Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akizungumza wa waandishi wa
Habari kuhusu kuanza kwa Mwaka wa Sheria 2016, Wiki ya Sheria na Utendaji wa
Mahakama ya Tanzania kwa mwaka 2016. Wengine Kushoto ni Jaji Mkuu wa Zanzibar
Mhe. Omary Othman Makungu
(Kushoto) na Jaji Kiongozi Mhe. Shaaban Lila (kulia).
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman (kushoto) akiwa ameambatana na Jaji
Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omary Othman
Makungu (Katikati) na Jaji Kiongozi Mhe. Shaaban Lila (kulia) wakielekea
kwenye mabanda ya Maonesho ya Wiki ya Sheria kwa mwaka 2016 katika viwanja vya Mnazi Mmoja ambapo kilele
cha Wiki hiyo kitakuwa Februari 4 2016 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Baadhi
ya Wananchi wakipata huduma katika mabanda ya maonesho wakato wa Maadhimisho ya
Wiki ya Sheria.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akitembelea banda la maonesho la
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Wakati
wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini leo viwanja vya Mnazi mmoja.
Na Aron Msigwa – MAELEZO
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman amesema kuwa Mahakama ya Tanzania itawachukulia
hatua za kinidhamu na za kisheria Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo,Wilaya na wale
wa Mahakama za Hakimu Mkazi wapato 508 kote nchini waliotekeleza majukumu yao chini
ya kiwango na kushindwa kutimiza wajibu wa Mahakama wa Utoaji wa Huduma Bora kwa
wananchi katika mwaka wa Sheria wa 2015/2016.
Akizungumza
na waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam alipokua akitoa ufafanuzi kuhusu
kuanza kwa mwaka mpya wa Sheria wa 2016
na Maadhimisho ya Wiki ya Sheria ambayo kilele chake kitakua Januari 4,2016 Mhe.Othman amesema kuwa kwa mujibu wa taratibu
za uendeshaji wa Mahakama na upimaji wa viwango vya
utendaji kazi vilivyowekwa, Mahakimu hao wa Mahakama za wilaya na Hakimu Mkazi
121 na 387 wa Mahakama za Mwanzo watatakiwa kutoa maelezo ndani ya siku 7 juu ya sababu
zilizowafanya washindwe kutimiza lengo lililowekwa la kushughulikia mashauri
260 kila mmoja.
Amesema
watakaothibitika kamati za nidhamu na maadili
za kila wilaya na Mikoa ambazo ni Kamati ndogo za Tume ya Utumishi wa Mahakama
zitawafungulia kesi za kinidhamu ndani ya siku 21.
“Wale
watakaobainika watakumbwa na adhabu ya kupewa Onyo, kushushwa vyeo na kufukuzwa
kazi ili iwe fundisho kwa wengine, ninajua wapo baadhi ambao waliajiliwa
katikati ya mwaka, wengine kwenda mafunzo ya vitendo vyuoni, wajawazito na
baadhi vituo vyao kuwa na kesi chini ya 260 kwa mwaka” Amesisitiza.
Aidha,
katika hatua hiyo amewapongeza Mahakimu waliofanya vizuri katika utendaji wao
wakiwemo 14 walioshughulikia mashauri zaidi ya 700 kila mmoja, Mahakimu 50 walioamua
kesi zaidi ya 500 kila mmoja baadhi wakitokea wilaya ya Mkuranga, Rufiji na Bukoba mjini na wengine wawili kutoka Dar
es salaam walioamua kesi zaidi ya 900 kila mmoja na kuvuka lengo la utendaji lililowekwa la
kushughulikia mashauri 260 kwa mwaka.
Akitoa
tathmini ya utendaji wa Mahakama kwa mwaka wa sheria uliopita amesema kuwa
Mahakama ya Tanzania ina Mahakama za Hakimu Mkazi kila Mkoa na Mahakama za
Wilaya 111 katika wilaya za Kiserikali 133 pamoja na Mahakama za Mwanzo ambazo hupokea
asilimia 93 ya mashauri yanayofunguliwa kote nchini.
Amesema mwaka 2015 Mahakama zote nchini zilipokea
jumla ya mashauri 206,115, kati ya hayo mashauri 220,815 yaliamuliwa kukiwa na
ziada ya mashauri 14700 jambo linaloonyesha kuwa Mahakama zinapokea mashauri na
kuyashughulikia kwa kasi inayoridhisha huku mashauri yanayosababisha mrundikano
ni yale yaliyo nje ya idadi iliyopangwa.
Ameongeza
kuwa katika katika kipindi cha mwaka huo wa 2015 Mahakama za Mwanzo zilipokea
mashauri 141,025 ambapo kati ya hayo Mashauri 149,757 yalishughulikiwa huku
idadi ya Mahakimu walioshughulikia mashauri hayo ni 1240.
“Ukiangalia
mwenendo wa ufunguaji wa mashauri yote kote nchini hasa Tanzania Bara utagundua
kuwa Mahakama za Mwanzo, Wilaya na zile za Hakimu Mkazi zinapokea mashauri mengi kwa asilimia 93 ,katika
kila mashauri 4 yanayofunguliwa nchini 3 yako mahakama za mwanzo ambako
wananchi wengi wanatafuta ufumbuzi wa kesi zao lazima tuweke mkazo” Amesema
Jaji Mkuu Mhe.Othman.
Kuhusu
kuanza kwa mwaka mpya wa Sheria mwaka 2016 amesema Mahakama inauanza chini ya
Kauli Mbiu Isemayo “Huduma Bora kwa Wananchi ni Wajibu wa Mahakama na Wadau
wake” ikiwa na kesi 20,431
ikilinganishwa na 34,126 ilizoanza nazo mwaka 2015 na kuongeza kuwa licha ya
changamoto zinazoikabili Mahakama ya Tanzania mkakati uliopo ni kupunguza idadi
hiyo hadi kufikia 0 kwa kila mwanzo wa mwaka wa sheria.
Akitoa
ufafanuzi kuhusu upatikanaji wa Nakala za hukumu amesema Serikali inaendelea
kuijengea uwezo wa kifedha Mahakama wa kuajiri wachapaji wa nakala wengi zaidi ili
Nakala za Hukumu za Kesi ziweze kupatikana pindi tu kesi zinapomalizika katika
mahakama zote nchini tofauti na ilivyo sasa ambapo hupatikana Mahakama Kuu na
Mahakama za Rufani
Aidha,
amesema Mahakama inaendelea kuboresha miundombinu yake ikiwemo majengo na ujenzi
wa mahakama mpya katika maeneo yasiyo na huduma hiyo katika mwaka 2016. “ Hivi
sasa tuna wilaya 23 hazina Majengo ya Mahakama za wilaya, kwenye baadhi ya
maeneo kesi zinasikiliziwa Ofisini kwa Hakimu wakati ilitakiwa ziwe kwenye jengo
lenye ukumbi wa wazi,tumejiandaa kwa michoro ya majengo kwa mahakama zote ili
tuanze kujenga kwa gharama nafuu”
Mhe.
Othman ametoa wito kwa wananchi kutosita kuitumia Mahakama ya Tanzania katika
kupata ushauri wa kisheria kupitia wataalamu wake, kuhudhuria maonesho
mbalimbali ya kisheria yanayofanyika nchini huku akitoa angalizo kwa baadhi ya
watu wanaochangia kuwepo kwa mrundikano wa kesi kwa kufungua kesi za madai au
kupeleka mashauri Mahakamani kama sehemu ya maegesho ya masuala yao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni