Na Teresia Mhagama, Mtera
Imeelezwa
kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya
kuendeleza miradi mbalimbali ambayo wananchi wameamua kuiendeleza
ikiwemo miradi ya uzalishaji umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali kama
maji,upepo, jua, nishati jadidifu, makaa ya mawe na mawimbi ya bahari.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
wakati wa kikao chake na wazalishaji wa umeme wa maji na wale wanaotaka
kuzalisha umeme huo chini ya megawati 20 kilichofanyika katika Kituo cha
Kuzalishia Umeme cha Mtera.
“Serikali
lazima iwe Msemaji wa wawekezaji hawa ili kuhakikisha wanapata fedha na
teknolojia za kuendesha miradi yao na hii itapelekea Taifa kuwa na
nishati ya kutosha kwani wawekezaji hawa sasa watakuwa na uwezo wa
kuzalisha umeme,” alisema Profesa Muhongo.
Ili
kufanikisha suala, Profesa Muhongo aliwataka wadau hao wanaotaka
kuzalisha umeme wa maji chini ya megawati 20 kuhakikisha kuwa wanaandika
na kuwasilisha wizarani mapendekezo yanayochanganua miradi wanayotaka
kuanzisha kabla ya mwisho wa mwezi huu ili litengenezwe kalabrasha
moja litakalotumika katika kuombea fedha kwa wafadhili mbalimbali na
Taasisi za Kifedha.
“Ifikapo
tarehe 28 mwezi huu mchanganuo wa mapendekezo yenu yawe yamemfikia
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Nishati ili serikali iangalie namna
ya kutafuta fedha zitakazowawezehsa kuendeleza miradi yenu ya umeme
badala ya mtu mmoja mmoja kuanza kuzunguka na maombi yake binafsi ya
kutafuta fedha kutoka Taasisi mbalimbali jambo linalochelewesha
upatikanaji wa fedha hizo, “ alisema Profesa Muhongo.
Profesa
Muhongo alisema kuwa tayari serikali imeshaanza majadiliano na Taasisi
za kifedha kama Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB), Benki ya Dunia
(WB) na nchi wahisani kwa ajili ya kupata fedha za kuendeshea miradi
mbalimbali ikiwemo ya Nishati ambapo alisema kuwa suala hilo litafanyika
kwa ufanisi endapo miradi yote inayoombewa fedha itajumuishwa katika
kalabrasha moja litakaloainisha miradi yote inayohitaji kuendelezwa.
Waziri
wa Nishati na Madini alisema kuwa kwa sasa serikali inazalisha umeme
kwa kutumia vyanzo mbalimbali ikiwemo gesi asilia (50%), maji (35%), na
mafuta mazito (15%) na kueleza kuwa Tanzania bado ina vyanzo vingi vya
kuzalisha umeme ambavyo vinahitaji wawekezaji makini ikiwemo upepo, joto
ardhi,makaa ya mawe na jua ili nchi iwe na umeme wa uhakika,
unaotabirika na wa bei nafuu.
“
Ndugu zangu tunapaswa kutekeleza miradi hii ya nishati kwa kasi kubwa
kwani Tanzania ni nchi mwananchama wa Mpango wa Umoja wa Mataifa wa
Nishati Endelevu kwa Wote (SE4ALL) ambao unaelekeza kwamba ifikapo mwaka
2030 kila mtu anapaswa kuwa na nishati ya umeme na sisi Tanzania ndio
tuliwakilisha nchi za Afrika kutengeneza Mpango huo, “ alisema Profesa
Muhongo.
Alisema
kuwa Mpango huo wa SE4ALL malengo yake makuu ni upatikanaji wa nishati
kwa wote ifikapo mwaka 2030, ongezeko la maradufu la utumiaji wa nishati
jadidifu na matumizi bora ya ya nishati.
Profesa
Muhongo alisema kuwa tayari ameshatia saini Mpango huo ambao utawezesha
Tanzania kufaidika na fedha zitakazotolewa ili kuendeleza miradi ya
nishati na kusema kuwa tayari Tanzania iko katika nafasi nzuri ya
kufaidika na Mpango huo wa SE4ALL na kutaka wawekezaji zaidi waendelee
kujitokeza ili kuendeleza miradi ya umeme nchini.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO),
Mhandisi Felchesmi Mramba, alisema kuwa Shirika hilo litaendelea kuwapa
ushirikiano wawekezaji hao wa umeme wa maji na wale wanaotaka kuanzisha
miradi hiyo ikiwemo kutoa msaada wa kitaalam ili kuongeza kiwango cha
nishati ya umeme nchini.
“TANESCO
itaendelea kutoa ushirikiano kwenu na naomba tuendelee kushirikiana ili
kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika uendelezaji wa
miradi hii na ninaomba mjitokeze zaidi na kuwekeza katika maeneo
mbalimbali ikiwemo Kigoma, Liwale na Loliondo sehemu ambazo bado
changamoto ya upatikanaji wa nishati hiyo ni kubwa.,”alisema Mhandisi
Mramba.
Naye
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Masoko na Teknolojia, kutoka Wakala wa
Nishati Vijijini (REA),Mhandisi Gissima Nyamohanga) alisema kuwa mpaka
sasa Wakala huo umeshatoa Dola za Marekani milioni 3.1 kwa ajili ya
upembuzi yakinifu kwa wajasiriamali wanaotaka kuwekeza katika miradi ya
nishati nchini.
Pia
Wakala huo umetoa Dola za Marekani milioni 5.4 kwa kampuni za
zilizoanza kuzalisha umeme ili waweze kuunganisha umeme huo kwa
wananchi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni