Ndugu Wasamaria wema,
Tunapenda
kutumia fursa hii kuwapa updates kuhusu dada Joyce Mwambepo, mkaazi wa
Sinde jijini Mbeya mwenye umri wa miaka 27 ambaye anaishi na bibi yake
mwenye umri wa miaka 80 pamoja na mwanaye mwenye umri wa miaka 4.
Kwa
bahati mbaya mwezi April mwaka jana dada huyu alipata ajali ya kugongwa
na gari ambalo dereva wake hakusimama kumsaidia. Ila kwa msaada wa
wasamaria wema alipelekwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mbeya ambako
inasemekana alikaa kwa miezi mitatu bila kupata matibabu kwa kukosa
fedha. Katika
uchunguzi wa awali ilibainika kuwa Joyce amevunjika miguu yote miwili,
hivyo akahamishiwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili ambako pia baada
ya kukaa kwa miezi kadhaa alirejeshwa Mbeya baada ya kukosa pesa za
matibabu.
Baada
ya mwanahabari Deo Kakuru wa Mbeya kumgundua na kufanya juhudi za kutoa
taarifa za dada Joyce katika mitandao mbalimbali, wasamaria wengi wa
ndani na nje ya nchi wakaguswa na kuchangia. Mungu mkubwa, kiasi
kilichopatikana (kiasi cha 3.2m/-) kimewezesha dada Joyce kupelekwa Dar
es salaam toka Mbeya kwa ndege ya Fast Jet Alhamisi iliyopita na moja
kwa moja kupelekwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kupokelewa katika
kitengo cha MOI na kupatiwa kitanda katika wodi mpya ijulikanayo kama
Wodi ya Magufuli, ghorofa ya tatu chumba namba mbili.
Cha
kufurahisha ni kwamba Joyce aliweza kukaa kwenye kiti cha kusukumwa na
hata kwenye ndege aliketi kama kawaida, zoezi ambalo hata yeye anasema
limemsaidia kwani kwa mara ya kwanza hivi sasa ganzi miguuni inapotea
taratibu na ukimgusa anahisi mguso tofauti na ilivyokuwa awali.
Daktari
bingwa ameshaonana naye na kumpa matumaini ya kupona, hasa sehemu ya
chini ya uti wa mgongo wake ambao inasemekana una matatizo yaliyopelekea
kubana mishipa ya fahamu na kufanya miguu ipooze. Zoezi linalosubiriwa
kwa sasa ni kupatiwa vipimo vya MRI ili kubaini kiufasaha tatizo lake
na hatimaye kupatiwa matibabu. Zoezi hili linatarajiwa kufanyika wakati
wowote kuanzia sasa.
Mpiganaji
Deo Kakuru amesharejea Mbeya na kijiti cha kumwangalia dada Joyce
amekabidhiwa Ankal ambaye anaomba Wasamaria wema waendelee kumuombea na
kumsaidia kwa hali na mali dada huyu ambaye ni yatima.
Kwa
bahati njema Ankal alikutana na kuongea na Msamaria mwingine aitwaye
Mama Rozi ambaye anamuuguza mama yake mzazi aliyelazwa wodi moja na
dada Joyce. Msamaria huyu amekubali kumsaidia dada Joyce kwa chakula na
pia kumsaidia usafi maana hapo kitandani hawezi kuondoka.
Mungu
kweli ni mkubwa. Dada Joyce anatabasamu na kuongea vizuri tu. Anatoa
shukurani sana kwa wote waliomsaidia na wanaoendelea kumsaidia. Anasema
hana cha kuwalipa ila kusema ASANTE SANA na anamwomba Mola Muumba
awazidishie pale patapopungua. Ameomba anayeweza kumtembelea atafurahi
sana maana hana ndugu hapa Dar es salaam.Pia anawashukuru sana madaktari
waliomhudumia vyema katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya ambao
amesema hatowasahau kwa msaada wao.
Ankal amejitolea kuendelea kusaidia uratibu wa kufanikisha matibabu ya dada Joyce. Hivyo unaweza kuwasiliana naye kwa email issamichuzi@gmail.com ama whatsapp namba+255 754 271266 kwa jina la Ankal.
AU mratibu-mwenza Deo Kakuru Msimu
Pia unaweza kuwasiliana moja kwa moja na dada Joyce kwa namba
Mpiganaji Deo Kakuru akiwa na dada Joyce ndani ya FastJet wakitoka Mbeya keuelekea Dar es salaam
Dada Joyce akiwa ameketi kwa utulivu kwenye siti yake ndani ya ndege
Mpiganaji Deo Kakuru akiwa na dada Joyce mara baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es salaam
Msamaria
mwema Mama Rozi akimhudumia dada Joyce akiwa kitandani kwake Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili kitengo cha mifupa cha MOI katika wodi ijulikanayo
kama Wodi ya Magufuli ghorofa ya tatu
Dada Joyce akiwa wodini Moi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni