Mkurugenzi
Mtendaji kutoka Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Kibo Mining, Louis
Coetzee ( wa pili kutoka kulia) akielezea mikakati ya kampuni hiyo
katika uwekezaji wa uzalishaji wa umeme kwa kutumia makaa ya mawe mbele
ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo na Watendaji
kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake.
Waziri
wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo ( kulia) akimweleza
Mkurugenzi Mtendaji kutoka Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Kibo Mining,
Louis Coetzee (kushoto) fursa za uwekezaji nchini kwenye sekta ya
umeme.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akisisitiza jambo katika kikao hicho.
Mkurugenzi Mtendaji kutoka Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Kibo Mining, Louis Coetzee akifafanua jambo katika kikao hicho.
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam.
Waziri
wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amezitaka taasisi
zinazosimamia miradi ya umeme nchini kuongeza kasi ya utendaji kazi
ili Tanzania iweze kupata umeme wa uhakika.
Profesa
Muhongo aliyasema hayo katika kikao chake kilichokutanisha Kampuni ya
Uchimbaji Madini ya Kibo Mining na watendaji kutoka Wizara ya Nishati
na Madini, Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Shirika la Madini la
Taifa (STAMICO), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wizara ya
Nishati na Madini.
Alisema
kuwa ili nchi iweze kuwa na umeme wa uhakika unaozalishwa kwa wakati ni
lazima taasisi zilizopo chini ya Wizara zikahakikisha zinaongeza
kasi katika uwekezaji kwenye uzalishaji wa umeme kwa kushirikiana na
wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wenye vigezo ili uchumi wa nchi
uweze kukua kwa kasi na kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa
ya Mwaka 2025 ambayo ni kuhakikisha kuwa nchi inatoka katika kundi la
nchi masikini duniani na kuingia katika kundi la nchi zenye kipato cha
kati ifikapo mwaka 2025.
Alisisitiza
kuwa ili kufikia lengo hilo ni lazima taasisi zikaongeza kasi katika
miradi yake ya umeme, kwa kushirikiana na wawekezaji mbalimbali na
kuwataka kuondoa urasimu kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kwenye
miradi ya uzalishaji wa umeme nchini.
Aliongeza
kuwa nishati ni roho ya uchumi wa nchi na kusisitiza kuwa hakuna nchi
yoyote duniani iliyopiga hatua bila kuwa na nishati ya umeme ya uhakika.
“
Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuhakikisha kuwa sekta ya
viwanda inakua kwa kasi na kutoa ajira hivyo kuchangia ukuaji wa
uchumi wa nchi, hivyo nishati ya umeme inahitajika sana; bila nishati
ya uhakika uchumi hauwezi kukua kwa kasi inayotakiwa,’ alisisitiza
Profesa Muhongo.
Waziri
Muhongo aliendelea kusema kuwa nishati ya umeme ya uhakika itachangia
ukuaji wa sekta za viwanda vidogo hasa maeneo ya vijijini, kilimo
kukua kwa kasi na hivyo kunufaisha wananchi na pato la taifa kukua
kwa kasi.
Aidha
Profesa Muhongo alilitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kushirikiana
kwa pamoja katika hatua zote za uwekezaji nchini ili kuondoa
mkanganyiko unaoweza kujitokeza kati ya serikali na wawekezaji.
“TANESCO
na EWURA naomba mshirikiane katika kila hatua, kwa kukaa meza moja na
wawekezaji na kufikia mwafaka kabla hawajaanza kuwekeza”, alisema
Profesa Muhongo
Awali
Mkurugenzi Mtendaji kutoka Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Kibo
Mining, Louis Coetzee akizungumza katika kikao hicho, alisema kuwa
kampuni ya Kibo Mining ina mpango wa kuwekeza katika uzalishaji wa
umeme kwa kutumia makaa ya mawe ambapo itaanza na ujenzi wa mtambo wa
kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe wa Megawati 900 kwa awamu
tofauti.
Alisema
awamu ya kwanza ambayo ni ujenzi wa mtambo wa kuzalisha Megawati 300
utakaogharimu Dola za Marekani milioni 800 utakamilika ifikapo mwaka
2019.
Akielezea
hatua iliyofikia ya maandalizi ya uwekezaji wa kampuni ya Kibo Mining
Coetzee alisema kuwa kampuni hiyo iliyoanza maandalizi yake mwaka 2008
inakamilisha upembuzi yakinifu (feasibility study) katika mradi wake
na kuongeza kuwa wana mpango wa kuanza ujenzi wa awamu ya kwanza mwaka
2017 baada ya taratibu zote kukamilika.
Alisema
mara baada ya ujenzi wa mtambo wa kwanza kukamilika mwaka 2019, umeme
utakaozalishwa mbali na kutumika viwandani utaongezwa kwenye gridi ya
taifa na hivyo kupunguza changamoto ya ukosefu wa umeme nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni