakati za kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania mwaka 2005 kwa tiketi ya DP alikuwa kati ya wagombea 10 wa
nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo.
Katika
uchaguzi huo alipata kura asilimia 0.27 ya kura zote, akiwa nyuma ya
Jakaya Kikwete wa CCM (asilimia 80.28), Prof. Ibrahim Lipumba wa CUF
(asilimia 11.68), Freeman Mbowe wa CHADEMA (asilimia 5.88), Augustine
Mrema wa TLP (asilimia 0.75) na Dkt. Sengondo Mvungi wa NCCR (asilimia
0.49).
Kwenye
uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 Mtikila hakugombea nafasi ya Urais na chama
chake hakikuweka mgombea na kwa mwaka huu 2015 hajaweka msimamo wake
wazi japokuwa taarifa za ndani ya chama hicho zinaonesha kuwa kinaweza
kusimamisha mgombea na mtu huyo akawa ni Mtikila.
Nimemuweka
katika Orodha hii kwa sababu tayari anatajwa kuwa na sifa,vigezo na
hata historia ya mapambano inayompa nafasi ya kuweza kusimama mbele ya
watanzania kuomba uongozi wa juu.
NGUVU YAKE
Jambo
la kwanza ambalo bila shaka linampa Mtikila nguvu ikiwa ataingia kwenye
kinyang’anyiro cha urais ni umaarufu wake. Mtikila ni maarufu sana, si
kwa watu wenye umri wa zamani tu, lakini pia hata kwa vijana wadogo wa
sasa.
Ni
vigumu sana kama mtanzania yeyote anafuatilia masuala ya siasa katika
nchi au anafuatilia habari mara kwa mara na asimjue Mtikila. Ni kiongozi
anayejishughulisha na mambo mengi mno na harakati zilizopitiliza na kwa
mwanasiasa anayetaka nafasi ya juu, umaarufu unaweza kuwa karata
muhimu, la msingi tu umaarufu huo vichwani mwa watu uwe na maana ya
kumuona kama “mtu muhimu” katika hatua zake.
Lakini
jambo la pili linalompa nguvu na sifa zaidi, ni kazi kubwa ambayo
amekuwa akiifanya mara kwa mara, ya kufungua kesi za masuala ambayo
serikali inakuwa imewanyima raia kwa muda mrefu. Mara nyingi katika
siasa za Afrika, kesi za kuishtaki serikali kwa masula ambayo
yanaonekana kuwa makubwa huwa linaonekana kama jambo hatari hata kwa
usalama wa mhusika, Mtikila.
Kesi
za kikatiba ambazo amewahi kufungua ni pamoja kesi ya kutaka wagombea
binafsi kuruhusiwa katika uchaguzi Tanzania, wananchi wa Tanzania Bara
kuruhusiwa kwenda Zanzibar bila pasipoti, na vyama vya siasa kuruhusiwa
kufanya mikutano bila kuomba kibali toka kwa Mkuu wa Wilaya na polisi
n.k. Hebu tujiulize, ni vyama vingapi vya siasa vimewahi kuwa na
“uthubutu” huo?
Mtikila
alishinda kesi ya mgombea binafsi na aliiweka serikalini kwenye njia
panda kwa asilimia mia moja. Katika suala hili yeye ni mtu wa kujivunia
sana na kama upiganaji wa kiwango hiki peke yake ndiyo ungekuwa tiketi
ya urais basi Mtikila tayari angestahili tuzo hiyo bila mjadala. Hakuna
mwanasiasa mwingine yeyote hapa Tanzania aliyewahi kupambana na serikali
mahakamani kila kukicha kama Mtikila, hayupo!
Lakini
jambo la tatu linalompa nguvu na sifa ni ni Misimamo ya kipekee.
Mtikila hajali anapokuwa ana ajenda zake na misimamo yake na mara nyingi
misimamo hiyo huwa ni ya kipekee hata kama ni mibaya kiasi gani, yeye
huisimamia na kubakia nayo hata kama wenzake wote mtamkimbia.
Nakumbuka
tulipokuwa Bunge Maalum la Katiba, Mtikila alikuwa na ajenda ya
kusimamisha bunge lile lisifanye kazi kwa sababu limeanza kinyume na
sheria na halina hadi ya kutunga katiba ya nchi. Pamoja na wanasheria
wakongwe sana kuwa na mawazo tofauti naye, bado alishikilia msimamo wake
na aliondoka kwenda Dar Es Salaam kwa minajili ya kufungua kesi husika
(sina taarifa jambo hili lilipoishia).
Na
hata baadaye, vyama vinavyounda UKAWA vilipoamua kutonoka Bungeni,
Mtikila aliunga mkono uamuzi huo na alisisitiza kuwa yeye anafanya kazi
na umoja huo kwa suala la katiba, sijapata taarifa za hatma yake katika
kuendelea kuwa ndani ya UKAWA, lakini nachojua ni kwamba misimamo hii ya
Mtikila kuna wakati imekuwa na tija kubwa sana, si kwake tu bali kwa
taifa zima.
UDHAIFU WAKE
Udhaifu
wa kwanza wa Mtikila ni utoaji wa “Kauli tata” ambazo kuna nyakati
zinaudhi na kuamsha hasira ya upande uliotuhumiwa. Mtikila ana tabia ya
kuongea mambo magumu na mkishindana sana akakudharau huweza kukuita jina
baya sana ambalo hukuwahi kufikiri kuwa unaweza kuitwa au kupewa.
Mara
kadhaa amewahi kusikika akitoa shutuma kali sana kwa viongozi wa nchi,
vyama vya upinzani n.k. Sifa hii ya Mtikila si sifa sahihi sana kwa mtu
ambaye ana ndoto au anaotewa ndoto za kushika uongozi wa juu wanchi siku
moja.
Lakini
jambo la pili ambalo naliona kama udhaifu pia, Mtikila hupenda
kushughulikia mambo ya hatari peke yake na wakati mwingine bila kufanya
kazi ya kutosha kuwaelimisha wananchi na vyombo vya habari na kutafuta
hali ya kupewa uzito na mioyo ya wananchi na wadau.
Tabia
hii ya Mtikila ya kuamka na ajenda nzito mkononi na kulazimisha ajenda
anayotoa iungwe mkono ghafla bila kuwaandaa wananchi, siyo jambo zuri
kisiasa.
Kuna
masuala ya msingi sana anayapigania na yanapotoshwa na vyombo vya
habari, na wanasiasa wa vyama vingine n.k kwa sababu tu hakufanya kazi
ya siasa ya kuyatangaza masuala hayo, kuomba ushirikiano wa wenzake n.k.
Ili uwe kiongozi mzuri una wajibu wa kuwashirikisha watu waliokuzunguka
maamuzi makubwa unayotaka kuyafanya ili uungwe mkono. Kujifanyia peke
yako kunakuwa hakuna tija kubwa kwa maslahi mapana ya wote.
Na
mwisho, Mtikila amekuwa akitoa kauli zinazodhaniwa kuwa ni za kibaguzi
sana na hili haliko “uvunguni”, amefanya hivyo mara nyingi mno katika
mikutano yake na hata mbele ya vyombo vya habari.
Kuna
wakati amekuwa akisikika hadharani akiwatuhumu Wahindi kwa lugha za
kibaguzi sana, anawaita “Magabacholi”, lakini pia kuna wakati amewahi
kulalamikiwa hata na nchi jirani ya Rwanda kwa namna alivyowahi
kuyashutumu makabila makubwa ya nchi hiyo kwa kauli za kibaguzi.
Kiongozi
mmoja wa juu wa Serikali nimewahi kumsikia akisema kuwa alipokutana na
Rais Kagame wa Rwanda, baada ya salamu Kagame akamuuliza kiongozi huyo
“Who is Reverend Mtikila”? (Mchungaji Mtikila ni nani?). Mtikila siyo tu
kuwa alikua anaipa chemsha bongo Serikali hapa ndani, hata huko nje ya
nchi wanaumiza vichwa juu yake na hili siyo suala la kujivunia sana kama
kweli nchi inatafuta viongozi watakaoimarisha uhusiano na nchi za
jirani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni