Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akimshukuru Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kwa kutimiza ahadi yake
ya kuipatia Mahakama kiasi cha shilingi Bilioni 12.3 zitakazotumika
katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo uboreshaji
wa miundombinu ya Mahakama na ujenzi wa Mahakama mpya katika maeneo
mbalimbali nchini. Kulia ni Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison
Mwakyembe na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango (kushoto).
Waziri
wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe (wa pili kutoka kushoto)
akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa Habari kuhusu Serikali kuendelea
kushirikiana na Mahakama ya Tanzania ili kuwezesha ufanisi wa shughuli
zake.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman amemshukuru Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kwa kutimiza ahadi yake
ya kuipatia Mahakama kiasi cha shilingi Bilioni 12.3 alizoahidi wakati
wa maadhimisho ya Siku ya Sheria Februari 4, 2016 jijini Dar es salaam.
Amesema
Fedha hizo zitatumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
maendeleo ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama na ujenzi wa
Mahakama mpya katika maeneo mbalimbali nchini.
Akitoa
shukrani hizo leo jijini Dar es salaam Mhe.Othman amesema kuwa kwa mara
ya kwanza tangu mwaka 2012 Mahakama imepata asilimia 100 ya fedha zote
za Maendeleo zilizokasimiwa na Bunge kwenye Bajeti yake ya mwaka
2015/2016.
Amesema
kupatikana kwa fedha hizo ambazo ni za Maendeleo kutasaidia kufufua
miradi ya ujenzi iliyosimama, kufufua Mahakama ambazo zilikua hazifanyi
kazi kwa sababu ya uchakavu na kuipatia Mahakama fursa zaidi ya kutoa
huduma bora kwa wananchi kwa kuwasogezea huduma za Haki karibu katika
maeneo wanayoishi.
Mhe.Othman
ameeleza kuwa kwa kipindi cha bajeti za miaka 3 mfululizo kuanzia mwaka
2012 /2013 hadi 2014/2015 Mahakama ilikua ikipokea fedha pungufu ya
kiasi kilichopangwa katika Bajeti hali iliyochangia kuzorota kwa
shughuli za Mahakama.
”
Kwa mara ya kwanza Mahakama tumepata asilimia 100 ya Bajeti yetu ya
mwaka 2015/2016 kutoaka Serikalini, mwaka 2012/2013 tulipata shilingi
bilioni 26.9 ikiwa ni pungufu ya bajeti yetu kwa asilimia 78, mwaka
2013/2014 tukapata Bilioni 42.7 pungufu kwa asilimia 82 na mwaka
2014/2015 tulipewa shilingi bilioni 41.5 ambayo ni pungufu kwa asilimia
92 “
Akizungumzia
miradi ya ujenzi wa majengo mapya ya Mahakama amesema kuwa tayari
Mahakama ina michoro ya ramani za majengo yatakayojengwa katika maeneo
mbalimbali ambayo hayakuwa na huduma hiyo ikiwemo mikoa 12 kati ya 25
ambayo haina Mahakama Kuu, wilaya 22 kati ya 133 ambazo hazina Mahakama
za Wilaya pamoja na kuongeza Mahakama za Mwanzo ambazo ziko 976 kufikia
kata zote 3,957.
Kuhusu
Mradi wa ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama utakaofanyika
katika uwanja wa Chimala jijini Dar es salaam amesema utahusisha
maeneo mbalimbali ya utoaji huduma za Kimahakama na kuongeza kuwa
Mahakama itajenga jengo lenye viwango kwa kuwatumia Wakandarasi na
wataalam wa kitanzania watakaojenga Mahakama nzuri na yenye viwango kwa
gharama nafuu.
“Mahakama
tutatoa kipaumbele kwa wataalam wetu wa ndani ili waweze kutujengea
Mahakama zetu, tunalenga kuwafikishia huduma zetu katika maeneo
wanayoishi tunao mfano mzuri wa Mahakama ya mwanzo ya Dumila iliyoko
Morogoro, Mahakama hii imejengwa kijijini ni ya kisasa” Amesisitiza
Mhe.Othman.
Kwa
upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe amesema
kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama ya Tanzania ili
kuwezesha ufanisi wa shughuli zake kwa kuhakikisha kuwa kiwango cha
fedha za Bajeti kinachopitishwa kwa ajili ya kuhudumia shughuli za
Mahakama kinafika kwa wakati.
Akizungumzia
kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi, amesema uanzishwaji wake
uko katika hatua nzuri na wakati ukifika wananchi watataarifiwa kama
ilivyoahidiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuungwa
mkono na Mahakama ya Tanzania.
Naye
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, akizungumzia fedha za
Maendeleo zilizotolewa na Mhe.Rais amesema kuwa lengo la ahadi ya Rais
kwa Mahakama ilikua ni kuhakikisha Haki inapatikana kwa wananchi kwa
Wakati na kwamba miongoni mwa vitu vilivyokua vikichelewesha haki kwa
watanzania walio na mashauri Mahakamani ni ukosefu wa fedha na uchakavu
wa miundombinu.
Amesema
Serikali inaendelea kujenga uwezo wa kifedha ili kuimarisha huduma
katika mihimili yote ikiwemo Bunge na Mahakama huku msisitizo ukiwekwa
katika kukusanya mapato ya ndani.
“Kwa
kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) tuna dhamira ya dhati
ya kukusanya mapato ya ndani ili kujenga uwezo wa Serikali tutawabana
wote waliokuwa wanakwepa kulipa kodi na hili tutalisimamia kikamilifu”
Amesema
utoaji wa Haki ni moja ya ukuzaji wa maendeleo ya nchi na kuongeza kuwa
Mahakama ya Tanzania inafanya kazi nzuri pamoja na ufinyu wa bajeti
yake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni